Mbegu za GMO ni mkombozi au janga kwa wakulima?
Wasomi wataka mjadala wa kitaifa na tathmini ya mbegu hizo ifanyike kabla ya kugawa kwa wakulima.
- Wasomi wataka mjadala wa kitaifa na tathmini ya mbegu hizo ifanyike kabla ya kugawa kwa wakulima.
- Zinadaiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza mavuno kwa wakulima.
Dar es Salaam. Wakulima nchini Kenya wataanza kutumia teknolojia ya uhandisi jeni ambayo hutengeneza mbegu za pamba maarufu kama GMO ili kuongeza uzalishaji na soko la zao hilo la biashara.
Ikiwa Kenya itafanikiwa kuzalisha na kutumia mbegu za GMO (Genetically Modified Organism) itakuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na ya tatu barani Afrika baada ya Afrika Kusini na Sudan kutumia mbegu hizo ambazo zimekuwa zikidaiwa kuathiri afya za watu na mazingira.
Ufunguzi wa matumizi ya mbegu za pamba za GMO, unatarajiwa kufanyika Januari 2019 na wakulima watapanda mbegu hizo Machi mwaka huo huo.
Taarifa kutoka Shirika la Kilimo na Mifugo la Kenya (KALRO) zinasema tayari watafiti wamepanda mbegu za pamba za GMO kwenye baadhi ya mashamba kwa ajili ya majaribio ya mazingira katika mji wa Kibos, Kisumu Magharibi mwa nchi hiyo.
“Tunatarajia katika miezi saba ijayo tutakuwa na data za kutosha kutoka kwenye vitalu vya majaribio kwaajili ya kugawa kwa taasisi za serikali,” amesema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo cha bustani nchini Kenya, Dk Charles Waturu.
Majaribio hayo ya kitaifa ya mbegu za GMO yatafanyika katika vituo vingine vitano vya Mwea, Bura Tana, Katumani, Kampi ya Mawe na Perkerra na vinatarajia kutumia Dola za Marekani 75,000 (Tsh 171 milioni) kwa miaka miwili.
Katika nchi za Afrika Mashariki ni Uganda, Tanzania na Kenya pekee ndiyo zinafanya majaribio ya mbegu za GMO.
Tayari Tanzania imezifanyia mapitio ya sheria zake ili kuruhusu majaribio ya mbegu hizo kwenye Kituo cha utafiti wa kilimo cha Makutupora kilichopo Dodoma kabla ya kuwapelekea wakulima.
Kulingana na sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 69 (1) – (3) kimeweka kanuni ambazo zinazozuia uingizaji wa vifaa vya kutengeneza mbegu hizo kwa ajili ya utafiti ambapo mtu yeyote atakayeingiza mbegu za GMO atawajibika kwa madhara yatakayotokea kwa afya za watu na mazingira.
Mbegu za GMO zinaaminika kwa uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kupungua kwa mvua. Pia zinazaliana sana kuliko mbegu za asili na zinaweza kuongeza uzalishaji na soko kwa wakulima.
Zinazohusina:
- Ripoti: Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika.
- Wakulima wanavyopigani bei nzuri ya mazao Afrika Mashariki.
Tanzania bado inatafakari ujio wa mbegu za GM0
Baadhi ya wataalamu wa mazingira na afya ya binadamu wamezikataa mbegu hizo na kudai kuwa zinaathiri afya ya binadamu, ukuaji wa akili ya watoto na ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.
Akiwasilisha mada katika mkutano wa Kavazi la kwanza la Mwalimu Nyerere (2018) kuhusu utafiti wa awali wa GMO, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaamu, Dk. Richard Mbunda amesema bado kuna taarifa ambazo zinapishana katika kiwango ambacho mbegu za GMO zinazostahimili ukame na uwezo wake wa kupunguza hasara kwa mkulima.
Dk. Mbunda amesema mashaka wanayoyaona baadhi ya watu ni kuhusu usalama wa vyakula vinavyotokana na mbegu za GMO kwa afya na mazingira, mambo ambayo ni lazima watafiti wayaangalie na kujiridhisha kabla ya kuzipeleka mbegu hizo kwenye mamlaka za serikali zinazopitisha mbegu zote nchini.
Wasiwasi mwingine ni namna mkulima mdogo atakavyoweza kunufaika na teknolojia hiyo ikiwemo upatikanaji wa mbegu hizo kwa bei nafuu.
Hata hivyo, aliiyewahi kuwa Mtafiti wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ((COSTECH), Dkt. Nicholous Nyange amesema ni wakati mwafaka kwa wakulima wa Tanzania kutumia mbegu za GMO ili kuongeza uzalishaji na kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
“Inakadiriwa kuwa Tanzania kwa sasa ina watu wapatao milioni 55 na idadi hii inaongezeka kila siku na kama sayansi haitatumika kusaidia kuzalisha chakula cha kutosha basi huenda taifa likasumbuliwa na njaa kila mwaka kwenye maeneo mengi”, amesema Dkt. Nyange.
Amebainisha kuwa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na wakulima kulima lakini bado hawajaweza kuzalisha chakula cha kutosha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wadudu, magonjwa na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mazao ya mbegu za GMO hasa pamba yanatajwa kuchochea ujenzi wa viwanda vingi vya nguo Afrika. Picha|IPPMedia
Ripoti ya Utafiti ya Hali ya Biashara na Kukubaliwa kwa Mazao ya Kibayoteki ya mwaka 2017 inaeleza kuwa mpaka sasa nchi 24 duniani zinalima mazao ya kibayoteki, huku nchi mbalimbali zikiendelea na utafiti wa mbegu hizo kabla hazijapelekwa kwa wakulima. Nchi 19 zinafanya biashara na kutumia bidhaa za mazao hayo.
Kwa upande wake, Mtafiti wa zao la mahindi, Dk. Aloyce Kulaya ametoa angalizo kuwa teknolojia ya uhandisi jeni sio njia pekee ya kupata ufumbuzi wa matatizo ya wakulima lakini pale mbinu za kawaida zinaposhindwa, teknolojia hiyo hutumika kupata ufumbuzi wa haraka na sahihi wa changamoto za magonjwa,ukame na wadudu ambazo zinawasumbua wakulima.
Mazao ambayo yanazalishwa kwa wingi kupitia teknolojia ya GMO ni pamoja na mahindi, pamba, maharage ya soya na viazi ambavyo hutegemewa na nchi za Afrika kama sehemu ya kuboresha usalama wa chakula na kuingiza kipato.
Naye Mtaalamu wa kujitegemea wa Mazingira na Uvuvi, Dkt. Modesta Medard amesema mijadala wa teknolojia ya uhandisi jeni haina umuhimu kwa taifa kwasababu sio rafiki kwa mazingira na viumbe hai ambapo ameishauri Serikali kujikita katika kuwatafutia wakulima teknolojia rahisi ya kuongeza mazao.
Majaribio ya mbegu za GMO yaliingia Tanzania mwaka 2008 chini ya mradi wa Water efficient Maize for Africa (WEMA) uliofadhiliwa na taasisi ya Bill&Merinda Gates ya nchini Marekani lakini yalianza kufanyika mwaka 2016 katika kituo cha utafiti wa kilimo cha Makutupora lakini bado serikali haijaridhia matumizi ya mbegu hizo kwa wakulima.