Mfumuko wa bei washuka na kuvunja rekodi
Umefikia asilimia 3.2 kwa mwaka ulioshia Oktoba 2018, kiwango ambacho Trading Economics wanasema ni cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa Tanzania.
- Umefikia asilimia 3.2 kwa mwaka ulioshia Oktoba 2018, kiwango ambacho Trading Economics wanasema ni cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa Tanzania.
- Ofisi ya Takwimu ya Taifa imesema bidhaa za vyakula zimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kasi ya bei ya bidhaa na huduma.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini umeshuka hadi kufikia asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2018 kutoka asilimia 3.4 iliyorekodiwa Septemba mwaka huu, ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za vyakula.
Kiwango hicho cha Oktoba kilichotangazwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni cha kihistoria kwa kuwa ni cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa nchini kwa mujibu wa tovuti ya Trading Economics. Kiwango cha juu zaidi cha mfumuko wa bei kuwahi kuripotiwa nchini ni asilimia 19.8 cha Desemba 2011.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
“Mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba umepungua hadi asilimia 1.2 kutoka asilimia 2 kwa mwezi wa Septemba,” inasomeka sehemu ya ripoti ya mfumuko wa bei ya NBS iliyotolewa Alhamis (Novemba 9, 2018).
NBS imesema kuwa baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kupungua kwa kasi ya bei kwa Oktoba ni pamoja na mchele kwa asilimia 3.8 na mahindi asilimia 21.8.
Ukiondoa mchele na mahindi bidhaa nyingine ambazo kasi ya mfumuko wa bei ilipungua ni unga wa mahindi asilimia 11.6, unga wa mtama (5.6), unga wa muhogo kwa (14.1), maharage asilimia (3), mihogo mibichi kwa (5.9), viazi vitamu (2.1), magimbi (23.5) na ndizi za kupika kwa asilimia 11.6.
Nafaka ndio chanzo kikubwa cha mlo kwa familia nyingi za Kitanzania. Picha| Mtandao
Bidhaa hizo hutumika karibu kila kaya nchini kutokana na umuhimu wake kwenye maisha ya kila siku na pia ni chanzo cha kipato kwa wanaojishughulisha na kilimo cha mazao hayo.
“Mfumuko wa bei ukishuka kiuchumi inamaanisha kuwa ukali wa maisha umepungua na thamani ya pesa imeongezeka,” amesema Ande Mathew, mtaalam wa mambo ya uchumi kutoka taasisi ya Just Economy and Joint Action For Human Rights.
Hata hivyo, mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki nao umeshuka ambapo Kenya ulishuka hadi asilimia 5.35 kwa mwaka ulioshia Oktoba kutoka 5.7 uliorekodiwa Septemba mwaka huu. Uganda nako ulishuka hadi asilimia 3 kutoka asilimia 3.7 kwa mwezi ulioshia Septemba 2018.