October 6, 2024

Wakulima wanavyoweza kunufaika na uzalishaji wa kakao nchini

Mahitaji yake yanaongezeka kwa kasi duniani hasa katika nchi za Ulaya na Marekani ambako inatumika kutengeneza chokoleti.


  • Mahitaji yake yanaongezeka kwa kasi duniani hasa katika nchi za Ulaya na Marekani ambako inatumika kutengeneza chokoleti.
  • Soko la ndani bado halijaguswa wala kufikiwa, jambo linalotengeneza fursa ya ujenzi wa viwanda na ajira kwa vijana ikiwa mikakati ya kuinua zao hilo itazingatiwa.
  • Matumizi ya teknolojia ya kisasa na mafunzo yatawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji.

Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya chokoleti duniani, wakulima wa Tanzania wanaweza kufaidika na soko la kakao ikiwa watajengewa uwezo wa kulima kisasa ili kuongeza uzalishaji.   

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kakao (ICCO) karibu asilimia 90 ya chokoleti yote inayotengenezwa duniani hutumiwa na nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika ya Kusini, huku asilimia 70 ya chokoleti hiyo hutokana na kakao inayozalishwa  barani Afrika.

Nchi za Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon ndio wazalishaji wakubwa wa kakao barani Afrika licha ya kuwepo maeneo mengine ya Magharibi na Afrika ya Kati ambayo hayajatumia vizuri fursa ya kulima zao hilo.

Nchini Tanzania, zao hilo hulimwa katika Wilaya za Kyela na Rungwe mkoa wa Mbeya ambapo huzalisha zaidi ya asilimia 80 ya kakao yote nchini. Maeneo mengine ni Ifakara-Morogoro na Maramba-Tanga na mchakato wa kulima zao katika mkoa wa Kigoma unaendelea.

Inakadiriwa kuwa Tanzania huzalisha tani 7,000 kila mwaka ambazo ni sehemu ndogo ya uzalishaji wote unaofanyika katika nchi za Afrika Magharibi ambao unazidi tani milioni 2.5 kila mwaka.


Zinazohusiana: Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?


Kutokana na ongezeko la mahitaji chokoleti duniani, wajasiriamali wa Tanzania wanaweza kutumia fursa ya kuzalisha kakao kwa wingi ili kutengeneza kipato cha familia na kuchangia kukuza uchumi kupitia fedha za kigeni.


Kwanini biashara ya kakao ni fursa muhimu kwa wajasiriamali wa Tanzania?

Mti wa kakao asili yake sio Afrika, uliingizwa barani Afrika zaidi ya miaka 100 iliyopita ukitokea Amerika ya Kusini, lakini sasa Afrika ndio mzalishaji mkubwa duniani.  Tanzania inaweza kufaidika na zao hilo kwasababu ni nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo hali ya hewa inaruhusu kulima zao hilo katika baadhi ya maeneo nchini.

Wakulima wakitumia vizuri fursa hii uwezekano wa kupata soko la uhakika la kakao ni mkubwa ikizingatiwa kuwa mahitaji yake yanaongezeka kila mwaka hasa katika nchi zilizoendelea ikiwemo Ulaya na Marekani.

Soko la ndani bado halijaguswa wala kufikiwa. Ikiwa wajasiriamali  watalima kwa wingi kakao na kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo chokoleti na kuweza kuishawishi jamii juu ya faida  za bidhaa hiyo; mafanikio ya kiuchumi yatakuwa makubwa kwa mkulima mmoja mmoja na Taifa.

Wakulima wa kakao wakiwezeshwa kiteknolojia wanaweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuleta faida katika uchumi wa Taifa. Picha| Ecacaos.

Wawekezaji wa zao hilo tayari wameingia katika maeneo mbalimbali ya Afrika ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda na mashamba makubwa ya kakao kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanainuka kiuchumi.

Taasisi ya TechnoServe  inayoendesha program ya Kokoa Kamili, imeanza kuwajengea uwezo wakulima wa kakao mkoani Morogoro kuchangamkia fursa hiyo adhimu Afrika Mashariki.

Simran Bindra na Brian LoBue waanzilishi wa program hiyo wanasema ikiwa Tanzania itajidhatiti na kuwekeza kwenye kakao uwezekano wa kubalisha maisha ya wakulima kiuchumi ni mkubwa.

“Ni sehemu mikakati ya biashara yetu”, amesema Simran. “Mafunzo ya kulima yameongeza ubora ikizingatiwa kuwa kakao ni zao linalokomaa kwa miaka minne. Pia tumeimarisha mahusiano na wakulima kuonyesha kwamba tunajali maisha yao”.

Kokoa Kamili ambayo inayoendesha shughuli zake katika bonde la Kilombero, Kusini Mashariki mwa Tanzania inanunua kakao mbichi na ghafi kutoka kwa wakulima 2,500 ambapo huichachusha na kuikausha kabla ya kuiuza kwa watengenezaji wa chokoleti waliopo Amerika ya Kusini, Ulaya na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwaka 2015, taasisi hiyo ilinunua tani 82 za kakao na kuongeza uzalishaji kwa wakulima kwa asilimia 70. 

Mti wa kakao ni mdogo kwa kiasi cha futi 13 hadi 26, matawi yake ni ya kijani ambapo hulimwa maeneo yenye hali ya hewa ya kitropiki.

Nchi za Afrika ya Magharibi na Kati hasa Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon zina zaidi ya wakulima milioni 2 ambao wanawajibika kuzalisha asilimia 70 ya kakao yote ya dunia.

Mti wa kakao hukomaa na kuanza kuzaa mbegu ambazo huwa ndani ya kokwa (pods) ikifikia miaka 4 au 5 tangu kupandwa. Kwa wastani mti mmoja wa kakao unazalisha matunda 20 hadi 30 wakati wa uvunaji. Kila kokwa hubeba mbegu 20 hadi 50 ambazo hujulikana kama mbegu za kakao.

Baada ya kokwa  kukomaa huvunwa na kupasuliwa ili kupata mbegu  ambazo huwekwa kwenye chombo maalum kwa siku 3 hadi 5 ili zichachuke. Mbegu hizo hukaushwa, huoshwa, hubanikwa na kupitia mchakato wa kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo chokoleti, vinywaji dawa za binadamu na vipodozi.