November 24, 2024

Mafuriko Ziwa Nyasa yalivyozipa thamani fukwe za Ngonga

Mafuriko hayo yalitokana na uamuzi wa Rais wa Malawi wa wakati huo, Kamuzu Banda kuzuia maji ya Ziwa Nyasa yasiende upande wa Msumbiji.

  • Mafuriko hayo yalitokana na  uamuzi wa Rais wa Malawi wa wakati huo, Kamuzu Banda kuzuia maji ya Ziwa Nyasa yasiende upande wa Msumbiji.
  • Ngonga zinazopatikana kilomita 15 kutoka mji wa Kyela na kilomita 140 kutoka uwanja wa ndege wa Songwe uliopo Mbeya mjini.   
  • Ni fukwe zilizosheheni vivutio vingi ikiwemo miti ya asili, samaki aina ya 400, mamba, viboko na mchanga laini.

Kyela. Ukitaja Kyela hautaitenganisha na umaarufu wa uzalishaji wa mchele na kilimo cha kakao.  Wengine hawataacha kutaja mpaka wa Kasumuro unaotenganisha Tanzania na Malawi, unaojulikana kama ‘border’.

Zote hizo ni sifa za Halmashauri ya Wilaya ya Kyela iliyopo mkoa wa Mbeya; Kusini Magharibi mwa Tanzania.

Kinachoipa thamani kipingine halmashauri hiyo ni uwepo wa vivutio vingi vya utalii kama fukwe za Ngonga zinazopatikana kilomita 15 kutoka mji wa Kyela na kilomita 140 kutoka uwanja wa ndege wa Songwe uliopo Mbeya mjini. 

Fukwe hizo zipo kwenye kijiji cha Ngonga ambacho ni miongoni mwa vijiji vichache Tanzania ambavyo vimefanikiwa kutunza asili yake, licha ya mabadiliko mbalimbali ya tabia ya nchi yanayotokea.

Mandhari ya fukwe za Ngonga inapambwa zaidi na uwepo mchanga laini na misitu yenye miti ya mizeituni, kakao na michikichi ambayo hutumika kuzalisha mafuta ya mawese na mbao za kutengenezea thama


Zinazohusiana:


Zina ukubwa wa hekali moja  katika mwambao wa Ziwa Nyasa ambalo linapokea maji yake kutoka mto Songwe na Kiwila. Fukwe hizo ni mpya na hazina uhusiano na fukwe za Matema ambazo zimezoeleweka masikioni mwa watu wengi wanaotembelea Kyela.

                         

Mkurugenzi Mtendaji wa Ngonga Beach Resort, Kennedy Mwamunyange akifafanua umaarufu wa fukwe za Ngonga. Video| Daniel Samson.

Chimbuko la fukwe hizo ni mafuriko

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Ngonga Beach Resort, Kennedy Mwamunyange anasema awali eneo la fukwe za Ngonga lilikuwa makazi ya watu lakini mafuriko yaliyotokea mwaka 1979 yalikifunika kijiji hicho.

Mafuriko hayo yaliyotokana na hatua ya  Rais wa Malawi wa wakati huo, Kamuzu Banda kuzuia maji ya Ziwa Nyasa yasiende upande wa Msumbiji.

Mwamunyange ambaye ni mzaliwa wa Ngonga anasema hali hiyo ilisababisha  ziwa hilo kufurika na maji kuingia kwenye makazi ya watu kikiwemo kijiji cha Ngonga na kuharibu mashamba na nyumba za wanakijiji. 

“Hili ziwa ni kubwa mno linaanzia Matema beach linafika mpaka Mbamba Bay (Ruvuma), Msumbiji linakwenda mpaka Malawi, hapa tuko karibu sana na mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto Songwe,” anasema.

Wakazi hao waliondoka na kutafuta maeneo mengine ya kuishi katika miji ya Tukuyu, Mbeya, Mbozi na Iringa.

Baada ya kupita muda mrefu maji katika eneo hilo yalipungua na baadhi ya watu walirudi tena ambapo Mwamunyange alinunua sehemu ya eneo hilo na kuliboresha kisha kujenga hoteli ya kisasa na fukwe kwa lengo la kuendeleza vivutio vya utalii vilivyopo katika eneo hilo.

“Nilipomaliza kufanya utafiti nikaanza kununua miji ambayo watu waliiacha wakaniuzia, hii ni beach (fukwe) mpya kabisa iko mbali na Matema. Lengo langu ni kuleta maendeleo kijijini, kutoa nafasi za ajira kwa wanakijiji wa huku na ambao tunao hapa tunawalipa mshahara wananufaika,” anasema Mwamunyange.


Kwanini ukatalii Ngonga Beach Resort

Fukwe za Ngonga ni paradiso ya duniani kutokana na asili yake ya mchanga laini wenye mazingira ya kuvutia yanayoambatana na upepo mwanana kutoka ziwani. 

Ukifika Ngonga utapokelewa na kupelekwa kwenye mgahawa wenye aina mbali ya vyakula vya asili na kimataifa, duka la zawadi, mitumbwi na boti za safari ili kujionea viboko, samaki na mamba wanaopatikana kwenye ziwa Nyasa.

Msimamizi wa Mgahawa wa fukwe hizo, Harry Duma anasema, “Hotel yetu inatoa huduma mbalimbali za malazi, chakula cha asili na cha kimataifa. Tuna baa ya Itete na viti vya asili ambavyo vinakupa muonekano mzuri na upepo wa ziwa Nyasa na Milima ya Livingstone.”

Pia utapata nafasi ya kucheza mpira wa miguu, pete na michezo mbalimbali ya ufukweni. Fukwe za Ngonga zinafahamika kimataifa kwa utajiri wa asili, usiri, aina mbalimbali za samaki kama Mbelele na Usipa ambazo zimelifanya Ziwa Nyasa kuwa na kina cha mita 702 kwenda chini.

“Ndani ya hili ziwa kuna samaki aina zaidi ya 400, dunia nzima hawapo wanapatikana ziwa hili tu. kuna wale samaki wengi wanatumia kuwaweka kwenye maboski kama mapambo wanapatikana hapa tu dunia nzima,” anasema Mwamunyange.

Muonekano wa fukwe za Ngonga Wilayani Kyela. Picha| Daniel Samson.

Kwa wale wanaopendelea utalii wa ziwani, basi Ngonga resolt ina mitumbwi ya asili, boti ya MV Livingstone itakayokutembeza katika maeneo mbalimbali ya ziwa ambako huko utajionea viboko, samaki na mamba.

Ngonga Beach Resort inafungua milango kwa vivutio mbalimbali vilivyopo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambavyo vinaweza kuiingizia nchi mapato na kutengeneza ajira kwa vijana.

“Utalii Nyanda za Juu Kusini umesahaurika sana kwasababu watu wengi wameenda kuwekeza Arusha, mzungu yoyote anajua Ngorongoro, Serengeti wakati huku kuna vivutio vingi kuna daraja la Mungu, Ziwa Ngozi, kile kimondo (Mkoa wa Songwe). Tunaiomba serikali itusaidie sisi wazawa kuwa na mazingira mazuri ya kuendeleza vivutio vya utalii,” anabainisha Mwamunyange.