October 6, 2024

ACT-Wazalendo waitaka Serikali ikomeshe vitendo vya ukatili dhidi ya wavuvi

Wadai vitendo hivyo vimetokea katika operesheni tatu za kutokomeza uvuvi haramu zinazotekelezwa katika Ziwa Victoria na bahari ya Hindi mwaka huu.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ameitaka Serikali iunge mkono kuwepo kwa chombo cha pamoja kitachowaleta pamoja wadau wa sekta ya uvuvi. Picha| Twitter.


  • Wadai vitendo hivyo vimetokea katika operesheni tatu za kutokomeza uvuvi haramu zinazotekelezwa katika Ziwa Victoria na bahari ya Hindi mwaka huu.
  • Serikali itumie sehemu ya mapato kuimarisha ulinzi wa wavuvi baharini na ziwani na kuwaendeleza kupitia mikopo na pensheni.
  • Amewataka wavuvi washikamane kupitia vyama na vikundi vyao kupaza sauti, kutetea maslahi yao na kupinga unyanyasaji.

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kimeipongeza Serikali kwa kufanikiwa katika operesheni za kutokomeza uvuvi haramu zinazotekelezwa katika Ziwa Victoria na bahari ya Hindi na kuitaka kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wavuvi katika operesheni hizo. 

Operesheni hizo zimetokana na kuwepo kwa uvuvi haramu uliokithiri  hasa mwaka 2017, hivyo mwaka huu wizara ya Mifugo na Uvuvi ilizindua na inatekeleza operesheni kubwa tatu dhidi ya uvuvi haramu; Operesheni Sangara katika Ziwa Victoria, Operesheni Jodari (Bahari ya Hindi) na Operesheni MATT (Dhidi ya uvuvi wa mabomu na baruti).

Operesheni hizo zimeambatana na kufanya doria kwenye bahari, maziwa, mabwawa na mito zinazolenga kukabiliana na wavuvi wanaotumia njia haramu kuvua samaki. 

Akizungumza leo na wanahabari, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho cha upinzani, Ado Shaibu amesema katika kufuatilia matokeo ya operesheni dhidi ya uvuvi haramu, wao kama chama wamegundua uwepo wa mambo yanayoweza kuepukwa na yasiyo ya lazima ili kuhakikisha lengo la Serikali linafanikiwa. 

“Jitihada zozote zinazolenga kutokomeza tatizo la uvuvi haramu zinapaswa kuungwa mkono na mtu anayelitakia mema taifa la Tanzania,” amesema Shaibu.

Amesema kuwa mtu yeyote anayekusudia kurudisha nyuma au kukwamisha jitihada za kutokomeza uvuvi haramu anapaswa kupingwa kwa nguvu zote na kutoa wasiwasi wake juu ya operesheni hizo kutokana na kuwepo kwa mazingira hatarishi kwa wavuvi wadogo.

“Serikali ihakikishe vitendo vya kinyama na kikatili kama vile kupiga wavuvi na kuwatesa vinakomeshwa kwenye operesheni zake,” amesema Shaibu. 

Kwa mujibu wa Shaibu, taarifa iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi karibuni ambayo ilitokana na utafiti uliofanywa na shirika hilo kisiwani Ukerewe inaonesha kwamba baadhi ya wasimamizi wa operesheni Sangara wanatuhumiwa kuvamia makazi ya wavuvi na kuwaibia mali zao, kuwajeruhi wavuvi na kutumia nguvu kupita kiasi.

“Mara nyingi, tofauti na wavuvi wakubwa wa bahari kuu, wavuvi wadogo hawana ubavu wa kupambana na vikosi vya doria na operesheni. Mara nyingi hujisalimisha bila kupambana. Hivyo basi, nguvu kubwa inayotumika ambayo inasababisha watu kufa, kujitosa majini au kujeruhiwa si ya lazima,” amesisitiza Shaibu.


Zinazohusiana: 


Ili kuhakikisha operesheni hizo zinafanikiwa siku zijazo, Serikali imetakiwa kuwashirikisha wavuvi kwenye utungaji wa sheria, kanuni, kutoa makatazo na kwenye programu zake hasa zile zinazowagusa wavuvi moja kwa moja ili wavuvi wapate sehemu ya kusemea matatizo yao.

Vilevile amependekeza Serikali ichunguze juu ya taarifa za vifo vya wavuvi na wafanyabiashara vilivyoripotiwa na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wataobainika kushiriki vitendo hivyo.

Serikali pia imeshauriwa kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuwakwamua wavuvi  ikiwemo kuwapatia mikopo, mitaji na pensheni hasa kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii.  

“Serikali iunge mkono kuwepo kwa chombo cha pamoja kitachowaleta pamoja wadau wa sekta ya uvuvi,”

Pamoja na hayo amewataka wavuvi washikamane kupitia vyama na vikundi vyao kupaza sauti, kutetea maslahi yao na kupinga unyanyasaji kwa kuimarisha ushirika na kuunda chombo cha Kitaifa cha kuunganisha wavuvi nchini ili kulinda maslahi yao ikiwemo kuongeza uzalishaji.

“Wavuvi watoe ushirikiano kwa serikali katika kuwabaini wale wanaojihusisha na uvuvi haramu. Bahari na maziwa vikibaki bila samaki, uvuvi wala wavuvi hawatakuwepo,” amesema Shaibu.