October 6, 2024

Ongezeko la vijana linavyotishia ukuaji wa kilimo vijijini

FAO yashauri vijana wabaki vijijini kuendeleza kilimo lakini wapatiwe ujuzi na teknolojia ya kisasa kuboresha maisha yao.

  • Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya vijana walio na umri kati ya miaka 15 na 24 inatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya milioni 90 ifikapo 2030.
  • Ushindani wa soko la ajira kuongezeka matokeo yake vijana wengi watakimbia kutoka vijijini kwenda mjini kutafuta maisha mazuri.
  • FAO yashauri vijana wabaki vijijini kuendeleza kilimo lakini wapatiwe ujuzi na teknolojia ya kisasa kuboresha maisha yao.

Dar es Salaam. Ripoti ya shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) ya mwaka 2017 imeeleza kuwa ili Tanzania na nchi nyingine za Afrika zikamilishe Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030 zinatakiwa kuzigeukia jamii za watu wanaoishi vijijini kwa kuboresha mfumo wa uzalishaji mazao ya kilimo.

Licha ya kuwepo kwa mikakati ya kuzikwamua jamii za watu waishio vijijini kutoka kwenye umaskini  kuipitia kilimo bado zitihada hizo hazifanikiwa kwa kiwango kinachohitajika kutokana na mabadiliko na mtawanyiko wa nguvu kazi hasa vijana.  

Ripoti ya FAO inaeleza kuwa kati ya mwaka 2015 na 2030, idadi jumuishi ya wakazi wa Afrika na Asia inatarajiwa kuongezeka kutoka bilioni 5.6 hadi zaidi ya bilioni 6.6.

Inabainisha kuwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya vijana walio na umri wa miaka kati ya 15 na 24 inatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya milioni 90 ifikapo 2030, na idadi hiyo itakuwa maeneo ya vijijini.

Ongezeko  la vijana linaweza kutengeneza changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa karne zijazo ukilinganisha na uzalishaji wa sekta ya kilimo na viwanda usiyoendana na mahitaji ya watu barani Afrika. 

Ushindani wa soko la ajira utaongezeka matokeo yake idadi ya vijana wanaokimbia kutoka vijijini kwenda mjini kutafuta maisha mazuri itaongezeka jambo linaloweza kuathiri maendeleo ya sekta ya kilimo. 


 Zinazohusiana: 


Ripoti hiyo inafafanua kuwa ikiwa wananchi waishio vijijini wanataka kuondokana na umasikini ni muhimu wabaki katika maeneo yao kuliko kwenda mjini. Maamuzi hayo lazima yaende sambamba na mabadiliko ya sera zinazosimamia kilimo na kuongeza uwekezaji wa teknolojia utakaowawezesha vijana kulima kilimo cha kisasa.

Vijana wapewe ujuzi na teknolojia ya kisasa kukuza sekta ya kilimo vijijini. Picha| IFAD.

Mshauri na Mtaalamu wa masuala ya Biashara na Maendeleo kutoka taasisi ya Small Starter, John-Paul Iwouha anasema licha ya  maendeleo ya viwanda katika bara la Afrika kwenda taratibu, mabadiliko vijijini yanaweza kufanyika kwa kuinua mfumo wa uzalishaji chakula ili kufikia mahitaji ya wakazi waishio mjini

“Lengo ni kuboresha mfumo wa chakula na kutengeneza fursa mpya za uchumi kwenye shughuli za kilimo ikiwemo kilimo cha biashara, uchakataji, usindikaji, usambazaji na utunzaji. Kuongezeka kwa mahitaji ya soko la vyakula kutoka mjini inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko vijijini,” anasema Iwouha.

Hata hivyo, fursa hiyo kwa wananchi wa vijijini bado ina changamoto ikizingatiwa kuwa itahusisha kuwatoa wakulima kwenye kilimo cha jembe la mkono hadi kwenye mashamba makubwa (large plantation) ambapo kuna uwezekano wa wakulima hao kuwekwa pembeni.

Iwouha anasema ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanamnufaisha kila mwananchi, watunga sera na serikali wanapaswa kuelewa utendaji jumuishi wa jamii na uchumi wa miji, majiji na maeneo ya vijijini na jinsi unavyoweza kuimarisha mfumo wa uzalishaji chakula bila kuwaathiri wakulima wadogo.