November 24, 2024

Simulizi ya wavuvi haramu walionusa kifo zaidi ya mara tatu baharini

Ni miongoni mwa wavuvi waliokuwa wanavua samaki kwa kutumia dhana haramu ambapo mmoja alikatika kidole na kushudia wengine wakifariki kwa kulipukiwa na mabomu.

  • Ni miongoni mwa wavuvi waliokuwa wanavua samaki kwa kutumia dhana haramu yakiwemo mabomu. 
  • Mmoja alikatika kidole na kushudia wengine wakifariki kwa kulipukiwa na mabomu.
  • Sasa wameageukia uvuvi halali na kuwa mabalozi wa kuelimisha wenzao madhara ya uvuvi wa mabomu.

Dar es Salaam. Ni majira ya saa nne asubuhi, katika kijiji cha Kizito Huonjwa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni, wavuvi watatu wameketi katika kijiwe kidogo kilichopo kijijini hapo wakipiga soga.

Kati ya wavuvi hawa watatu, waliokuwepo katika eneo hili lililowahi kuwa soko lisilo rasmi la samaki,  wawili walishawahi kufanya uvuvi haramu kiasi cha kuhatarisha maisha yao mara kadhaa na kusababisha vilema vya kudumu

Kwa mgeni ni vigumu kubaini kwa haraka historia na machungu waliyopitia wavuvi hawa ambao kwa sasa wamekuwa ni moja wa mabalozi wa kupambana na uvuvi haramu katika ukanda wa pwani wa Kigamboni.

Seleman Kondo, ambaye ni miongoni mwa vijana wa kijiji hicho waliokuwa wakijishughulisha na uvuvi wa mabomu kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita, anajuta kwa nini alijiingiza katika shughuli hizo kabla ya kuacha kwa hiari mwaka huu akihofia kukamatwa na vyombo vya dola.

Licha ya kwamba kujisalimisha kwake katika Serikali ya mtaa kumempa uhuru na fursa ya kufanya uvuvi wa njia halali, pia umesaidia kumuacha akiwa hai kwa kuwa huenda angefariki iwapo angeendelea na uvuvi haramu kutokana na madhara makubwa ya mabomu waliyokuwa wanatumia kuvua.


Zinazohusiana:


“Uvuvi wa gharama”

Kondo, mwenye mke na familia ya watoto watatu, anasema uvuvi wa mabomu ulikuwa unawawezesha kupata samaki wengi kwa haraka lakini gharama zake ni kubwa kuliko uvuvi wa kawaida. 

“Awali tulikuwa tunafikiri kuwa uvuvi wa mabomu una manufaa…kwa kuwa tulikuwa tunalipua samaki wengi na tukishapata tulikuwa hatuhangaiki wala kufikiri kuwa kuna athari zozote…tukirudi baharini wateja wanakuja wenyewe,” anasema Kondo akionyesha fikra hasi walizokuwa nazo awali kuhusu uvuvi huo wa kutumia mabomu. 

Bila kujua walichokuwa wakifanya, Kondo na wenzie walikuwa wanaziweka afya zao rehani na wakati mwingine mauti ilikuwa karibu nao kutokana na vifaa walivyokuwa wakitumia hasa mabomu yaliyotengenezwa kwa njia za kienyeji. 

Shauku ya kupata samaki wengi kwa wakati mmoja iliondoa hofu ya kuchukua tahadhari ya kujikinga wakati wakilipua matumbawe (mazalia ya samaki) haikuwepo kutokana na kukosa elimu ya vilipuzi.  

Omary Mussa Omary amepata kilema cha mkono baada ya kukatika kidole kimoja wakati akirusha bomu baharini. Picha|Daniel Samson.

Mabomu yawanusisha kifo

Kondo anasema wakati bomu likilipuliwa hutoa sauti kubwa na kisha hufuata mtikisiko unaotokea kwenye miamba ya baharini. 

Kama mvuvi ameingia kwenye maji na kulipua bomu anaweza kupata mshtuko kwenye mifupa, kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu kwa dakika kadhaa. 

“Maana lile bomu lina asili ya umeme, unaanza kulia umeme halafu unafuata mlio, kwa hiyo ule umeme unapoanza kulia lazima uusikie unakuja kwenye kiuno. 

“Unaweza ukasikia kama mifupa imevunjika kwa muda kama wa sekunde tatu au sita halafu hali ikajirudia tena vizuri ukaendelea kufanya shughuli zako,” anasema Kondo huku akitikisa kichwa chake kuonyesha masikitiko baada ya kunusurika kifo kutokana na vitendo hivyo.

Kutokana na milipuko ya mara kwa mara, wavuvi wengi wameathirika kisaikolojia ikiwemo kupata matatizo ya akili, kupungua kwa usikivu na afya ya miili yao kudhoofika kwa sababu ya kutumia muda mwingi majini bila kupata chakula kwa wakati.

“Unaporudi ule muda wa mapumziko umehangaika kwa maana hata muda wa kula hupati, nilichokigundua unakuwa tight (unabanwa) na kazi hata muda kula hakuna… unaweza ukala chakula tonge tatu, nne umeshiba. 

“Hali hiyo inakuwa hivyo usiku na mchana,” anasema Kondo ambaye anaonekana kudhoofika huku uso wake ukiwa umekunjamana kutokana kuchoshwa na matumizi ya mabomu hayo katika uvuvi.

Kabla ya kuachana na uvuvi huo haramu, Kondo ameshuhudia matukio mengi ya hatari akiwa na wenzake baharini ikiwemo yeye mwenyewe kunusurika kufa zaidi ya mara tatu kwa sababu kulipua vibaya mabomu. 

Wakati Kondo akinusurika kufa na kubaki na madhara ya kisaikolojia na udhoofu wa mwili, mwenzake Omary Mussa Omary amepata kilema cha mkono baada ya kukatika kidole kimoja wakati akirusha bomu baharini. 

Omary ambaye naye ni mvuvi katika kijiji hicho anasema hataisahau siku ambayo alinusurika kupoteza maisha kutokana na maumivu aliyoyapata na kuvuja damu nyingi baada ya kidole chake kukatika wakati akifungua kilipuzi cha bomu.

“Kidole hiki unachokiona hakikutika kwa mapanga. Hii ilitokana na suala la kurusha mabomu baharini wakati huo tunatumia njia za uvuvi haramu…kwa bahati mbaya sikuona kama bomu limewaka, sasa katika kujitetea likanikata kidole,” anasema Omary na kuongeza kuwa;

“Nilisikia uchungu sana yaani nilijisikia vibaya baadhi ya wavuvi wenzangu walinikimbia wengine majasiri walibaki kwa sababu ni kiongozi wao wakanichukua wakanipeleka hospitali.” 

Licha ya kueleza kuwa matatizo katika kazi yeyote hayakosekani, lakini anasema shughuli haramu waliyokuwa wanaifanya imegharimu maisha ya wenzake wengi ambao baadhi ya walionusurika wamebaki na vilema mwilini kama yeye.

Meli iliyotumika katika operesheni iliyoratibiwa na MATT na Shirika la Sea Shephard ya kusambaratisha mtandao wa wavuvi haramu mapema mwaka huu katika ukanda wa bahari ya Hindi. Picha| Sea Shephard.

Doria za vyombo vya dola “hazikuwaacha salama”

Wakati wakiendelea na uvuvi wa mabomu usiokubalika kisheria iliwalazimu pia kubuni njia za kukabiliana na doria za vyombo vya dola ili waendelea kuvua kwa njia haramu.

Kondo na wenzake waliunda mtandao wa wavuvi ambao ulihusisha baadhi ya wafanyakazi wanaoendesha doria ili kupata taarifa wakati vikosi vikiingia baharini kuangalia usalama lakini hawakufua dafu baadaye.

 “Tulikuwa tunafunga simu kwenye kofia tunakwenda nazo baharini. Tunafanya shughuli zetu askari wa doria wakitoka ghafla tunapigiwa simu kwamba wametoka kwa hiyo sisi tunarudi haraka nchi kavu…kwa hiyo doria inapoondoka sisi kazi tunakuwa tushafunga tunasubiria mpaka kesho tena,” anasema Kondo.

Lakini wakati mwingine mawasiliano yalikuwa yanasumbua na wanajikuta katikati ya askari wa doria, kinachofuata ni kuvitosa vifaa vyote visivyoruhusiwa kwenye maji ili kupoteza ushahidi. 

Mapambano yalivyokuwa

Ilikuwa ni mapambano kati yao na dola kila mmoja akitaka kumshinda mwenzake.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa wao kuendelea na uvuvi huo baada ya kudhibitiwa na 

operesheni kali ya baharini na nchi kavu zilizoendeshwa na Kikosi kazi cha kitaifa (Mult Agency Task Team – MATT) iliyojumuisha msako wa baharini na nyumba kwa nyumba katika maeneo yaliyokuwa vituo vikuu vya uvuvi huo haramu kanda ya pwani.

“Tukarudi katika uvuvi wa mishipi na kadiri muda alivyokuwa unaenda tukajiongeza katika kazi zingine binafsi kwa hiyo tunaishi na watoto mpaka leo,” anasema Omary ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chombo cha usimamizi wa rasilimali za bahari (BMU) katika kijiji hicho. 

Wadau wa masuala ya uvuvi na utunzaji rasilimali bahari wanaeleza kuwa mbinu haramu zinaweza kuzuiwa iwapo wavuvi watapatiwa elimu juu ya athari za uvuvi kwa afya zao, viumbe bahari na katika uchumi wa Taifa. 

Afisa ufuatiliaji na tathmini miradi ya rasilimali za uvuvi na bahari wa Mfuko wa Wanyamapori Duniani (WWF), Elia Sabula ameiambia Nukta kuwa wamekuwa wakishirikiana na wadau wengine vikiwemo vyombo vya dola na wavuvi katika utoaji wa elimu juu ya athari za matumizi ya milipuko katika uvuvi.

“Lakini pia huwa tunawaelimisha wavuvi hao kuhusu sheria na hatua ambazo Serikali inaweza ikazichukua iwapo utakutwa unatumia uvuvi wa mabomu,” amesema.

Wavuvi wakielemishwa matumizi sahihi ya dhana za uvuvi wanaweza kuwa sehemu ya kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za bahari. Picha| Tanga kumekucha

Hata hivyo, elimu pekee kwa wavuvi waliokuwa wamezoea kupata kipato kupitia njia haramu haitoshi kuwarudisha katika hali ya kawaida ya kiuchumi.

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwasaidia kuweza kurudi katika maisha yao ya kawaida ili wasitamani kurudia uvuvi haramu kutokana na kukosa kipato?

Mkurugenzi wa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi anasema wana mipango ya kuwaendeleza wavuvi  kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na wizara ambapo wavuvi kupitia BMU hujengewa uwezo wa usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

“Tuna mpango kwa wavuvi ambapo wizara hutoa ruzuku kwa ununuzi wa  injini za kupachika kwa kugharamia asilimia 40 na wavuvi kuchangia asilimia 60,” amesema.

Hata hivyo, kwa sasa sehemu kubwa ya uvuvi huo wa mabomu umepungua baada ya operesheni ya kikosi cha MATT kilichoundwa kuzuia uhalifu wa kimazingira na kusimamia uvuvi wa bahari kuu.

Kikosi hicho kazi kinajumuisha wataalam kutoka Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), jeshi la polisi, Usalama wa Taifa (TISS), maafisa uvuvi, mazingira na mashirika yasiyo ya kiserikali na wavuvi wa maeneo husika.

Serikali inasema kuwa hadi sasa uvuvi wa mabomu umepungua kwa zaidi ya asilimia 85 na inaendelea kushirikiana na wadau kuutokomeza.