October 6, 2024

Chamwino kujenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi

Kiwanda hicho kinategemewa kujengwa kwa gharama ya Sh500 milioni mpaka kitakapokamilika na kitatoa ajira kwa watanzania 70 ambao watapangiwa majukumu mbalimbali kiwandani hapo.

Bidhaa zinazotokana na ngozi ya wanyama mbalimbali nchini. Picha| Mwananchi.


  • Kiwanda hicho kinategemewa kujengwa kwa gharama ya Sh500 milioni mpaka kitakapokamilika na kitatoa ajira kwa watanzania 70 ambao watapangiwa majukumu mbalimbali kiwandani hapo.
  • Miongoni mwa viwanda vinavyosindika ngozi hapa nchini ni pamoja Lake Trading Co. Ltd Kibaha, Himo Tanner & Planters Ltd Moshi, ACE Leather (T) Ltd Morogoro pamoja na Meru Tanneries Ltd kilichopo mkoani Arusha.

Dar es Salaam. Huenda wafugaji mkoani Dodoma wakaanza kunufaika na biashara ya ngozi hasa ng’ombe baada ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ngozi na kuzalisha bidhaa za ngozi katika kata ya Idifu, wilaya ya Chamwino.

Kiwanda hicho kinategemewa kujengwa kwa gharama ya Sh500 milioni mpaka kitakapokamilika na kitatoa ajira kwa watanzania 70 ambao watapangiwa majukumu mbalimbali kiwandani hapo.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Hozen Mayaya amesema hayo wakati wa sherehe za mahafali ya 32 ya Chuo hicho Kampasi ya Dodoma, ambapo wahitimu 2,596 wametunukiwa vyeti na shahada mbalimbali.

“Kupitia mradi wa Eco Act, unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, Chuo kimetekeleza falsafa ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda hiki ambacho kikikamilika kitakuwa na jumla ya wafanyakazi 70, kati ya hao 50 watakuwa wa kudumu na vibarua 20” amesema Prof. Mayaya.

Miongoni mwa viwanda vinavyosindika ngozi hapa nchini ni pamoja Lake Trading Co. Ltd Kibaha, Himo Tanner & Planters Ltd Moshi, ACE Leather (T) Ltd Morogoro pamoja na Meru Tanneries Ltd kilichopo mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa Chama Cha Kusindika Ngozi Tanzania katika taarifa yake mwaka 2017 kilieleza kuwa kuna ukosefu wa ngozi unaofikia zaidi ya asilimia 80, na ngozi inayopatikana ni chini ya asilimia 20 kutokana viwanda vilivyopo kuwa na uwezo mdogo wa kusindika ngozi.

Aidha, Prof Mayaya ameeleza kuwa Chuo hicho kinatekeleza mradi mwingine wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kuzijengea uwezo halmashauri za wilaya ya  Longido, Ngorongoro na Monduli mkoani Arusha ambao umepunguza changamoto za ufugaji kwa kujenga mabwawa matatu ya kunyweshea mifugo.

“Mradi huu ni wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi za kimataifa ya mazingira na Maendeleo (IIED), Mfuko wa Umoja wa Mataifa na Maendeleo (UNCDF LoCAL), mashirika yasiyo ya kiserikali ya Haki Kazi (HKC) na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF),” amesema Prof Mayaya.


Zinazohusiana: Dawa ya Ejiao inavyohatarisha kutoweka kwa punda Afrika Mashariki


Kwa Upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Mugabe Mtani amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo ya wananchi umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano iliyojipambanua kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi.

“Katika Kipindi chake cha miaka mitatu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, amerudisha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma, kuimarisha sekta ya kilimo, usafirishaji, miundombinu, na nishati” alisema Bi. Mtani

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Khatibu Kazungu, amekipongeza chuo hicho kwa kushiriki katika ujenzi wa viwanda hatua itakayochochea na kuiwezesha nchi kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa miaka 39 iliyopita na kinatoa mafunzo ya ngazi ya astashahada, stashahada, shahada na shahada ya uzamili.