October 6, 2024

Bosi mpya CRDB aweka wazi mipango mitano kuinua sekta ya benki nchini

Mipango hiyo ni pamoja na kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wananchi wengi wa vijijini.


Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Ally Laay wakati wa kumtambulisha rasmi kama bosi mpya. PIcha| Michuzi.


  • Mipango hiyo ni pamoja na kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wananchi wengi wa vijijini. 
  • Ifikapo mwaka 2022 benki hiyo itakuwa imefika katika wilaya zote nchini. 
  • Dk Charles Kimei amepumzishwa kabla ya muda wake kumalizika kwababu ni vigumu kwa benki hiyo kuwa na wakurugenzi wawili kwa wakati mmoja.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameweka wazi mipango yake mitano ya kuinua sekta ya benki nchini ikiwemo uwekezaji katika mifumo ya kidijitali na kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wananchi wengi wa vijijini.  

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo (Oktoba 10, 2018), wakati wa akitambulishwa rasmi kuiongoza benki hiyo, amesema mifumo hiyo itawezesha kuwafikia wateja wengi kwa urahisi popote walipo na kuwaondolea ulazima wa kwenda kwenye matawi ya benki hiyo yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tutatumia fursa ya zaidi ya watanzania milioni 19.3 wanaotumia simu za mkononi kufanya miamala yao na kuwashawishi kutumia bidhaa zetu za SimBanking na SimAccount ambazo nazo hutoa huduma kama hizo,” amesema Nsekela. 

Amebainisha kuwa kuna maeneo ambayo benki hiyo haijafika, lakini kwa kutumia simu ya mkononi mteja atapata huduma zote za kibenki popote alipo. 

Hilo litaenda sambamba na kusogeza karibu huduma za kibenki kwa wateja ikiwemo kufika katika wilaya zote ifikapo mwaka 2022 na kuongeza idadi ya mawakala wa FahariHuduma kila kona ya nchi. 

Nsekela amebainisha kuwa mkakati mwingine ni kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma kwa wateja ili ziendane na mahitaji halisi ya wananchi na soko kwa kuimarisha mahusiano na wateja wao. 

“Tutakuwa tukiboresha mara kwa mara taratibu za kutoa na kupata huduma zetu. Tunataka upatikanaji na utoaji wa huduma za CRDB uwe rahisi huku tukiendelea kuzisogeza huduma hizo karibu na wateja wetu,” amesema.

Aidha, ataongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinazingatia viwango vya ubora, jambo litakalosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya benki na wateja ambao ni sehemu muhimu ya mafanikio ya ukuaji wa taasisi hiyo. 

Amefafanua kuwa chini ya uongozi wake ataimarisha uhusiano na serikali na wadau wengine ili kuongeza wigo wa biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo. 

“Benki ya CRDB itaendelea kujivunia mahusiano yake na serikali na taasisi zake na tutaendelea kubuni bidhaa na huduma mbalimbali mahususi kwaajili ya kufikia mahitaji ya Serikali na wafanyakazi wake mmoja mmoja,” amesema. 


Zinazohusiana: 


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Ally Laay emesema wataendelea kutoa ushirikiano na kuwa wameamua kumpumzisha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk Charles Kimei kabla ya muda wake kumalizika kwababu ni vigumu kwa benki hiyo kuwa na wakurugenzi wawili kwa wakati mmoja.

Bodi hiyo imeeleza kuwapo kwa kipindi cha mpito cha takribani miezi minane ambacho Mkurugenzi Mtendaji mpya aliyetambulishwa leo angefanya kazi na Dk. Kimei aliyemaliza muda wake.

“Tuliamua Dk Kimei apumzike na kumpisha Mkurugenzi Mtendaji mpya kwa kutilia maanani misingi ya utawala bora na maadili yetu ya kazi ingeleta ugumu kwa benki kuwa na wakurugenzi watendaji wawili kwa pamoja kwa kipindi kirefu,” amesema Laay.