November 24, 2024

HESLB yafungua dirisha kukata rufaa wanafunzi waliokosa mikopo elimu ya juu

Dirisha la kuwasilisha rufaa litakuwa wazi kwa siku tano, kuanzia leo hadi Novemba 25, 2018 na linawahusu wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au wasioridhika na viwango walivyopatiwa katika mwaka wa masomo wa 2018/19.

  • Dirisha la kuwasilisha rufaa litakuwa wazi kwa siku tano, kuanzia leo hadi Novemba 25, 2018 na linawahusu wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au wasioridhika na viwango walivyopatiwa katika mwaka wa masomo wa 2018/19.
  • Baada ya muda huo kupita wanafunzi watakaokua wametimiza masharti na sifa watapangiwa mikopo kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Novemba, 2018.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha la kukata rufaa kwa wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au hawajaridhika na kiwango cha mkopo walichopangiwa katika mwaka wa masomo wa 2018/2019.

Taarifa ya HESLB iliyotolewa leo (Novemba 21, 2018) imewataka wanafunzi wote wa taasisi za elimu ya juu ambao wanataka kukata rufaa kuziwasilisha kwa njia ya mtandao.

Dirisha la kuwasilisha rufaa hizo litakuwa wazi kwa siku tano, kuanzia leo hadi Novemba 25, 2018 na linapatikana kupitia http.olas.heslb.go.tz ambapo baada ya muda huo kupita wanafunzi watakaokua wametimiza masharti na sifa watapangiwa mikopo kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Novemba, 2018.

Ili kuwasilisha taarifa na nyaraka za rufaa, mwanafunzi anapaswa kufungua mtandao huo, kusoma maelekezo na kutumia namba yake ya mtihani wa kidato cha nne aliyoombea mkopo kwa mwaka huu (2018/2019) kuingia na kuwasilisha taarifa zake kwa njia ya mtandao tu.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hadi leo takribani wanafunzi 37,969 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo na wanaendelea na masomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini. 

Idadi hiyo ya waliopata mikopo ni kati ya wanafunzi 40,000 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kupatiwa mkopo na bodi hiyo yenye makao yake makuu Mwenge jijini hapa.


Zinazohusiana: 


Katika mwaka huu wa masomo, Serikali imetenga Sh427.5 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ambazo zitawanufaisha wanafunzi zaidi ya 120,000 wakiwemo 83,000 wa mwaka wa pili, tatu na kuendelea waliopo vyuoni ambao wamefaulu mitihani yao ya mwaka. 

Hata hivyo, idadi ya wanafunzi waliopata mkopo mwaka huu imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2017/2018 ambapo Serikali ilitenga bajeti ya Sh427 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo waliopata mikopo hiyo walikuwa 33,244 kati ya zaidi ya 66,000 waliotuma maombi.

Oktoba 17 mwaka huu, wakati HESLB ikitangaza orodha ya majina ya wanafunzi waliopata mikopo awamu ya kwanza, Mkurugenzi Mkuu wa HESLB, Abdulrazak Badru alinukuliwa akisema upangaji mikopo unategemea orodha ya wanafunzi waliodahiliwa kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambapo mpaka sasa imefikia wanafunzi 49,000.