October 6, 2024

Majaliwa aanika faida za chaneli mpya ya utalii Tanzania

Itatoa fursa kwa wadau kutangaza utalii ndani na nje ya Tanzania ili kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo watakaochangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

  • Itatoa fursa kwa wadau kutangaza utalii ndani na nje ya Tanzania ili kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo watakaochangia katika ukuaji wa pato la Taifa.   
  • Watangazaji na wafanyakazi wa chaneli hiyo washauriwa kutafutiwa fursa za masomo nje ya nchi ili kupata ujuzi zaidi.
  • Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema kuna haja Serikali kukaa chini na wadau kuangalia namna ya kurekebisha sheria ili kuruhusu chaneli hiyo ionyeshwe bure. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa amezindua rasmi chaneli ya utalii itakayotoa fursa kwa wadau kutangaza utalii ndani na nje ya Tanzania ili kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo watakaochangia katika ukuaji wa pato la Taifa.   

Chaneli hiyo imepewa jina la “Tanzania Safari Channel” ambayo inasimamiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kupatikana katika ving’amuzi mbalimbali kikiwemo cha Startimes.

Huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa alipozuru makao makuu ya shirika hilo Mei 16 na kuelekeza uongozi wa TBC uangalie uwezekano wa kuanzisha chaneli ya utalii kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) 

Katika uzinduzi huo uliofanyika leo (15 Disemba 2018) Jijini Dar es Salaam, Majaliwa ameweka wazi kuwa ufunguzi wa chaneli hiyo ni moja ya fursa ya kutangaza utalii ndani na nje ya Tanzania ili kuweza kuleta watalii wengi zaidi watakaochangia katika ukuaji wa sekta ya utalii nchini.

“Faida zitakazopatikana kwa chaneli hii ya utalii tutanufaika kupata idadi kubwa ya watalii na tutapata fedha za kigeni, tukipata idadi kubwa ya watalii pato litaongezeka,” amesema Majaliwa.

Amesema channeli hiyo ambayo anatamani iwe huru na kupewa jina la TBC3, itafungua milango ya ajira kwa watu mbalimbali wakiwemo wananchi ambao watanufaika na shughuli na biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali yenye vivutio nchini.

Ajira hizo zitajumuisha pia wafanyakazi watakaokuwa wanazalisha maudhui ya vipindi vya chaneli hiyo ambayo inakusudia kurusha matangazo yake kwa saa 24 kwa wiki.


Zinazohusiana: 


Amewapa changamoto TBC kuongeza wafanyakazi ili kila mkoa kuwe na mwakilishi ambaye atarahisisha upatikanaji wa maudhi katika chaneli hiyo na wapewe fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi ili waweze kuzalisha vipindi bora na vyenye kuvutia.

“Tuna mahusiano mazuri na balozi mbalimbali, baadhi ya wafanyakazi wa chaneli hii mpya wapelekwe kwenda kujifunza zaidi kwa wenzetu,” amesema Majaliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Dk Ayoub Rioba amesema kuzinduliwa kwa chaneli hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa wadau wa utalii hasa Tanapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambao wamechangia manunuzi ya mitambo na upatikanaji wa studio mpya.

“Vifaa vya kuanzisha chaneli hii ni gharama tunawashukuru Tanapa na Ngorongoro ambao walitoa kiasi cha zaidi ya milioni 700 ili kufanikisha upatikanaji wa chaneli hii,” amesema Dk Rioba.

Hata hivyo, katika uzinduzi huo suala la kurusha matangazo bila malipo katika ving’amuzi vya ndani limeibuka ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema kuna haja Serikali kukaa chini na wadau kuangalia namna ya kurekebisha sheria ili kuruhusu chaneli hiyo kupata kibali cha kuonyeshwa bure ndani na nje ya nchi.

“Masuala ya ‘free to Air’ (bila malipo) na mengine inapaswa yaangaliwe kisheria ila tunataka zaidi ionekane nje, kipato cha watalii wa ndani ni kidogo sana ukilinganisha na cha nje ya nchi,” amesema Kigwangwalla.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), chaneli zinazoruhusiwa kuonekana bila malipo ni TBC, Star TV, ITV, Channel Ten na EATV pekee ambazo zinapatikana kwenye king’amuzi cha Startimes.

Wadau wengine waliofanikisha uanzishwaji wa Chaneli hiyo mpya ya Utalii ya Tanzania Safari ni Shirika la Utangazaji Tanzania, Wizara ya Maliasili na Utalii, wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ni jambo la kujivunia kuanzishwa kwa chaneli hiyo lakini nguvu zaidi ya mitandao ya kijamii itumike kutangaza vivutio vya utalii na kutumia maeneo ya wazi kuwafikia watu wengi.