November 24, 2024

Rais Magufuli atoa vitambulisho maalum kwa wafanyabiashara wadogo

Vitambulisho hivyo viko 670,000 na kila mkuu wa mkoa amepewa vitambulisho 25, 000 ili wakavigawe kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Sh4 milioni viwasaidie kuzitambulisha biashara zao.

  • Vitambulisho hivyo ni maalumu kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Sh4 milioni ili viwasaidie kuzitambulisha biashara zao.
  • Ameagiza kuwa wafanyabiashara watakaogawiwa vitambulisho hivyo wasisumbuliwe na mtu yeyote wakati wa kufanya shughuli zao.
  • Amefikia hatua ya kutoa vitambulisho hivyo yeye mwenyewe kwa sababu mamlaka husika inachelewesha na wafanyabiashara wadogo wanaendelea kusumbuliwa.
  • Amewataka TRA kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha zaidi watu kulipa kodi.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa vitambulisho maalum 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania kwaajili ya kuwagawia wajasiriamali katika mikoa yao wakiwemo wa machinga vitakavyouzwa kwa Sh20,000 kwa kila kimoja.

Rais Magufuli amegawa vitambulisho hivyo leo (Desemba 10) katika kikao kilichoikutanisha  Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) na viongozoi mbalimbali wa umma nchini na kueleza kuwa vitambulisho hivyo ni maalumu kuwatambulisha wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Sh4 milioni.

Baada ya kugawa vitambulisho hivyo maalumu kwa wakuu wa mikoa, Rais Magufuli ameagiza kuwa wafanyabiashara watakaogawiwa wasisumbuliwe na mtu yeyote  wakati wa kufanya shughuli zao.

“Mfanyabiashara mdogo akivaa kitambulisho hiki asisumbuliwe na mtu yeyote, na niseme kwa dhati ndugu zangu viongozi wa siasa mtu utakayemkuta na kitambulisho hiki na anafanya biashara ya chini ya Milioni 4 usimsumbue,” amesisitiza Rais Magufuli.

Amesema amefikia hatua ya kutoa vitambulisho hivyo yeye mwenyewe kwa sababu mamlaka husika inachelewesha na wafanyabiashara wadogo wanaendelea kusumbuliwa.

Vitambulisho hivyo viko 670,000 na kila mkuu wa mkoa amepewa vitambulisho 25, 000 ili wakavigawe kwa wafanyabiashara wa maeneo yao na fedha watakazopewa wakazilipe TRA.

“Vitambulisho hivi navitoa bure ila wafanyabishara watachangia 20,000 kila mmoja, kama kurudisha gharama ya utengenezaji wake ili fedha hizo zikatumike kutengenezea vitambulisho vingine na kianze kutumika mara tu anapokipata,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara watakaopata vitambulisho hivyo kuvitumia kwa matumizi yao si kuvichukua kisha wakawafanyie biashara kwa wafanyabiashara wakubwa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameitaka TRA kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha zaidi watu kulipa kodi, kushirikiana na vyombo vya dola kubaini na kuwakamata wakwepa kodi wote hususani wanaosafirisha bidhaa mipakani kimagendo na kuacha kuwakatisha tamaa wafanyabiashara kwa kuwafanyia makadirio ya kodi kwa viwango cha juu visicholipika.

“TRA mnakwenda kwa mfanyabiashara mnamkadiria kodi shilingi Bilioni 2, anawaambia nitatoa Bilioni 1 au Milioni 800, mnakataa na mnaamua kumfungia biashara, sasa biashara ikifungwa utakuwa umepata nini? Tunashindwa hata kutumia busara zetu katika ukusanyaji wa kodi,” amesema Rais.

Pia amewaonya baadhi ya viongozi wa siasa ambao wamekuwa wakiwakingia kifua wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na amewaagiza maafisa wa TRA kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria bila kushinikizwa na mtu yeyote.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof Florens Luoga amesema benki hiyo inaendelea kufanya juhudi za kusimamia na kuimarisha sekta ya fedha ambapo ukopeshaji kutoka benki mbalimbali kwa wafanyabiashara umepanda kutoka asilimia 0.8 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 Septemba 2018.

Agosti 23, mwaka huu, BoT ilishusha riba ambayo huitumia kuzikopesha benki za biashara nchini (discount rate) kutoka asilimia tisa iliyokuwepo awali hadi asilimia saba ambapo kwa makadirio yaliyopo inaweza kufika asilimia 3.5.


Zinazohusiana:


Kutokana na ahueni hiyo kwa benki za biashara nchini, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, aliyekuwa anazindua tawi la Benki Azania, Sokoine Jijini Dodoma (Desemba 6, 2018), alizitaka benki hizo kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Albina Chuwa ametoa maelezo ya hali ya takwimu za kiuchumi hapa nchini na kubainisha kuwa takwimu za ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018 zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani wa asilimia saba na mfumuko wa bei umeandika rekodi ya chini zaidi kuwahi kutokea katika miaka 10 ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 3.0 Novemba 2018.