Maagizo makuu 3 ya Rais Magufuli kwa watendaji serikalini
Maagizo hayo ni pamoja na kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini na kuongeza ubunifu katika maeneo yao ya kazi ili kuboresha maslahi ya watanzania.
- Amuagiza Waziri mpya wa madini Dotto Biteko kuhakikisha anasimamia uanzishwaji wa vituo vya ununuzi wa madini kwenye maeneo ya migodi.
- Awapa changamoto watendaji wa Serikali kuongeza ufanisi na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
- Wizara ya madini, BOT kuanza ununuzi wa dhahabu kukabiliana na utoroshaji wa madini hayo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaapisha viongozi wapya wa wizara walioteuliwa na kutoa maagizo makuu matatu ikiwemo kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini na kuboresha ubunifu katika maeneo yao ya kazi ili kuboresha maslahi ya watanzania.
Maagizo hayo aliyoyatoa leo (Januari 09, 2019) Ikulu jijini Dar es Salaam yameelekezwa kwa mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali aliowateua jana ambapo amesema wanatakiwa waanze kuyafanyia kazi mara moja katika wizara zao ili kuongeza tija kwa wananchi.
Katika agizo lake la kwanza ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi na wizara ya madini inayoongozwa na Dotto Biteko, ni kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo yenye migodi ukiwemo mji wa Geita ambao una wachimbaji wengi wadogo wadogo wa dhahabu.
Ameleza sheria ya madini ya mwaka 2017 inaelekeza kuanzishwa kwa vituo hivyo lakini mpaka sasa bado havijajengwa katika maeneo mengi, jambo linalokwamishwa Serikali kupata mapato na wananchi kunufaika na rasilimali za madini.
“Najua kwenye sheria inatakiwa kuanzishwa kwa ‘mineral centers’ (vituo vya madini) lakini tujiulize, zimeanzishwa ngapi? Ziko wapi? Waziri wa Madini Dotto Biteko naomba uanze na suala la kuanzisha vituo vya madini, kwenye maeneo ya migodi,” amesema Rais.
Sambamba na hilo imeitaka wizara ya madini kushirikiana na wizara ya fedha na mipango pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhakikisha wanaratibu zoezi la ununua dhahabu ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha BoT kuwa na hifadhi ya kutosha.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na jitihada za kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu kuongeza uzalishaji lakini kwa sehemu kubwa mapato yake hayajulikani yanakwenda wapi.
“Kama tuna maeneo mengi ya kuchimba dhahabu, Je, Tumejiuliza sisi wizara ya madini wanapochimba wanauza wapi? Na kama wanachimba wanauza hiyo hela sisi percentage (asilimia) tunapata kiasi gani?” amesema Rais huku akihoji utekelezaji wa Sheria ya madini ambayo imeweka wazi ushirikishwaji wa wadau mbalimbali na jinsi wanavyonufaika na rasilimali hiyo.
Amesema watendaji wa wizara mbalimbali wanapaswa kuongeza ufanisi na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili maslahi ya watanzania ya kupatiwa huduma bora za afya, elimu, maji yatimie kwa wakati.
Zinazohusiana:
- Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage, joto la korosho likipanda
Katika hafla hiyo ya kuapisha iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, Rais ameweka wazi kuwa hata sita kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri ikiwa hataridhishwa na utendaji wa wizara husika.
“Mimi nitaendelea kufanya mabadiliko, kila mahali ambapo nitakuwa sikuridhika anayehusika ataondoka hata Biteko nimekuteua lakini nikiona haparidhishi utaondoka,” amesisitiza.
Msisitizo wa Rais wa kutokuwavumilia watendaji wazembe umekuwa ukifanyika mara kwa mara ambapo Novemba 10, 2018 aliwafuta kazi mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo na Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwasababu walishindwa kuwajibika katika nafasi zao hasa kusimamia bei ya korosho na kahawa.
Bado swali linabaki ni nani mwingine ataondolewa katika nafasi yake kabla ya Rais Magufuli hajamaliza muda wake mwaka 2020?
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amewapongeza viongozi walioteuliwa na kubainisha kuwa Serikali inaamini kuwa wataongeza nguvu katika utekelezaji wa majukumu ili kuwaleta wananchi maendeleo.