October 6, 2024

Majaliwa awataka wananchi kata ya Mnacho kujenga mabweni ya wanafunzi

Mabweni hayo yatawaondolea wanafunzi wa kata hiyo adha ya kutembea umbali mrefu kwenda katika shule ya sekondari Mnacho.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awataka wazazi kushiriki kuboresha elimu. Picha| The Citizen.


  • Mabweni hayo yatawaondolea wanafunzi wa kata hiyo adha ya kutembea umbali mrefu kwenda katika shule ya sekondari Mnacho.
  • Shule hiyo ina wanafunzi 334 lakini wananchi wameanza kujenga bweni lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 tu wa kike.
  • Ataendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika katika hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia kwa wakati.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa kata ya Mnacho wilayani Ruangwa mkoa wa LIndi kujenga mabweni katika shule ya sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni hapo.

Maagizo hayo ameyatoa leo (Novemba 19, 2018) wakati alipotembelea shule hiyo kwaajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni ambalo ujenzi wake unagharimu Sh92.4 milioni ikiwa ni mchango uliotolewa na wadau wa elimu.

“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwasababu wataishi hapa. jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu,” amesema Majaliwa.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio katika kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo bweni linalojengwa sasa haliwezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi wote waliopo shuleni hapo.

Amesema yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika katika hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia kwa wakati.

Pia wananchi hao wametakiwa kushirikiana na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto waliopo shuleni na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja.


 Zinazohusiana: 


Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa shule ya sekondari Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo amesema ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari, 2019.

“Kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni hapa, bweni hili litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu. Tutaendelea kuwaomba wahisani waendelee kutusaidia ili tupate bweni lingine kwaajili ya kuwalaza wanafunzi wa kiume,” amesema Mwakalobo.

Mwalimu Mwakalobo amesema iwapo watafanikiwa kuwa na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shulebi hapo yatawasaidia katika kutatua changamoto ya utoro na kushuka kwa taaluma kwa wanafunzi kwasababu wengi wanatataka maeneo ya mbali.

Mradi wa ujenzi wa mabweni utawawezesha walimu kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni.

“Mradi huu pia utapunguza wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito,” amesema Mwakalobo.

Ameongeza kuwa uwepo wa mabweni shuleni hapo utaongeza ari ya wanafunzi kupenda shule tofauti na hali ilivyo sasa kwasababu wengi wanalazimika kutembea muda mrefu kwa kuwa wanatoka vijiji vya mbali, jambo linalowafanya wasipende shule.