November 24, 2024

Mambo ya kufanya kumuandaa mwanafunzi kuanza masomo 2019

Hakikisha unachunguza afya ya mtoto wako na kumjengea mazingira ya kumka mapema ili kumuanda kiakili kwenda shuleni.

  • Anza kumuandaa kwa kuamka mapema ili aweze kuzoea hadi shule itakapofunguliwa.
  • Jipe muda wa kuijua vizuri shule anayoenda mtoto wako na taarifa zake ili kumuandalia mazingira mazuri ya kusoma.
  • Hakikisha unachunguza afya ya mtoto wako kabla hajaanza shule.

Kutoka likizo na kurudi katika majukumu ya kawaida huwa siyo kazi ndogo, mwili unakuwa umezoea kupumzika hivyo kuurudisha kazini unahitaji mipango.

Basi hii ni sawa kabisa na shule zinapofunguliwa na wanafunzi wanapaswa kurudi masomoni, lakini hapa ni jukumu la mzazi kuhakikisha anamuandaa vizuri mtoto ili arudi katika hali ya kawaida.

Hili ni muhimu kwa sababu mzazi amebeba jukumu kubwa la kumlea, kumtunza na kumuandalia mtoto wake mazingira mazuri ya kupata elimu itakayomkomboa kifikra na kumsaidia kumudu mazingira yanayomzunguka. Ili kumuandaa vema mtoto wako, fanya mambo haya: 


Mjengee mazingira ya kuamka mapema

Kwa nini ufanye hivyo? Mzazi unapaswa kuhakikisha mtoto anapata muda wa kutosha kupumzisha akili na kuamka mapema kulingana na muda unaotumia siku za kawaida kwenda shuleni. Zoezi hili ni vema lifanyike wiki ya mwisho ya likizo ili hadi siku ya kufungua shule mtoto anakuwa amejiweka sawa kiakili kuanza masomo.

“Mwanangu anaingia darasa la tatu, alikuwa anaingia  darasani mchana kila siku, hivyo nimeshaanza kumzoesha kuamka mapema ili azoee, maana mwaka huu watakuwa wanaingia asubuhi,” anasema Naomi Edward, mkazi wa Mbezi.

Lakini ni vema kumuelewesha mtoto kwanini aamke mapema na katika kipindi hicho anapaswa kupewa kazi za kuandaa kiakili kumudu majukumu yake ya kila siku.

Usingizi wa kutosha kwa mtoto ni muhimu kwa ubongo wa mtoto kukua na kufanya vyema katika masomo darasani. Picha| MommyBrown.com

Fanya manunuzi ya vifaa vya shule na mtoto wako

Mzazi  unatakiwa  kupanga siku ambayo mtaenda pamoja na mtoto wako kununua vifaa vya shule na mahitaji mengine yanayohitajika kwa ajili ya masomo ya 2019.

Hii inamjengea mtoto hali ya kuwa na hamu ya kwenda shule na hasa akipata vitu ambavyo alikuwa anatamani kuwa navyo. Mfano watoto wengine wanaweza kukwambia mzazi ninunulie chupa cha maji, ukimnunulia anakuwa na shauku zaidi ya kuanza masomo.

“Wafanye watoto wapende kurudi shule, kama kuwanunulia vifaa vipya kama madaftari,” anasema Dk Richard Mbunda, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)


Zinazohusiana: 


 

Mpe mazoezi machache ya kumchangamsha akili

Baadhi ya wanafunzi wakati wa likizo wanapelekwa kusoma masomo ya ziada (tution) lakini kuna wale ambao likizo ni muda wa kukaa nyumbani na kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.

Wataalam wa masula ya elimu kutoka idara Elimu ya nchini Marekani wanashauri kuwa wakati wa likizo, wazazi wawandae wanafunzi kwa kuwapa mazoezi ya kusoma au kuandika ili wasisahau kabisa kuhusu shule. Hii itamsaidia mwanafunzi kuchangamka kiakili na kupata muunganiko wa masomo anaporudi shuleni.

Wakati huu, ni muhimu kumpunguzia muda wa kuangalia televisheni na michezo ya video ‘Video games’ ili kuijenga akili yake kufakiwa kimasomo.

Mazoezi yanahusiana na masomo humjenga mtoto kupenda shule na kutojisahau kutimiza majukumu yake. Picha| awriterfirst.wordpress.com

Chunguza Afya ya Mtoto wako

Hakikisha unachunguza afya ya mtoto kabla hajaanza shule ili kipindi akiwa shuleni aweze kukomaa na masomo vizuri. Kama uchumi uko vizuri nenda hospitali kamfanyie mtoto vipimo “Body checkup” hasa kwa wanafunzi ambao wanaosoma shule za bweni. Hii itamuhakikishia afya ya akili na mwili na kumuwezesha kumudu masomo kipindi chote anapokuwa shuleni. 

Pia hakikisha unampa na dawa ya minyoo ambayo wazazi wengi huwa wanajisahau, ili kumuepusha na vimelea vya magonjwa. Muhimu ni kumpatia chakula bora zenye virutubisho muhimu kuichangamsha akili. 


Jipe muda wa kupata taarifa za shule anayoenda mwanao 

Kwa kuwa ni mwaka mpya mzazi una jukumu la kutathmini shule anayoenda mtoto hasa kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza ili kubaini kama mazingira ni mazuri kufanikisha ndoto zake za kusoma. Kama shule haina vifaa fulani vya kujifunzia mnunulie mwanao.

Kwa wanaoendelea na masomo, ni vema kujiridhisha na ratiba ya darasa jipya analoingia kama atahitaji kuwepo shule muda tofauti na darasa la mwaka 2018. Lakini inatakiwa kufahamu ni michango au mahitaji gani mengine yanahitajika shuleni. 

Mafanikio ya elimu ya mtoto wako ni jukumu lako mzazi. Elimu ndiyo urithi pekee unaoweza kudumu lakini maandalizi ya masomo ni muhimu zaidi kukamilisha ndoto zake.