Majaliwa atoa neno korosho kukosa wanunuzi
Serikali inaendelea kuzungumza na mataifa makubwa ili kuangalia uwezekano wa kuwauzia korosho iliyopo ghalani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awataka wakulima wa korosho kuwa watulivu wakati Serikali ikiwatafutia soko. Picha |Millard Ayo
- Serikali inaendelea kuzungumza na mataifa makubwa ili kuangalia uwezekano wa kuuza korosho ili kuwanufaisha wakulima.
- Awataka wakulima kuwa wavumilivu wakati jitihada za kutatua changamoto ya bei ikitafutiwa ufumbuzi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuzungumza na mataifa makubwa duniani ili kuangalia uwezekano wa kuwauzia korosho kutokana na changamoto zilizojitokeza katika soko la ndani.
Ametoa msimamo huo wa Serikali leo bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kutoka kwa Mbunge wa Mtwara Mjini , Naftaha Nachuma (CUF) ambaye alitaka kujua ni kwanini minada ya korosho inasuasua na kusababisha wakulima kushindwa kuuza zao hilo.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amekiri kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza katika soko la kimataifa la korosho na kusababisha bei ya zao hilo kushuka lakini Serikali inaliangalia kwa karibu suala hilo kwa kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali ili kuwatafutia wakulima soko la uhakika.
“Serikali tunazungumza na Mataifa makubwa moja kwa moja ambapo pia tunaendelea kuuza magunia kwa wanunuzi wanaochukua korosho. Leo hii kutakuwa na kikao na baadhi ya wanunuzi kujua nani wanaweza kununua korosho kwa kiasi gani,” amesema Majaliwa.
Hivi karibuni wakulima wa halmashauri za wilaya ya Newala na Tandahimba mkoani Mtwara waligoma kuuza korosho ghafi katika minada iliyokuwa ikiendelea kutokana na bei ndogo ambayo walieleza kuwa haiendani na gharama za uzalishaji.
Katika msimu huu mpya wa mauzo wa mwaka 2018/2019 bei zilizokatawaliwa na wakulima zilikuwa ni kati ya Sh1,771 na 2,717 kwa kilo moja, ambapo ni chini kwa takriban mara mbili ya zile zilizotumika mwaka jana zilizokuwa zimefikia hadi Sh4,128 kwa kilogramu.
Zinazohusiana:
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Ripoti: Tanzania ni miongoni mwa nchi 11zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Kwanini ufuatilie majadala wa korosho?
Amesema kwasasa hawezi kutoa takwimu za kiasi cha korosho kitakachonunuliwa mpaka wakamilishe mazungumzo na kutatua changamoto zote zilizojitokeza kama walivyofanya kwenye mazao mengine.
“Kwahiyo baada ya kupata mauzo yale na takwimu zikija tutaweza kujibu tani ngapi tumeuza,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo, amewataka wakulima kuendelea kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta masoko katika mataifa makubwa na tayari Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba ameanza kufanya mazungumzo na wadau wengine hapa nchinI, hatua itakalosaidia kuondokana na mkanganyiko wa bei unaojitokeza wakati huu.
“Nitoe ujumbe kwa wakulima na waheshimiwa wabunge wanaotoka kwenye maeneo hayo ya korosho kwamba waendelee kuwa wavumilivu korosho tuitafutie masoko na Serikali tunajitahidi kuhakikisha kwamba zao hili linanunuliwa kama ambavyo tumefanya kwenye zao la kahawa,” amesema.
Oktoba 10 mwaka huu, Rais John Magufuli aliingilia kati sakata la bei ya korosho na kuagiza bei ya zao hilo isipungue Sh3,000 kwa kilogramu na kama wanunuzi wasiponunua kwa bei pendekezwa, Serikali itatumia majeshi kununua na kuhifadhi kwaajili ya kutafuta masoko katika nchi kubwa duniani.