November 24, 2024

Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?

Zao hilo ndiyo liliongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni kuliko mazao mengine yote ya biashara mwaka jana.

  • Zao hilo ndiyo liliongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni kuliko mazao mengine ya biashara.
  • Uuzaji wa korosho nje ya nchi umeongezeka mara dufu ndani ya mwaka mmoja wa 2017.
  • Ni tegemeo la wakulima na familia za mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga na Ruvuma.

Dar es Salaam. Licha ya Rais John Magufuli kuingilia kati sakata la bei ya korosho na kuagiza bei ya zao hilo isipungue Sh3,000 kwa kilogramu, kuna kila sababu ya Watanzania kufuatilia kwa karibu sakata hili kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi nchini.

Hivi karibuni wakulima wa halmashauri za wilaya ya Newala na Tandahimba mkoani Mtwara waligoma kuuza korosho ghafi katika minada iliyokuwa ikiendelea kutokana na bei ndogo ambayo walieleza kuwa haiendani na gharama za uzalishaji. 

Bei zilizopendekezwa katika minada hiyo, iliyokuwa imesimamishwa na Serikali kabla Rais Magufuli kuingilia kati Oktoba 28, zilikuwa ni chini kwa takriban mara mbili ya zile zilizotumika mwaka jana zilizokuwa zimefikia hadi Sh4,128 kwa kilogramu. 

Bei iliyokuwa imefikiwa mwaka jana haijawahi kurekodiwa katika kipindi chote cha nyuma na kwa kiasi kikubwa iliwanufaisha wakulima na kusaidia kuingiza fedha za kigeni Dola za Marekani 541.77 milioni sawa na zaidi ya Sh1.2 trilioni kwa mwaka 2017 pekee kutoka Dola za Marekani 270.6 milioni mwaka 2016.

Hata hivyo, katika msimu huu mpya wa mauzo wa mwaka 2018/2019 bei walizogomea wakulima zilikuwa ni kati ya Sh1,771 na 2,717 kwa kilo moja.

Hali hiyo iliwaibua wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa kuingilia kati sakata hilo na kuungana na wakulima kugomea bei ya sasa ili kuhakikisha bei inapangwa upya itakayoendana na gharama za uzalishaji, usafirishaji na kiwango cha kodi ya Serikali. 

“Kama hamtanunua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima, Serikali itanunua korosho kwa bei nzuri kwa wakulima na tutaihifadhi,” alinukuliwa Rais Magufuli Oktoba 28, 2018 wakati alipokutana na wafanyabiashara na wadau wa korosho na kutoa msimamo wa Serikali wa bei ya zao hilo isiwe chi ya Sh3,000 kwa kilo. 

                           

Meneja wa Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) Mohammed Nassoro ameiambia Nukta kuwa bei mpya iliyotolewa na Rais Magufuli angalau itasaidia wakulima kufidia gharama za uzalishaji na kuwapatia faida.

“Wakulima wamepokea vizuri bei hiyo lakini kikubwa tunasubiri minada ijayo kuona iwapo namna wanunuzi watakavyo ‘respond’ (watakavyoitikia) bei ya Sh3,000 kwa kilo,” amesema Nassoro anayesimamia moja ya vyama vikubwa vya ushirika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Nassoro amesema sehemu kubwa ya tatizo hilo limetokana na mfumo wa awali unaowapa wanunuzi fursa ya kutangaza bei yao wanayotaka bila kuzingatia uhalisia wa soko.

“Katika kikao cha juzi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilibainika kuwa mnunuzi mmoja katika mnada wa Liwale wa tarehe 24 alitangaza bei ya Sh2,657…alivyoenda Lunali Oktoba 25 alitangaza Sh2,400 na katika mnada mwingine tena mnunuzi yule yule alitangaza Sh2,350 kwa kilo,” amesema Nassoro na kuongeza; “Hii inaashiria hali ya mashaka.”


Zinazohusiana:


Mmoja wa wakulima wa korosho wilayani Masasi mkoani Mtwara, Ally Nampwita ameiambia Nukta kuwa bei iliyokuwa imetangazwa awali na wanunuzi ilikuwa haiwezi hata kurudisha gharama za uzalishaji ambazo “kiuhalisia ni zaidi ya Sh2,000 kwa kilo”.

“Sh3,000 iliyotangazwa italeta ahueni japo siyo kama tulivyotarajia awali. Tulitarajia kuwa angalau mwaka huu tungeuza kati ya Sh4,100 na Sh4,300 kwa kilo lakini nilivyoenda minada ya Nanyumbu na Newala nilishtushwa sana kuona bei ambayo haifikii gharama ya uzalishaji kwa kilo,” amesema.

Mapema Jumapili iliyopita, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alieleza kuwa aliitupia lawama Serikali kwa kile alichokiita “kutowasikiliza wabunge kuhusu maslahi ya wakulima wa korosho kufuatia uamuzi kuhamisha fedha za ushuru wa mauzo ya zao hilo nje ya nchi na kuzipeleka hazina”.

“Serikali inunue korosho hii kwa bei ya Sh4,000 kama ilivyokuwa mwaka jana. Ikiishanunua iwauzie watu wa minada hata wakipata hasara haina shida na si mkulima apate hasara kwasababu kwa hali ilivyo hivi sasa, mwananchi ndio anaumia,” alisema Zitto wakati akiongea na wanahabari jijini Dar es Salaam. 

Kwanini korosho imeibua mjadala?

Korosho ina upekee wake katika maisha ya watanzania hasa wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kwa kuwa hutegemea zao hilo kujiingizia kipato ambacho hutumika kutunza familia na kusomesha watoto ili kuondokana na umaskini katika jamii.

Lakini kupitia korosho wanalipa ushuru na kodi kwa Serikali ili kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya katika maeneo yao. 

Katika hali hiyo wakulima wamejitoa na kuwekeza nguvu zao nyingi wakitarajia zao hilo liwe mkombozi wa maisha yao, lakini soko linapoyumba linawaacha katika wakati mgumu wa kuamua hatma yao kujihusisha na kilimobiashara.

Korosho ni zao muhimu la biashara kutokana na mchango wake katika pato la Taifa kwasababu sehemu kubwa husafirishwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017, korosho ndiyo zao la biashara lililoongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni kuliko mazao mengine, jambo linaloiweka katika nafasi ya kupewa kipaumbele na kuwekewa mikakati ya kuiendeleza. 

Mathalani,  mwaka 2017 thamani ya mauzo ya korosho nje ya nchi ilikuwa Sh1.2 trilioni ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya tumbaku iliyoshika nafasi ya pili kwa mauzo ya Sh430 bilioni. Pia korosho imeyapita kwa mbali mauzo ya mazao mengine ya biashara kama kahawa, karafuu, chai, pamba na katani ambayo yamekuwa yakitegemewa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Mauzo ya korosho nje ya nchi yaliongezeka kwa kasi hadi kufikia tani 331,100 kwa mwaka 2017, ikiwa ni mara mbili ya kiwango kilichorekodiwa mwaka 2016 cha tani 169, 200. Kiwango cha mauzo ya korosho nje ya nchi kilichorekodiwa mwaka jana hakijawahi kufikiwa kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita. 

Takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaeleza kuwa katika uzalishaji, korosho imeendelea kufanya vyema ambapo mwaka jana uzalishaji wa korosho ulifikia tani 265,238, ikiwa ni kiwango kikubwa ukilinganisha na miaka iliyotangulia. Mwaka huu, Rais Magufuli amesema inatarajiwa kuwa uzalishaji utafikia tani 220,000. 

“Ongezeko hili lilitokana na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo, matumizi ya teknolojia na zana za kisasa, kuimarika kwa bei ya mazao katika soko la dunia na hali nzuri ya hewa. Mazao yaliyokuwa na ongezeko la uzalishaji ni pamoja na korosho, tumbaku, sukari na pareto.,” inaeleza sehemu ya kitabu cha hali ya uchumi wa taifa.

Ni dhahiri kuwa korosho ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi na mikakati zaidi ya kuboresha zao hilo inatakiwa kuimarishwa ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, teknolojia na soko la uhakika nje ya nchi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. 

Mfumo huo tangu kuanzishwa kwake umekuwa sehemu muhimu ya kuboresha bei ya zao la korosho ambayo imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 17.8 kwa mwaka kutoka Sh720 kwa kilo mwaka 2007/08 hadi Sh2,350 kwa kilo mwaka 2016/17.

(Nyongeza na Nuzulack Dausen) (Habari hii imeboreshwa kwa kuongeza video Oktoba 31, 2018)