October 6, 2024

Sakata la kutekwa Mo Dewji lamuibua Lema ataka uchunguzi wa kimataifa

Aitaka Serikali ishirikiane na wapelelezi wa kimataifa kuchunguza tukio hilo ili kuondoa hofu na mashaka yanayoendelea katika jamii.

  • Aitaka Serikali  ishirikiane na wapelelezi wa kimataifa kuchunguza tukio hilo ili kuondoa hofu na mashaka yanayoendelea katika jamii.
  • Amesema suala hilo lisiposhughulikiwa kikamilifu linaweza kuathiri uchumi wa nchi.
  • Vingozi wa dini, taasisi mbalimbali zaaswa kuendelea kupaza sauti ili kupunguz matukio ya utekaji nchini.

Dar es Salaam. Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema ameitaka Serikali  ishirikiane na wapelelezi wa kimataifa kuchunguza tukio la kutekwa bilionea Mohammed Dewji (Mo) ili kuondoa hofu na mashaka yanayoendelea katika jamii.

Kauli ya Lema inakuja siku moja baada ya familia ya Mo kuahidi kutoa Sh1 bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mfanyabiashara huyo aliyetekwa Oktoba 11 mwaka huu katika hoteli ya Collesseum iliyopo Masaki Jijini Dar es Salaam. 

Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema amesema matukio ya kutekwa na kupotea kwa watu yameanza kuzoeleka katika jamii na ili kuondokana na dhana hiyo ni vema Serikali ikaruhusu wapelelezi wa kimataifa kuja nchini kutegua kitendawili hicho.

“Ni lazima sasa Serikali walete wachunguzi wa kimataifa waje wasaidiane na wapelelezi walioko hapa kubaini nani anawajibika katika matukio haya ya utekaji yanayoendelea,” amesema Lema.

Amesema kuomba msaada kutoka nje sio udhaifu bali itaongeza uwajibikaji na ujasiri wa mamlaka katika kushughulikia matukio ya kutekwa kwa raia ambao wanapaswa kuhakikishiwa usalama na mali zao.

“CHADEMA tunaitaka Serikali iruhusu wapelelezi wa kimataifa waje kuchunguza suala hili kinyume na hapo tutaendelea kuishuku Serikali kuhusu utekaji huu,” amesema.  

Aidha, amesema tukio la kutekwa kwa Mo limeleta mshtuko na kujenga hofu kwa wananchi na wafanyabiashara jambo linaloweza kuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi na wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini.

Pia amewataka watu kuendelea kupaza sauti kukemea vitendo vya utekaji vinavyoendelea nchini ili wahusika watafutwe na kuchukuliwa hatua za kisheria kwasababu Mo ana mchango mkubwa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa. 

“Ni wito wangu kwa viongozi wa dini, taasisi  ambazo zinashughulika na mambo ya viwanda watoke hadharani wapige kelele kwa sauti kwamba tuungane sasa, wasipofanya hivyo kuna mwingine atachukuliwa kwasababu wameona na wameshuhudia kwamba mambo haya yanafanyika na hakuna kitu kinachofanyika,” amesema. 


Zinazohusiana:


Baadhi ya watu ambao walipotea katika mazingira ya kutatanisha na hawajulikani walipo ni pamoja na Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited, Azory Gwanda na Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane.

Hata hivyo, Oktoba 13 mwaka huu, Waziri wa mambo ya Ndani, Kangi Lugola alinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa bado nchi iko salama ambapo Jeshi la Polisi litaendele kutekeleza wajibu wake wa kulinda wananchi na wawekezaji.

“Serikali inawahikishia wawekezaji kuwa nchi yetu iko salama, tukio la Mo Dewji lisiwe kikwazo kwao kuwekeza nchini kwetu. Tutazidi kuimarisha usalama, hakuna haja ya kuwa na hofu. Nchi gani duniani wataenda yenye usalama kama Tanzania? Hakuna!,” alinukuliwa Lugola.

Hadi sasa zimepita siku tano tangu Mo mwenye umri wa miaka 43 na tajiri namba moja Afrika Mashariki atekwe na watu wanaodhaniwa ni raia wa kigeni “wazungu” ambapo mpaka sasa haijulikani alipo.

Baadhi ya watu wanashikiliwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kutokana na tukio hilo.