October 6, 2024

Ufungaji viremba unavyompaisha mwanadada Judith Laizer kimataifa

Anatumia fursa ya watalii wanaokuja nchini kuwauzia viremba vya kichwani na kutangaza utamaduni wa Tanzania kimataifa.

Judith Laizer anaamini kujitangaza ndiyo msingi wa kukuza biashara na kuwafikia wateja waliokusudiwa. Picha| Mesisisi Headwarps. 


  • Pia anatumia fursa ya watalii wanaokuja nchini kuwauzia viremba vya kichwani na kutangaza utamaduni wa Tanzania kimataifa.
  • Anaamini mitandao ya kijamii ndiyo msingi wa kukuza biashara na kuwafikia wateja wengi. 
  • Anawashauri vijana kufanya kazi na majaribio ya kutosha ili kufika wanapopataka.

Dar es Salaam. Unaposikia ubunifu wa mavazi, moja kwa moja unaweza kuhisi ni gauni, suruali au nguo yoyote ya kuvaa mwilini, lakini wengi huwa wanasahau kuhusu vitambaa au viremba vya kichwani kama moja ya vazi linalotumiwa zaidi na wanawake kama njia ya kujisitiri, fasheni au urembo ili kuwa na muonekano unaovutia.

Wapo ambao wanatumia fursa hiyo kujiajiri kwa kutengeneza na kuwafunga wanawake wenzao kwa mitindo mbalimbali ili kujiongezea kipato cha kuendeleza maisha yao. 

Kwa Tanzania huwezi kutaja wabunifu na wauzaji wa vitambaa vya kichwani bila kumtaja Judith Laizer mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa duka la mtandaoni la Mesisisi Fashion akitoa huduma ya kuuza na kufunga watu viremba.

Njia anayoitumia Judith ni kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii hasa instagram  ambapo ameweza kuwafikia watu wengi na kuitumia biashara yake kutangaza utamaduni wa mtanzania kimataifa. Lakini pia bidhaa zake vimekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea Tanzania kila mwaka.


Zinazohusiana:


Kutokana na kuwapa kipaumbele vijana wanaochipukia katika ujasiriamali na ubunifu, nukta.co.tz tunakuletea mahojiano iliyofanya na mwanadada huyo kuhusu biashara ya viremba ambayo inaweza kufungua milango kwa vijana ambao wana ndoto za kujiajiri kupitia ubunifu wa mavazi.


Nukta: Karibu Judith, tungependa kujua safari yako ya kuuza na kufunga viremba ulianza lini?

Judith: Asante sana, well safari yangu ya kuingia katika kuuza viremba nilianza mwaka 2016, ilianza kwa kupenda alafu ikaja biashara. Nilikuwa napenda kwasababu nilikuwa mvivu kusuka hivyo nikawa nataka kuwa na muonekano mzuri bila kuvaa mawigi au kusuka nywele za bei na nilitaka wasichana wawe na njia nyingine ya kupendeza.

Nukta: Ilikuaje mpaka umefika hatua hii ya kupata soko kubwa la bidhaa zako wakiwemo watalii toka nchi za nje?

Judith: Haikuwa rahisi kusema ukweli, na nilitengeneza mpango wa biashara, kujua wateja wangu ni kina nani na nitawatoa wapi na hata muda mwingine nilitoa bure kwasababu nilijua nahitaji nini na nikuwe kwa kiasi gani na matumizi ya mitandao ya kijamii yamenisaidia sana.

Wazo la kufanyia ‘branding’ lilianza nilipotaka biashara yangu ifahamike zaidi kwasababu ukifanya ‘Packaging’ (ufungishaji) unaviongezea bidhaa thamani hivyo nikafanya hivyo kwa kuweka lebo na nembo yangu katika bidhaa zangu.

Nukta: Unapata wapi malighafi za vitambaa vyako?

Judith: Malighafi napata hapa hapa Tanzania, nyingine nafanya oda kwa njia ya mtandao kutoka China na Dubai ambao wana malighafi nzuri za vitambaa na huwa nachagua rangi nzuri ninazozipenda au wanazozipenda wateja wangu zinazoendana na uafrika.

Bidhaa za Mesisisi zimefanyiwa ubunifu ambao unampelekea aweze kuuza sehemu yoyote na wakati wowote kwa wateja wake. Picha|Judith Laizer.

Nukta: Soko la bidhaa zako linawafikia watu gani ikizingatiwa kuwa kila biashara ina watu wake waliokusudiwa?

Judith: Wateja wangu wamegawanyika nusu kwa nusu, kuna wateja wangu ni watalii ambao hupenda kuvaa vitambaa wakiwa beach (ufukweni) na wanajivunia sana kununua vitu vya watanzania  na wengine ni wasichana najua utashangaa ila ni wateja wangu wakubwa hasa wale wanaotaka kuwahi asubuhi iwe kwenye kikao, kazini, vyuoni au matembezini.

Nukta: Mpaka sasa umewavalisha mastaa wangapi ambao unajivunia kufanya nao kazi?

Judith: Nimemvalisha Hamisa Mobetto alipokuwa balozi wa lipstick, Mhe Jokate Mwegelo (Mkuu wa wilaya ya Kisarawe), Shilole, Vanessa Mdee na pia nimevalisha model () kwenye ile video ya shukrani ya Godluck Gozbert.

Nukta: Unawashauri nini vijana hasa wasichana ambao wamemaliza masomo au wapo tu nyumbani na hawajishughulishi na chochote?

Judith: Niwashauri tu wajaribu kufanya vitu mbalimbali kwa sababu muda huu wa ujana ni nafasi ya kujaribu kama unataka kuajiriwa au kujiajiri. Huu ni muda wao wafanye kazi na majaribio ya kutosha, uzeeni wasije kupata shida.