Mastaa walivyoitangaza Tanzania kimataifa 2018
Mastaa hao ni pamoja na Jodi Sta Maria (Maya), Juhi Chawla, Barack Obama huku Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiongoza kutembelewa.
- Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti zaongoza kwa kutembelewa na mastaa hao.
- Serikali inazidi kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya kuvutia watalii wengi zaidi kuja Tanzania.
- Mastaa hao ni pamoja na Jodi Sta Maria (Maya), Juhi Chawla, Barack Obama na wengineo.
Dar es Salaam. Katika kuelekea kufunga mwaka 2018, sekta ya utalii Tanzania haikubaki nyuma katika anga za kimataifa imeweza kuvutia watalii kuja kutembelea vivutio vinavyopatikana maeneo mbalimbali nchini.
Nukta tunakuletea baadhi ya mastaa na watu maarufu duniani waliotembelea Tanzania mwaka huu ambao wamechangia kutangaza vivutio vya utalii kimataifa katika mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram.
Juhi Chawla
Ni Muigizaji wa muda mrefu kutoka nchini India ambaye ameanza kuigiza tangu mwaka 1984. Chawla ameigiza filamu nyingi na mastaa wengine wa Bollywood kama Shah Rhuk Khan, Aamir Khan na wengine wengi.
Kama ni mpenzi wa sinema za kihindi basi utakuwa unaikumbuka filamu ya ‘Ram Jaane’ ambayo ilimpa umaarufu zaidi miaka ya 1990.
Januari mwaka huu akiwa na familia yake walitembelea Tanzania lakini walichagua kupanda Mlima Kilimanjaro ambao ndiyo wenye kilele kirefu zaidi barani Afrika, na kutembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Jodi Sta.Maria
Ni staa mwingine kutoka Ufilipino aliyetembelea Tanzania katika eneo la utalii, najua wengi wanamjua kwa jina la Maya kutokana na tamthilia maarufuya ‘Be Careful with My Heart’ aliyoigiza kama msichana wa kazi na kumpa umaarufu duniani.
Sta.Maria aliingia Tanzania mapema Februari mwaka huu na kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa anaongeza orodha ya mastaa filamu duniani waliotembelea nchini. Siku chache aliweka picha katika ukurasa wake instagram akionyesha yuko juu ya mlima ambapo mashabiki wake walionyeshwa kufurahishwa na jambo hilo.
Barrack Obama na famiia yake
Rais huyo mstaafu wa Marekani alikuja nchini Julai kwa ajili ya mapumziko ya siku nane akiambatana na mkewe, Michelle Obama pamoja na watoto wake Malia na Sasha. Habari zake hazikupata muitikio mkubwa wa vyombo vya habari kwasababu ilikuwa safari ya binafsi.
Obama alifikia katika hoteli ya Singita Grumeti iliyopo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ni moja ya hoteli zenye hadhi ya kimataifa ambayo imekuwa ikipokea ugeni wa watu mashahuri duniani.
Kabla ya ujio wa Obama na familia yake, Marais wengine wastaafu wa Marekani Bill Clinton aliyewahi kuwa Rais wa 42 wa Marekani na George W Bush nao waliwahi kufikia katika hoteli hiyo. Pia inaelezwa kuwa mmiliki wa kampuni za Microsoft duniani bilionea Bill Gates naye ni miongoni mwa watu waliowahi kufikia katika hoteli hiyo.
Zinazohusiana:
- Prince William atua Tanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wanyamapori
- Tamasha la ‘Urithi Festival’ kufanyika mikoani kila mwaka
Prince William
Ni mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, na yeye alifika Tanzania Septemba katika ziara yake ambayo lengo lilikuwa kuhakikisha Tanzania inashirikiana na Uingereza katika kuimarisha na kuendeleza ushirikiano katika uhifadhi wa wanyamapori na kukabiliana na vitendo vya ujangili dhidi ya tembo ambao wako hatarini kutoweka.
Vilevile baada ya mazungumzo na Rais John Magufuli alibahatika kwenda katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Tanga na kuangalia jinsi faru weusi wanavyotunzwa na kulindwa dhidi ya vitendo vya ujangili kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Prince William, ni mjukuu wa Queen Elizabeth II wa Uingereza naye alikuwa mmoja wa watu mashuhuri waliotembelea Tanzania mwaka huu. Picha|Michuzi.
Anne Curtis Smith
Jodi siyo muigizaji pekee kutoka Ufilipino aliyepata nafasi ya kutembelea Tanzania, bali muigizaji mwingine maarufu wa aliyetamba na tamthilia ya “More Than Love” kati ya mwaka 2006 hadi 2007, na kujipatia umaarufu sehemu mbalimbali duniani, anaingia katika orodha ya watu waliotembelea Tanzania mwaka 2018.
Anne ametembelea hifadhi ya Taifa ya Mahale kwa siku tatu ikitimiza ndoto yake ya kufanya utalii katika nchi za Afrika. Mahale iko magharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika linalozungukwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,613.
Kama ilivyo hifadhi jirani ya Gombe, hifadhi ya milima ya Mahale ni makazi ya jamii adimu za Sokwe zilizobakia barani Afrika. Katika hifadhi hii yenye misitu minene inayovuta mvua kwa wingi, kundi kubwa la Sokwe huonekana katika vilima na mabonde.
Serikali yajipanga kuvutia wawekezaji wengi
Ujio wa watu maarufu nchini ni ishara kuwa juhudi za kutangaza utalii zikiimarishwa, Tanzania itaongeza mapato yatokanayo na sekta hiyo na kuchangia katika uboreshaji wa huduma za kijamii.
Takwimu za wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha kuwa mwaka 2017 idadi ya watali walioingia nchini ilifika milioni 1.3 huku wengi wakitokea Marekani.
Tanzania imekuwa ikitumia kampeni mbalimbali za kukuza utalii ikiwemo kutumia kauli mbiu ya #UnforgettableTanzania katika mitandao ya kijamii. Pia hivi karibuni imezindua chaneli mpya ya Safari inayoangazia kutangaza vivutio vilivyopo nchini kimataifa.
Pamoja na hayo, imezidi kujiimarisha kwa kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kununuliwa kwa ndege 5 kubwa za kisasa ikiwemo Bombardier Q400, Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262.
Kuanzia Februari 2019, Air Tanzania itaanza safari zake moja kwa moja hadi Jiji la Guangzhou, China na ndege nyingine inatarajiwa kusafiri hadi Mumbai, India hivyo tutegemee watalii wengi kama Juhi kuja nchini kutokana na kuimarishwa kwa sekta ya usafiri wa anga.