October 6, 2024

Rais Magufuli awaomba wahisani kujenga viwanda vya dawa nchini

Viwanda hivyo vitaisaidia Serikali kuokoa bajeti inayotumika kuagiza dawa nje ya nchi.

Wataalam wa magonjwa ya Moyo wakimsikiliza Rais Magufuli katika mkutano wa pamoja uliofanyika Ikulu.Picha| http://presstz.net


  • Amesema uwekezaji huo utaisaidia Serikali kupunguza bajeti ya kuagiza dawa nje ya nchi.
  • Wahakikishiwa soko na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.
  • Israel na Marekani kusomesha wataalam wengi zaidi wa afya kutoka Tanzania.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli awaomba wawekezaji wa Israel na Marekani kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya kuzalisha vifaa na dawa za binadamu ili kupunguza gharama za kuagiza toka nje ya nchi.

Amezungumza hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 8, 2018 katika mkutano aliofanya na timu ya waatalam wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Israel na Marekani na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile.

Rais amesema licha ya ongezeko na maboresho makubwa yaliyofanyika katika vituo vya afya, zahanati na   hospitali kubwa bado kuna changamoto ya uhaba wa vifaa na dawa katika sekta hiyo nyeti nchini.

“Tuna Tatizo kubwa la (equipments) vifaa, hivyo nawakaribisha wageni kuja kuwekeza katika viwanda vya vifaa na madawa,” amesema Rais Magufuli.

Amewatoa wasiwasi kuhusu kutokupata wateja kwasababu Tanzania imepewa jukumu la kusambaza dawa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), jambo linaloiongezea wigo wa kunufaika na fursa za viwanda vya dawa vitakavyojengwa nchini. 

Pamoja na hayo Rais ameziomba nchi za Israel na Marekani kuendelea kuisaidia Tanzania katika kuinua sekta ya afya kwa kufungua zaidi milango ya kuwasomesha wataalam wa afya ili kuongeza idadi ya wataalam wanaotakiwa katika maeneo mbalimbali ya matibabu.  

Katika hatua nyingine, Rais amewapa ofa ya bure wataalam hao kutembelea hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini. Pia amesema Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati yake na Israel.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohammed Janabi amesema mafunzo yanayotolewa kwa wataalam wa afya katika nchi za Israel na Marekani yamesaidia kuongeza idadi ya madaktari wa magonjwa ya moyo katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo mpaka sasa imefanya upusuaji kwa wagonjwa 2,855 na kuokoa gharama kubwa za kuwatibu nje ya nchi.  


Zinazohusiana: Magufuli sasa aangazia rada kuongeza mapato Tanzania

                         MSD yashauri vituo vya afya kununua mfuko maalum kwa wajawazito


Awali huduma za upasuaji wa moyo ilikuwa inafanyika nje ya nchi kama India kwa kutumia gharama kubwa ambapo mtu mmoja ilikuwa anatumia Sh29 milioni kusafiri na matibabu.

“Kwa miaka mitatu tumefanya upasuaji wa watu 2,855 ambapo ingechukua miaka 14 kama wangepelekwa India kwa matibabu,” amesema  Prof. Janabi.

Prof Janabi ameweka wazi kuwa bado kuna changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ikiwemo watu wengi kukosa huduma za bima ya afya na kuisababishia taasisi hiyo kupata hasara kila mwaka. 

“Serikali ihimize watu kukata bima ili kupunguza gharama kwa hospitali,” amesema Prof Janabi.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile amesema timu hiyo kutoka Israel ina wataalam 32 ambao wako nchini kwaajili ya kufanya uchunguzi na upasuaji wa moyo kwa watoto 51.

Shughuli nyingine ni kushirikiana na kuwajengea uwezo wataalam waliopo nchini ili kuimarisha huduma za upasuaji katika taasisi ya JKCI.