Kilovoti 200 za umeme kuchochea maendeleo kijiji cha Mwamashimba mkoani Tabora
Awali walikuwa wanatumia umeme wa kilovoti 100, jambo lilozuia ukuaji wa viwanda vidogovidogo vya kusaga na kukoboa nafaka, kukamua mafuta yatokanayo na uchomeleaji vyuma.
- Awali walikuwa wanatumia umeme wa kilovoti 100, jambo lilozuia ukuaji wa viwanda vidogovidogo vya kusaga na kukoboa nafaka, kukamua mafuta yatokanayo na uchomeleaji vyuma.
- TANESCO yaagizwa kuongeza nguvu ya umeme katika vijiji vyenye uhitaji mkubwa nchini kulingana na mahitaji ya kila kijiji.
- Wananchi hao wataunganishiwa huduma hiyo ya umeme katika nyumba zao kwa bei nafuu ya Sh27,000.
Dar es Salaam. Neema ya umeme wa gridi inawashukia wakazi wa Kijiji cha Mwamashimba katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya umeme kijijini hapo kwaajili ya shughuli za maendeleo.
Wakazi wa kijiji hicho wamekuwa mstari wa mbele kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa viwanda vidogodogo vinavyojumuisha mashine za kusaga na kukoboa nafaka, mashine za kukamua mafuta yatokanayo na mbegu pamoja kuwepo kwa shughuli nyingi za uchomeleaji vyuma.
Hayo yamejili wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kukagua utekelezaji wa usambazaji na kuwasha huduma ya umeme vijijini kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 (400kV Backbone BTIP) katika mkoa wa Tabora ambapo ameliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuongeza nguvu ya umeme katika vijiji vyenye uhitaji mkubwa nchini kulingana na mahitaji ya kijiji husika.
“Hapa Mwamashimba kunahitajika umeme zaidi , watu wamejiajiri kwelikweli, wanafanya shughuli za maendeleo, hii ndiyo sera ya Serikali ya awamu ya tano, kwamba umeme uwafikie wananchi na uwanufaishe kwa kubadili maisha yao,” amesema Mgalu
Amesema transfoma iliyofungwa kijijini hapo haikidhi mahitaji ya shughuli zao ni nyingi, TANESCO wahakikishe wanaongeza transfoma nyingine yenye uwezo mkubwa walau wawe wanapata umeme wa kilovoti 200 kutoka 100 ya sasa, ili wahamasishe na vijiji vingine katika shughuli za maendeleo.
Katika ziara hiyo, Mgalu aliwataka wananchi waliopitiwa na mradi wa BTIP kujiandaa kwa kusuka nyaya katika nyumba zao ili mkandarasi anapopita katika maeneo yao wawe tayari kuunganishwa na huduma hiyo kwa bei nafuu ya Sh27,000.
Zinazohusiana:
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya taifa.
- Namna umeme unavyoweza kuchochea maendeleo vijijini.
Aidha amewatoa hofu wananchi wote wa maeneo husika kuwa watapata huduma ya umeme kwasababu wakandarasi wamefanya upimaji, ramani ya utekelezaji, usambazaji na uunganishaji wa umeme katika vijiji vyote vilivyopitiwa na BTIP uko tayari.
Amewataka wananchi hao pamoja na wakandarasi kushirikiana pamoja katika kutekeleza mradi huo katika maeneo yao, pia wananchi wa eneo husika wapatie fursa ya ajira kulingana na uwezo wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Akiwa wilayani humo, Mgalu aliwasha huduma ya umeme katika vijiji vya Mwabakima, Mwamashimba na kukagua kazi ya utekelezaji wa mradi huo inayoendelea katika kijiji cha Jogohya.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikagua utekelezaji wa usambazaji na kuwasha huduma ya umeme vijijini kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 (400kV Backbone BTIP) katika mkoa wa Tabora. Picha| Wizara ya Nishati.