October 6, 2024

Dawa ya Ejiao inavyohatarisha kutoweka kwa punda Afrika Mashariki

Ni dawa ya asili ambayo hutengenezwa kwa ngozi ya punda na hutumika kupunguza uzee, kuongeza nguvu za kiume, kuzuia ugumba, kuharibika kwa mimba na kusawazisha hedhi kwa wanawake.

  • Ni dawa ya asili ambayo hutengenezwa kwa ngozi ya punda na hutumika kupunguza uzee, kuongeza nguvu za kiume, kuzuia ugumba, kuharibika kwa mimba na kusawazisha hedhi kwa wanawake.
  • Licha ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji punda kimataifa bado baadhi ya watu wanauza kwa magendo katika nchi jirani.
  • Kama hatua hazitachukuliwa kuna uwezekano mkubwa mnyama huyo akatoweka duniani.

Dar es Salaam. Licha ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kukifunga kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilichopo Jijini Dodoma, inaelezwa kuwa biashara isiyo halali ya mnyama huyo inaendelea katika mipaka ya Afrika Mashariki jambo linalotishia kutoweka kwake.

Barua iliyoandikwa na Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Vedast Makota Novemba 5 mwaka huu imeeleza kwamba kiwanda hicho ambacho kinashughulika na uchinjaji na usafirishaji wa nyama ya punda nje ya nchi kwa muda mrefu sasa kimeonyesha kushindwa kuzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira licha ya maonyo kadhaa yaliyofanywa na baraza.

Kabla ya hatua hiyo, mwaka 2016 Serikali iliamua kuruhusu kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wa China kusindika bidhaa za punda nchini ili kuepusha usafirishaji na biashara haramu ya punda nje ya mipaka ya Tanzania. 

Hali hiyo haikuzuia baadhi ya punda kusafirishwa kimagendo hadi Kenya ambako kuna kiwanda cha kusindika ngozi ya punda kijulikanacho kama Goldox Kenya Limited kinachomilikiwa na raia wa China.

Kutokana na uchache wa wanyama hao, bei yake imeongeza mara dufu ambapo vijana hutumia fursa hiyo kuingia katika vijiji na kuiba punda na kuwasafirisha hadi Kenya ili kujipatia fedha nyingi ambazo hutolewa na wanunuzi.

Kwa mujibu wa shirika la Utangazaji la VOA, Biashara hiyo imeathiri shughuli za kiuchumi hasa katika mikoa ya kaskazini ya Arusha na Manyara ambayo iko karibu na Kenya.  Inaelezwa kuwa mwaka jana punda zaidi ya 475 waliibwa ili kusafirisha hadi nchi jirani lakini 175 waliookolewa.


Zinahusiana: 


Licha ya punda hao kupelekwa hadi Kenya, sehemu kubwa ya nyama na ngozi yake husafirishwa hadi China katika kampuni ya Dong-E-E-Jiao ambayo inajihusisha na uagizaji wa ngozi ya punda kutoka nchi mbalimbali duniani ili kutengeneza dawa ya asili ijulikanao kama “ejiao“.

Ngozi ya punda inafika China kupitia nchi mbalimbali ikiwemo Kyrgyzstan, Brazil na Mexico. Lakini Afrika ndio kitovu cha biashara hiyo ikiongoza kwa punda wanaochinjwa na madhara yanayopatikana kwenye uchumi na mazingira.

Kulingana na ripoti ya Msajili wa Dawa za Asili China (2017) inaeleza kuwa mahitaji ya ngozi ya punda yameongezeka kuliko punda waliopo. Inakadiriwa kuwa ngozi milioni 1.8 zinauzwa kila mwaka, huku mahitaji ya dunia ni kati punda milioni 4 hadi milioni 10.  Baadhi ya nchi za Afrika zimepiga marufuku usafirishaji wa nyama na ngozi ya punda kwenda China. Picha| Conservation Action Trust

  

Siri iliyofichika ndani ya dawa ya Ejiao

Ngozi inayopatikana baada ya punda kuchinjwa husagwa na kuchanganywa na kemikali zingine ili kupata dawa ya asili ya Ejiao ambayo hutumika kutibu magonjwa mbalimbali.

Dawa ya Ejiao ambayo hapo awali ilikuwa inatumika kuzuia kuvuja kwa damu hasa kwa watu waliopata majeraha, wakati huu matumizi yake yameongezeka.

Kwa mujibu wa kampuni ya Dong-E-E-Jiao, Ejiao husaidia kupunguza uzee, kuongeza nguvu za kiume, kuzuia ugumba, kuharibika kwa mimba na kusawazisha hedhi kwa wanawake.

Licha ya dawa hiyo kuwepo kwa miaka mingi, lakini ilijipatia umaarufu mkubwa mwaka 2010 baada ya kampuni hiyo kuendesha kampeni ya kuitangaza dawa hiyo ambayo imewavutia watu wengi wanaokabiliwa na matatizo ya uzazi. 

Miaka 15 iliyopita ejiao ilikuwa inauzwa kwa Dola 9 za Marekani lakini sasa imepanda hadi zaidi Dola 400 (Takribani Sh900,000).

Kampuni za China zilianza kununua ngozi ya punda kutoka nchi za Afrika baada ya nchi zilizoendelea kuzuia biashara hiyo kwenye nchi zao ili kuepusha kupotea kwa myama huyo. Lakini sasa nchi za Afrika nazo zimeanza kukabiliana na tishio la kutoweka kwa punda.

Nchi 14 za Afrika ikiwemo Uganda, Botswana, Niger, Burkina Faso, Mali, na Senegal zilizuia biashara ya kimataifa ya punda na bidhaa zake, ambapo Tanzania iliungana na nchi hizo Juni mwaka 2017 kutokana na tishio la kutoweka kwa wanyama hao.

Akihojiwa na gazeti la Financial Times mapema mwaka huu, Makamu rais wa kampuni hiyo, Liu Guangyuan alisema wanaagiza ngozi 450,000 za punda kila mwaka ambapo bei yake imepanda maradufu hadi kufikia Dola za Marekani 473 (Sh1.065 milioni) kwa ngozi moja.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya Ejiao wameanza kujenga vituo vya uzalishaji wa mazao ya punda ili kukidhi usambazaji wa dawa hiyo kwa wateja.

“Hadi 2020 vituo vya uzalishaji vitatengeneza ngozi ya punda ya kutosha kukidhi mahitaji ya msingi,” alinukuliwa Guangyuan.

Amebainisha kuwa wakati wanaendelea kujenga vituo vya uzalishaji, wamezigeukia nchi za Amerika ya Kusini ikiwemo Brazil, Colombia na Mexico ili kukabiliana na zuio la nchi za Afrika.

 Dawa ya asili ya Ejiao inayotumika zaidi nchini China kwa kutibu magonjwa mbalimbali. Picha| Tokopedia

Punda hatarini kutoweka duniani

China ambayo ilikuwa inaongoza kuwa na  punda wengi  duniani, lakini idadi inapungua kila mwaka ambapo punda waliopo katika nchi hiyo ni milioni 6 kutoka milioni 11 na kwa makadirio ya chini inaweza kufikia milioni 3.

Tofauti na wanyama wengine kama nguruwe na ng’ombe, punda hawazaliani sana ambapo jike huzaa mara moja kwa mwaka na wana hatari ya mimba kuharibika kutokana mazingira na kazi ngumu wanazofanya.

Inaelezwa kuwa kuna punda milioni 44 duniani kote, lakini kila mwaka punda milioni 1.8 huchinjwa kwa ajili ya kutengeneza ejiao, hii ni kulingana na ripoti ya taasisi ya Donkey Sanctuary iliyopo Uingereza.

Mwaka 2017, watafiti wa Chuo Kikuu cha Misitu cha China walionya kuwa mahitaji ya ejiao yanaweza kusababisha punda kutoweka kabisa kama ilivyo kwa mnyama pangolin.

“China imeamua kuagiza punda kwa gharama kubwa kutoka maeneo mbalimbali duniani, jambo linaloweza kuitumbukiza dunia kwenye mgogoro mkubwa wa kutoweka kwa punda”, imeeleza  ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye jarida la Equine Veterinary.