October 6, 2024

Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar

Mbinu hizo ni pamoja na msako wa baharini na wa nyumba kwa nyumba katika maeneo yaliyokuwa vituo vikuu vya uvuvi huo haramu jijini hapa.

  • Mbinu hizo zinajumuisha msako wa baharini na wa nyumba kwa nyumba katika maeneo yaliyokuwa vituo vikuu vya uvuvi huo haramu jijini hapa.
  • Baadhi ya wavuvi haramu walijisalimisha wenyewe kutokana na taharuki.
  • Mbinu mpya za uvuvi haramu zabuniwa yakiwemo mabomu ya ‘kimyakimya’ ikiwemo matumizi ya kemikali ya Chroline. 
  • Serikali yasema hakuna atayesalimika. 

Dar es Salaam. Pembezoni mwa kijiji cha uvuvi cha Kizito Huonjwa katika mji mdogo wa Kimbiji uliopo takriban kilomita 40 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, pilikapilika za wavuvi na wafanyabiashara wa samaki zimetoweka.

Kwa mtu anayefika mara ya kwanza katika eneo hilo la wilaya ya Kigamboni hawezi kugundua haraka kuwa liliwahi kuwa soko kubwa la biashara ya samaki kutokana na ukimya. Baadhi ya makazi ya familia za wavuvi yametelekezwa baada ya msako mkali uliofanywa na vyombo vya dola.

Ukimya umetokana na usitishwaji wa soko hilo la samaki baada ya Serikali kubaini kuwa lilikuwa ni moja ya vituo vikuu vya uvuvi haramu wa kutumia mabomu jijini hapa.

Maeneo mengine ambayo yaliyokuwa  yakitumika kwa uvuvi huo haramu, kwa mujibu wa uchunguzi wetu, ni Kunduchi, Kawe na Ununio katika Halmashauri ya Wilaya Kinondoni; Buyuni na Minazi Mikinda (Kigamboni) na sehemu za mbali kidogo ya Bahari ya Hindi.

Hata hivyo, kwa sasa sehemu kubwa ya uvuvi huo wa mabomu umepungua baada ya operesheni kali ya baharini na nchi kavu zilizoendeshwa na Kikosi kazi cha kitaifa (Mult Agency Task Team – MATT).

Kikosi hicho kilichoundwa kuzuia uhalifu wa kimazingira na kusimamia uvuvi wa bahari kuu kinajumuisha wataalam kutoka Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), jeshi la polisi, Usalama wa Taifa (TISS), maafisa uvuvi, mazingira na mashirika yasiyo ya kiserikali na wavuvi wa maeneo husika.

Nyavu za ringi (Ringnet) ndiyo zinazotumika kwa wavuvi wa eneo la Minazi Mikinda Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha uvuvi endelevu wenye manufaa kwao na rasilimali zingine za bahari. Awali baadhi ya wavuvi walikuwa wakitumia uvuvi haramu wa mabomu. Picha| K15.

Operesheni ya “machozi na damu”

Operesheni kubwa, iliyowatowesha wavuvi wengi haramu jijini hapa, ilianza Januari mwaka huu baada ya MATT kujumuisha mbinu mpya za msako wa baharini na wa nyumba kwa nyumba katika maeneo yaliyokuwa na wavuvi hao ikiwemo Kizito Huonjwa.

Mmoja ya wavuvi waliokuwa wakijihusisha na uvuvi wa mabomu kabla ya kuachana nao hivi karibuni Omary Mussa Omary anasema hajawahi kuona operesheni kali kama hiyo kwa kuwa ilizua taharuki kwa wavuvi na wakazi.

 “Kwanza walikuja kisirisiri wakataka kujua wakina nani wanajihusisha na uvuvi huo na wanawapataje,” anasema Omary aliyepoteza kidole baada ya kulipukiwa na bomu wakati akivua samaki.

“Kwa sababu ya ile nguvu iliyotumika kuwakamata watuhumiwa…hadi wanawake nyumbani walikuwa wakiwaambia wanaume zao ‘kama unafanya uvuvi wa bomu mimi sikutaki’,” anasema Omary na kueleza operesheni hiyo ilileta taharuki miongoni mwa wavuvi haramu.

Baadhi kama Selemani Kondo, mvuvi anayekaa Kizito Huonjwa, ilimbidi aitekeleze familia yake kwa zaidi ya wiki tatu akihofia kukamatwa kabla kutakiwa kujisalimisha Serikali za mitaa kwa masharti ya kukubali kuachana na uvuvi wa mabomu.


Zinazohusiana: 


Mtafiti wa masuala ya bahari, Gill Braulik kutoka kampuni ya utafiti na uhifadhi ya Downstream (Downstream Research & Conservation) anasema kuwa mtandao wao wa ving’amuzi vya kurekodi sauti za mabomu katika ukanda wa pwani nchini umeripoti millipuko kwa kiasi kidogo sana jambo linalosadifu kauli za jamii ya wavuvi kuwa uvuvi wa aina hiyo umepungua kwa kiwango kikubwa.

 “MATT walitusaidia sana katika maeneo ambayo sisi hatukuweza kufika awali,” anasema Emmanuel Bulayi, Mkurugenzi wa uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Doria hizo zilihusisha kuharibu na kuteketeteza mitumbwi na malighafi zote za kutengenezea mabomu ili kuhakikisha wahusika hawaendelei na shughuli za kuvua kwa njia zisizokubalika kisheria.

Baada ya operesheni hiyo, Bulayi anasema kuwa tathmini ya awali inaonyesha kuwa kwa sasa uvuvi wa kutumia mabomu katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi umekomeshwa kwa asilimia 85.

Wakati Mkurugenzi huyo akieleza mafanikio hayo, vyanzo vyetu vimeeleza kuwa baadhi ya wavuvi wameanza kutumia mbinu mpya za uvuvi haramu ikiwemo milipuko isiyotoa sauti “silent bombs” (mabomu ya kimyakimya) ili kukwepa mamlaka.

Mbinu hiyo inahofiwa na wataalam wa viumbe vya bahari kuwa huenda inahusisha matumizi ya kemikali kama ‘Chroline’ ambayo ni hatari kwa afya za binadamu na viumbe wengine wa majini.

“Pamoja na uvuvi wa mabomu kupungua, ving’amuzi vyetu vilivyopo baharini vimerekodi sauti mbalimbali katika ukanda wa pwani wa Tanzania. Japo utafiti unaendelea kuhusu jambo hilo lakini milipuko hiyo ya Chroline inajulikana kama “mabomu ya kimyakimya” kwa sababu haitoi sauti juu ya usawa wa maji,” amesema Braulik 

Lydia Mwakanema, Afisa miradi wa usimamizi wa rasilimali za uvuvi na bahari wa Mfuko wa Wanyama Pori (WWF) anasema matumizi ya mabomu yasiyotoa sauti yanafanya iwe vigumu kwa vyombo vya dola na wale wanaosimamia sheria kwenda kufuatilia na kujua mahali mlipuko ulipotokea.

Licha ya kuwa wanafuatilia suala hilo la milipuko ya kimyakimya kupitia utafiti wa kina, Mwakanema anasema taarifa za awali zinaonyesha kuwa “wavuvi wanatengeneza milipuko mikubwa ya aina hiyo kama ndoo ya lita 20 ambayo ikilipuka inaharibu mahali pakubwa”.

Mbinu nyingine iliyozuka baada ya uvuvi wa mabomu ni matumizi ya tochi zenye mwanga mkali ambazo wavuvi huzama nazo baharini ili kuwalevya samaki na kuwakamata kirahisi.

“Zile tochi sijui zina madini gani, samaki wakimulikwa wanalala kabisa, sasa mvuvi anapata nafasi nyepesi ya kuwachoma samaki kirahisi,” anasema Omary.

 Polisi wanaeleza kuwa hadi sasa wahajabaini aina hiyo mpya ya uvuvi haramu.

“Kama kuna uvuvi wa ‘design’ (mbinu) hiyo watu watoe taarifa mapema ili michakato ifanyike na kuwakamata,” anasema Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

 

Uvuvi wa mabomu unagharimu walipakodi

Vita dhidi ya uvuvi haramu, ambayo haikutakiwa kuwepo iwapo wavuvi wangezingatia mbinu rafiki, huitaji rasilimali lukuki kama watu na fedha za umma ambazo zilipaswa kugharamia miradi mingine ya maendeleo kama elimu, afya na maji.

“Gharama zilizotumika kwa ujumla wa zoezi zima bajeti yetu ilikuwa milioni 89 kwa mwaka na tunaendelea vizuri,” anasema Bulayi.

Hata hivyo, Bulayi katika mahojiano zaidi aliyeeleza kuwa kiasi cha fedha za doria hutegemeana na kiwango cha uvuvi haramu.

Wavuvi wanaovua samaki kwa njia halali waliokuwa ni miongoni mwa wadau walioungana na mamlaka kukabiliana na wale wanotumia dhana haramu yakiwemo mabomu ili kuwahakikishia upatikanaji wa samaki. Picha| K15.

Uvuvi wa mabomu ulivyokuwa ukifanyika

Kabla ya operesheni ya hivi karibuni, katika baadhi ya maeneo ambayo Nukta ilifanya uchunguzi imebainika kuwa wavuvi haramu walikuwa wakivua kwa mabomu mchana bila kuhofia kukamatwa wakitumia vilipuzi vya kisasa na kienyeji.

Kwa kuwa walikuwa wakipata kipato cha haraka bila kujali athari za kiafya kwa binadamu na mazingira, mvuvi ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema baadhi ya wamiliki wa boti walikuwa wakiwashiwi kutumia vyombo vyao kufanya uvuvi wa mabomu ili kupata samaki wengi kwa muda mfupi.

Hali hiyo ilifanya wavuvi haramu, ambao ni wenyeji wa Dar es Salaam na baadhi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, kuendelea kufanya vitendo hivyo na sehemu kubwa ya samaki walikuwa wakiwauza maeneo ambayo hakuna maofisa wa uvuvi wa kukagua bidhaa hizo.

Ili kukwepa mamlaka, wavuvi hao walikuwa wanasafirisha boti zenye vilipuzi hadi umbali kidogo wa bahari na kuzizamisha ndani ya maji huku wakizifunga na maboya madogo nje ili zisizame.

“Ilikuwa ngumu kujua kama kuna boti eneo hilo, wakienda kuvua samaki na milipuko wanaibua wakirudi wanazamisha, hivyo tulikuwa hatuwezi kuwapata kirahisi.

“Kupitia vikundi vya usimamizi wa fukwe  boti tuliweza kukamata boti zaidi ya 60 au 70,” anasema Ernest Kamata,  Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kigamboni na kuongeza kuwa sehemu kubwa ya boti hizo wamiliki wake wahakubainika kwa haraka kwa kuwa hazikusajiliwa.

Serikali inasema kuwa katika operesheni hiyo ya MATT kwa kushirikiana na shirika la Sea Sense iliyofanywa kati ya Januari na Juni mwaka huu watuhumiwa 32 walikamatwa na kesi 13 zilifunguliwa mahakamani. Mbali na kesi, wizara inasema faini ya Sh15.45 milioni zilikusanywa kutoka kwa waliotiwa hatiani.

Wadau wa uvuvi wanasema utashi wa kisiasa wa viongozi wa Serikali umesaidia operesheni ya kutokomeza uvuvi wa mabomu hasa baada ya Rais John Magufuli  kuingia madarakani mwaka 2015 kutaka shughuli zote za uvuvi haramu zitokomezwe ili wananchi wafaidike na rasilimali za bahari na maziwa.

Baadhi ya wavuvi waliokamatwa wakiwa na vifaa vinavyotumika kuvua samaki kwa kutumia mabomu. Picha| SmartFish.

“Rais mwenyewe Julai 2016 alitoa hotuba kuonyesha kutokuwepo uvumilivu katika masuala ya uvuvi haramu (zero telerance) hivyo ni bora wadau wote tushirikiane kutokomeza uvuvi huo,” anasema Mkurugenzi wa Shirika la uhifadhi wa viumbe wa baharini la Sea Sense Tanzania.

Tofauti na awali, kwa sasa mvuvi haingii kirahisi baharini kama hana leseni ambazo zinatolewa kwa wavuvi wenye historia nzuri na wanaotumia njia endelevu za uvuvi.  

Baadhi ya wavuvi wa Kunduchi na Ununio wameiambia Nukta kuwa leseni na doria zimefanya wavuvi wengi kuachana na uvuvi haramu na kujifunza mbinu halali.

Kama ilivyo kwa Kimbiji, wavuvi wa maeneo mengine wameunda vikundi vya uvuvi ambavyo huwasaidia kulinda maeneo yao yasivamiwe na wavuvi wanaotumia vilipuzi.

“Sisi hapa tunatambuana, wapo wavuvi ambao kazi yao ni kushika doria baharini ni vigumu kuvua kwa mabomu ukikamatwa unafukuzwa,” anasema Hafidhi Amani, mvuvi wa Kizito Huonjwa.

Ongezeko la wavuvi baharini pia limepunguza eneo la uvuvi, jambo linalosababisha wanaotumia vilipuzi kukosa uhuru na eneo kubwa la kutekeleza vitendo hivyo haramu.

Bulayi anasema kwa sasa “wanaanza kuona samaki wakipatikana tena kwa viwango vizuri bei nzuri na tunategemea sekta itakuwa zaidi ya asilimia nne kwa kuwa mwanzo ilikuwa kati ya asilimia mbili hadi 2.5.”

“Nawashauri wananchi wafuate sheria na waache uvuvi haramu, hakuna atakayebakia. Mwananchi yoyote atakayefuata uvuvi haramu awe nyumbani kwake au baharini tutamfikia,” anasema huku akieleza kuwa kwa sasa wamejikita zaidi kutoa elimu juu ya athari za uvuvi haramu nchini.

Ripoti hii maalum imeandaliwa na Nuzulack Dausen, Daniel Mwingira, Rodgers George, Daniel Samson, Tulinagwe Malope na Zahara Tunda. Awali ilichapishwa katika gazeti la Mwananchi Desemba 6, 2018.