Waitara kuongoza tume ya uchunguzi wa ajali ya Mv Nyerere
Tume hiyo ya watu saba itafanya kazi kwa mwezi mmoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atawapatia hadidu za rejea kwa ajili ya uchunguzi huo.
- Tume hiyo ya watu saba itafanya kazi kwa mwezi mmoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atawapatia hadidu za rejea kwa ajili ya uchunguzi huo.
- Sanjari na uteuzi wa tume hiyo, Majaliwa amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Temesa, Dk Mussa Mgwatu kupisha uchunguzi wa ajali hiyo.
- Kuongeza ufanisi wa usafiri, Rais John Magufuli ameagiza itangazwe mara moja zabuni ya kuunda kivuko kipya chenye uzito wa tani 50 na chenye uwezo wa kubeba zaidi abiria 200 kwa ajili ya eneo hilo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza tume ya uchunguzi ya watu saba itakayochunguza chanzo cha ajali ya kivuko cha Mv Nyerere itakayoongozwa na Jenerali Mstaafu George Waitara.
Majaliwa, aliyekuwa akizungumza baada ya kupata ripoti ya maendeleo ya uokoaji na ugeuzaji wa kivuko hicho leo asubuhi (Septemba 24, 2018), amesema tume hiyo inatakiwa kuanza kufanya kazi hiyo mara moja na itatakiwa kufanya kazi kwa mwezi mmoja.
Kivuko cha Mv Nyerere kilichotengenezwa mwaka 2004, kilipinduka Septemba 20 mwaka huu mita chache kufika mwaloni katika Kisiwa cha Ukara huku uchunguzi wa awali ukubaini kuwa kilikuwa kimezidisha abiria na mizigo.
Wengine wanaounda tume hiyo ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi na aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) Mercelina Magesa ambaye ni mhandisi kitaaluma.
“Mwingine ni wakili Julius Kalolo ambaye tunataka atufanyie mapitio ya sheria, mfumo mzima na uendeshaji wa vivuko,” amesema Majaliwa katika matangazo yaliyoonyeshwa mubashara na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Tume hiyo itaundwa pia na Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Queen Mlozi, Ofisa Mwandamizi wa polisi, Camillus Wambura na Bashiru Hussein ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu. Mlozi atasimamia stahili za kina mama katika uchunguzi huo.
“Nataka kazi hii ianze mara moja na nitakuja niwape hadidu za rejea,” amesema Majaliwa.
Zinazohusiana: Mv Nyerere yaondoka na bodi mbili ndani ya saa 24
Namna waathirika wa ajali ya Mv Nyerere wanavyoweza kusaidiwa kisaikolojia
Sanjari na kutangaza tume hiyo, Majaliwa amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Temesa, Dk Mussa Mgwatu kupisha uchunguzi wa ajali ya kivuko hicho kilichogharimu maisha ya watu 227 hadi Jumatatu mchana. Watu 41 waliokolewa wakiwa hai akiwemo Fundi Mkuu, Augustino Charahani aliyeokolewa siku mbili baada ya kivuko kupinduka.
Amesema Dk Mgwatu alikuwa msimamizi mkuu wa vivuko vyote nchini hivyo atakuwa miongoni mwa watu watakaohojiwa na tume hiyo iliyounda leo.
Ili kuhakikisha huduma za usafiri zinarejea na zinafanywa kwa ufanisi mkubwa kuliko awali, Majaliwa amesema Rais John Magufuli ameagiza itangazwe zabuni ya kuunda kivuko kipya mara moja.
Kivuko hicho kipya, amesema kinatakiwa kiwe na uzito usipungua tani 50 na kubeba abiria zaidi ya 200 kikiwa na uwezo zaidi ya mara mbili ya Mv Nyerere ambacho kitapelekwa matengenezoni baada ya kuopolewa.
Aidha, Majaliwa amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kuhakikisha zabuni hiyo inafanywa haraka ikiwezekana hata kesho ili kivuko hicho kijengwe ndani ya miezi miwili au mitatu na kuanza kutumika na wakazi wa visiwa hivyo vya Ukerewe na Ukara.