Bilionea Mo Dewji apatikana baada ya kutekwa kwa siku nane
Kamanda Mambosasa amesema watekaji walimtelekeza Gymkana na gari lililokuwa linasakwa na polisi.
- Kamanda Mambosasa amesema watekaji walimtelekeza Gymkana na gari lililokuwa linasakwa na polisi.
- Bilionea huyo yupo salama wala hajaumizwa eneo lolote zaidi ya kuchubuka mikononi kwa sababu ya kamba.
- Polisi wasema watekaji walikuwa wanampa hadi chakula.
- Walimuachia baada ya kuona msako mkali unaendelea.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji aliyekuwa ametekwa kwa zaidi ya wiki sasa amepatikana akiwa salama na mwenye afya njema.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa ameiambia Nukta kuwa watekaji walimtelekeza Dewji maarufu kama Mo Saa 8:30 usiku katika viwanja vya Gymkana jijini hapa pamoja na gari ambalo vyombo vya dola vilikuwa vikilisaka.
Taarifa za kupatikana kwa Mo, aliyetekwa Oktoba 11, 2018 akiwa anaingia kufanya mazoezi katika hoteli ya Collesseum Oysterbay jijini hapa, zilianza kusambaa mapema Saa 9 alfajiri katika mitandao ya kijamii hususan Twitter.
Mambosasa amesema kuwa Mo ni mzima wa afya wala hakudhuriwa na watekaji wake kwa sababu walikuwa wakimpa hadi chakula.
Zaidi ya michubuko kidogo na damu damu mikononi alimwokuwa amefungwa kamba, Mambosasa anasema hakuna sehemu nyingine ambayo Mo ameumizwa.
Kamanda huyo ameeleza kuwa inaonekana kuwa alitekwa kwenye chumba ndani ya miongoni mwa nyumba ambazo zilikuwa zikikaribiwa kufikiwa na polisi katika uchunguzi uliokuwa ukiendelea.
“Mo ametumbia kuwa baada ya kutekwa walitembea kwa kasi kama dakika 15 hivi na kufika katika eneo hilo alilotekwa. Walimfunga mikono, miguu na kumziba uso asione hivyo hakuweza kuwa ‘identify’ (kuwatambua) waliomteka hadi anaachiwa,” amesema Mambosasa kwa njia ya simu alfajiri ya leo Oktoba 20, 2018.
Amesema kuwa inaonekana kuwa watekaji walishtushwa na msako mkali uliokuwa ukiendelea na kwamba taarifa zao nyingi zilikuwa zimeshaanza kujulikana na umma na kwamba waliona wasingekuwa salama.
Zinazohusiana:
- RC Makonda aeleza mazingira ya kutekwa Bilionea Mo Dewji
- Dau la Bilioni 1 kutolewa kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Bilionea Mo Dewji
- Polisi kumsaka Mo Dewji nje ya Tanzania.
Watekaji hao, kwa mujibu wa Mambosasa nao walikuwa na “intelijensia” iliyokuwa ikiwapa taarifa juu ya msako uliokuwa ukiendelea.
“Ametuambia kuwa kadri siku zilivyokuwa zinaenda ‘frustration’ ya watekaji ilizidi kuwa kubwa kuliko hata aliyetekwa. Walivyoona msako unakua mkali kwa kutumia ufuatiliaji wa baadhi ya picha za CCTV tulizobahatika kuzipata wakaenda kumdump pale Gymkana pamoja na gari tulilokuwa tunalisaka,” amesema.
Mambosasa amesema lengo kuu la watekaji lilikuwa kujipatia kipato kutoka kwa bilionea huyo lakini walishindwa kumwambia kiwango walichokuwa wakihitaji licha ya yeye kuwaomba wataje ili familia iweze kukitoa na kufanikisha kuachiwa kwake.
Katika video ambayo imerushwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwa na Mambosasa, Mo amesema; “Namshukuru mwenyezi Mungu. Pia, namshukuru mheshimiwa Rais na Jeshi la Polisi, Asanteni sana…mimi ni mzima…nawashukuru Watanzania wote kwa kuniombea mimi ni mzima”.