October 6, 2024

Serikali yazitaka benki kushusha riba za mikopo

Lengo ni kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.kuchochea maendeleo.

  • Lengo ni kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.
  • Amesema kuhusu fedha za kigeni, kisheria benki zote za biashara zinatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu kuhusu miamala ya soko la fedha za kigeni kati ya mabenki waliyofanya kwa siku.
  • Benki zashauriwa kutekeleza mikakati ya kutoa mikopo ili kuimarisha sekta ya ujenzi wa viwanda nchini.

Dar es Salaam. Serikali imezitaka benki za biashara nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, aliyekuwa anazindua tawi la Benki Azania, Sokoine Jijini Dodoma (Desemba 6, 2018), amesema benki zina nafasi kubwa kuisaidia Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji na biashara..

Amesema kuwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia 16 hadi asilimia tisa.

Katika hotuba yake hiyo, Dk Kijaji amesema Serikali imepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10 hadi asilimia nane, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17.

“Kama haya yote yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa kisingizio cha kuogopa mikopo chechefu wakati Serikali kupitia Benki Kuu, imeanzisha kanzi data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji (Credit Reference Bureau System),” alihoji Dkt Kijaji katika taarifa iliyotolewa na Idara ya mawasiliano ya wizara hiyo.


nayohusiana: 


Ripoti ya Uchumi ya Oktoba 2018 (Monthly Economic Review) ya BoT inaeleza kuwa kiwango cha riba za mikopo katika benki za biashara nchini zilipungua kidogo kutoka wastani wa asilimia 18.65 Septemba, 2017 hadi asilimia 17.42 Septemba mwaka huu. 

Mbali na kuagiza kushushwa kwa riba, Dk Kijaji amesikitishwa na hatua ya benki ya Azania kuwa miongoni mwa benki tano zilizofungiwa kwa kipindi maalum kushiriki katika kuuza na kununua fedha za kigeni baada ya kukiuka taratibu za biashara hiyo.

“Kisheria, benki zote za biashara zinatakiwa kutoa taarifa benki kuu kuhusu miamala ya soko la fedha za kigeni kati ya mabenki waliyofanya kwa siku lakini benki yako ni miongoni mwa benki zilizovunja utaratibu huu, hii ni aibu!” amesema Dk Kijaji.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine Jijini Dodoma. Picha| Saidina Msangi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe amesema taasisi yake imeendelea kufanya vema katika soko baada ya kupata faida na kueleza kuwa imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.

“Benki yetu mwaka 2017 imetengeneza faida ya Sh1.81 bilioni ikilinganishwa na hasara ya Sh6 bilioni iliyoripotiwa Desemba 2016 na imeongeza rasilimali zake kutoka Sh338 bilioni hadi Sh390 bilioni,” amesema Itembe.

Benki hiyo imeongeza kiasi cha mikopo iliyotoa kutoka Sh129 bilioni mwaka 2016 hadi Sh187.7 bilioni mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 10.23.

Akiba za wateja za benki hiyo, Itembe amesema zimeongezeka kutoka Sh236 bilioni mwaka 2016 hadi Sh 271 bilioni mwaka jana.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Azania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Umma (PSSSF), Eliud Sanga ameitaka benki hiyo kutekeleza mkakati wake wa kuanza kutoa mikopo ili kuimarisha sekta ya ujenzi wa viwanda nchini.