Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
Wadau hao wamesema hatua hiyo imekuja kufuta kilio cha muda mrefu cha kuwa na wizara maalum inayoshughulikia masuala ya uwekezaji.
Angela Kairuki ambaye ni Waziri mpya wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, atakayeshughulikia Uwekezaji, atakuwa na kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Picha| Mtanzania.
- Wadau hao wamesema hatua hiyo imekuja kufuta kilio cha muda mrefu cha kuwa na wizara maalumu inayoshughulikia masuala ya uwekezaji.
- Kairuki apewa changamoto ya kuboresha utendaji TIC ili kuongeza kasi ya uwekezaji nchini.
- Rais pia amefanya uteuzi wa makatibu wakuu wanne, makatibu wawili na kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba ambapo balozi wake atatangazwa baadae.
Dar es Salaam.Kufuatia Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kumteua Angela Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, atakayeshughulikia Uwekezaji, wadau wa sekta binafsi wamesema ni hatua kubwa katika kufuta kilio cha muda mrefu cha kuwa na wizara maalum ya uwekezaji.
Kabla ya uteuzi huo, Kairuki alikuwa waziri wa madini, nafasi inayochukuliwa na Doto Biteko ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo. Biteko atasaidiwa na Stanlaus Nyongo ambaye walikuwa pamoja katika nafasi hiyo kabla ya mabadiliko.
Akitangaza teuzi hizo (Januari 8, 2019) Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema Rais pia amefanya uteuzi wa makatibu wakuu wanne, makatibu wawili na kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba ambapo balozi wake atatangazwa baadae.
Wateuliwa hao na sehemu walizopelekwa ni pamoja na Mhandisi Joseph Nyamuhanga (Katibu Mkuu Tamisemi), Dk. Zainabu Chaula (Katibu Mkuu Afya) na Elinsi Mwakalinga (Katibu Mkuu Ujenzi).
Weingine ni Doroth Mwaluko (Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uwekezaji), Dk Doroth Gwajima (Naibu Katibu Mkuu Tamisemi) na Dk Francis K. Michael (Naibu Katibu Mkuu Utumishi).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye ameiambia nukta.co.tz kuwa uteuzi huo umekuja wakati mwafaka ikizingatiwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipagania kuwa na wizara inayojitegemea ya uwekezaji ambayo haichangamani na shughuli nyingine.
“Tulikuwa tunataka siku zote tuwe huru kabisa tusiwe chini ya waziri gani fulani, sisi kwa upande wetu kama sekta binafsi tumepata habari nzuri, Rais ametusikia hata kama ameipeleka katika Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Simbeye.
Amesema hatua hiyo itasaidia kutatua changamoto za uwekezaji nchini, ikizingatiwa Waziri aliyeteuliwa utakuwa na uwanja mpana wa kushughulikia masuala yote yanayohusu uwekezaji kwa ukaribu ikiwemo kufanya kazi na TPSF.
Zinazohusiana:
Kwa mujibu Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia mwishoni mwa mwaka 2018 inaonyesha kuwa Tanzania inazidi kuporomoka katika urahisi wa kufanya biashara duniani, jambo linaloweza kuleta changamoto katika kuvutia wawekezaji nchini.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la Urahisi wa kufanya Biashara (Doing Business 2019) imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 144 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani ikiwa imeshuka nafasi 7 kutoka 137 mwaka 2018. Na ndiyo mwaka ambao imefanya vibaya zaidi ukulinganisha na miaka mitano iliyopita.
Kulingana na vigezo vya ripoti hiyo, Tanzania imeangushwa na mchakato mrefu wa upatikanaji wa vibali vya ujenzi, leseni, usajili wa biashara na changamoto za ulipaji kodi.
Kairuki amepewa majukumu mapya ya uwekezaji ikiwa umepita zaidi ya mwezi mmoja tangu Rais Magufuli atengue uteuzi wa Charles Mwijage aliyekuwa akisimamia wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kwa kushindwa kusimamia majukumu ya wizara hiyo ikiwemo bei ya korosho na kahawa.
Simbeye amesema mambo muhimu ambayo yanapaswa kushughulikiwa katika siku za kwanza za Kairuki katika wizara hiyo ni kuongeza ufanisi na utendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuwafikia wawekezaji wengi wa ndani na nje wenye nia ya kuwekeza nchini.
Amesema hatua hiyo iende sambamba na kuongeza ofisi katika mikoa yote nchini ili kurahisisha uhusiano na kuwafikia wadau wa sekta binafsi wakiwemo wazalishaji wanaopatikana nchi nzima.
“La kwanza ninalomwambia apiganie kufanya kituo kiwe na uwezo na watumishi wa kutosha, wawekezaji wako nchi nzima tungependa kuwe na kituo kila mkoa na kanda. Angalie kwa namna gani anaboresha uwezo wa vituo vya uwekezaji kwasababu bila ya hivyo hataweza kutimiza malengo,” amesema Simbeye.