October 6, 2024

Mv Nyerere yaondoka na bodi mbili ndani ya saa 24

Ni bodi ya Wakurugenzi Sumatra na Bodi ya Washauri TEMESA.

  • Ni bodi ya Wakurugenzi Sumatra na Bodi ya Washauri TEMESA.
  • Pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dk Mussa Mgwatu asimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa ajali ya Mv Nyerere.
  • Mpaka sasa waliofariki katika ajali hiyo wafikia 227 na waliokolewa wakiwa hai ni 41.

Dar es Salaam. Rais Dkt. John Magufuli amevunja bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (SUMATRA) ikiwa ni zimepita saa chache  baada ya kuivunja bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Septemba 23, 2018 kama hatua za uwajibikaji kufuatia kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere katika Ziwa Victoria.

Kivuko hicho kilizama Septemba 20 mwaka huu wakati kikitoka Kisiwa cha Ukerewe kuelekea kisiwa cha Ukara ambapo watu 227 wamefariki na 41 waliokolewa wakiwa hai.  

Taarifa ya kuvunjwa kwa bodi ya Sumatra imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mapema leo, ambapo sababu kubwa ni muendelezo wa matukio ya ajali nchini yanayosababisha uharibifu wa mali, ulemavu pamoja na vifo vya watu. 

Pia, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Dk John Nduguru. 

Mhandisi Dk Nduguru alikuwa akifanya kazi kwa karibu na Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo yenye jukumu la kusimamia  na kudhibiti wa soko la usafirishaji wa nchikavu na majini pamoja na usalama na utunzaji wa mazingira. 

Bodi hiyo ilianzishwa nchini kwa Sheria ya Bunge Na. 9 ya mwaka 2001 na kuanza kazi April 20. 2004 kwa Tangazo la Serikali Na. 297/2004, ambapo jukumu lake lingine ni kuratibu na kuwezesha utatuzi wa malalamiko na migongano katika soko la usafirishaji nchini.

Mnamo Februari 14, 2015 Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Samuel Sitta, alizindua Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA ambayo ni ya pili tangu kuanzishwa Mamlaka ya Sumatra. 

Wajumbe walioteuliwa walikuwa ni Prof. Iddi Mkilaha (Mwenyekiti), Injinia Alfred Nalitolela (Mjumbe), Dk Issack Legonda (Mjumbe), Injinia Khalid Kachenje (Mjumbe), Maregesi Manyama (Mjumbe) na Hilda Gondwe. 

Mwingine ni Mkurugenzi Mkuu, Gilliard Ngewe (Mjumbe) kutokana na nafasi yake kama Mtendaji Mkuu wa Mamlaka.

Lakini June 24,  2016, Prof Mkilaha alifariki dunia na nafasi yake ikachukuliwa na Mhandisi Dk Ndunguru ambaye amedumu mpaka uteuzi wake ulipotenguliwa leo na Rais.

Kuvunjwa kwa bodi ya Wakurugenzi Sumatra ni muendelezo wa hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwawajibisha watendaji wa Serikali kufuatia ajali ya kivuko cha Mv Nyerere ambapo jana Rais alivunja bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Bodi hiyo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri ambayo iliundwa mwaka 1997 ikiwa na jukumu la kuhakiki usalama na kuwapanga raia na vyombo vya usafiri wawapo kwenye vivuko na kuwasilisha matatizo yoyote yanayohusu vyombo vya usafiri majini.  

Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mapema leo asubuhi amemsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Dk Mussa Mgwatu ili kupisha uchunguzi wa ajali ya Mv Nyerere .

Imeandikwa na Rodgers George.