Majaliwa apigilia msumari TCU kufuta vyuo vilivyokosa ubora
Amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini ili viendelee kutoa elimu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa.
- Amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini ili viendelee kutoa elimu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa.
- Lengo ni vyuo vikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu.
- Changamoto ya wahadhili, miundombinu ya kufundishia na kujifunzia husababisha baadhi ya vyuo kushindwa kukidhi viwango vya ubora.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini ili viendelee kutoa elimu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa.
Kauli ya Majaliwa inakuja baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kufuta vyuo zaidi ya viwili na kusitisha mafunzo katika vyuo vingine zaidi ya vitano na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo kuhamishiwa katika vyuo vingine nchini, uamuzi unaowaacha wanavyuo hao katika sintofahamu ya mustakabali wa elimu yao.
Vyuo vilivyotangazwa kufutwa na TCU kwa mwaka 2018 ni pamoja na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji cha Tabora (TEKU), Kituo cha mjini Moshi cha Chuo Kikuu Kishiriki chaKumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo – Town Centre) na Kituo cha Msalato cha Chuo Kikuu Mt. Yohana Tanzania (SJUT) kilichopo mkoani Dodoma.
Amesema suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia ubora na viwango vinavyostahiki.
“Nafahamu jitihada ambazo vyuo vikuu binafsi vinafanya katika kuendeleza Rasilimali Watu wao na hasa katika eneo la taaluma ili viwe na Wahadhili na Maprofesa wa kutosha.
“Nitoe rai kwa vyuo vikuu vyote vizingatie matakwa ya ithibati zao ili viweze kutoa elimu iliyo bora itakayokidhi matamanio ya Watanzania na ushindani wa soko la ndani na nje,” amesema.
Msimamo wa Serikali umetolewa Novemba 23,2018 kwenye mahafali ya tisa ya chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kampasi ya Chifu Mazengo, Jijini Dodoma.
Amebainisha kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi hususan wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania katika maendeleo ya elimu ya juu.
“Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu, ambapo hadi sasa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote,” amesema Majaliwa.
Amebainisha kuwa baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono azma yao vyuo vikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu.
Zinazohusiana:
- Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania
- TCU wafungua dirisha dogo la usajili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
- TCU yaacha maumivu vyuo vikuu, ikivifuta vituo viwali.
TCU katika tamko lake la Novemba 19, 2018 imeendelea kuvishauri na kuelekeza vyuo kurekebisha mapungufu sambamba na kufanya kaguzi za kawaida na zakushtukiza katika baadhi ya Vyuo Vikuu kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ili kujiridhisha kama maelekezo yametekelezwa na mapungufu yaliyobainishwayamerekebishwa.
Majaliwa amesema changamoto ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile mabweni na nyumba za watumishi, husababisha baadhi ya vyuo kushindwa kukidhi matakwa ya ithibati zao na kuzuiwa kufanya udahili au kufungiwa kabisa.
“Ni kweli tunahitaji Watanzania wengi wapate elimu ya juu kwenye vyuo vyetu vikuu. Hata ninyi wanafunzi, mngependa kupata elimu iliyo bora itakayoweza kuwasaidia maishani na itakayowakomboa kifikra, itakayowapa ujuzi na maarifa ya kupambana na changamoto za maendeleo. Kila mmoja anataka elimu bora na si bora elimu,” amesema Majaliwa. Baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa. Picha| Michuzi.
Akizungumzia kuhusu changamoto zinazokabili sekta ya elimu ya juu, amesema baadhi ya changamoto zinafanana katika vyuo vikuu vyote nchini na pia zipo changamoto zinazokabili vyuo vikuu binafsi na wakati mwingine zipo changamoto zinazohusu chuo kikuu kimoja kimoja.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania ambacho kimeomba kuruhusiwa kufanya udahili baada ya kufungiwa, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kujiridhisha iwapo chuo hicho kimekidhi vigezo kabla ya kukipa kibali cha kudahili wanafunzi wapya.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, chuo hicho kimetoa wahitimu zaidi ya 10,000 ambao ni afamasia, wauguzi, walimu wa sayansi, walimu wa anaa, wataalamu wa aabara. wasimamizi na waendeshaji wa fani mbalimbali kama utawala, masoko na wahasibu, mchango ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa Taifa katika nyanja tajwa.