November 24, 2024

Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni

Yawapa siku 50 kufanya hivyo la sivyo mkono wa sheria utachukua nafasi yake

  • Iwapo wanaokodisha nyumba watalii bila leseni watakamatwa na kukutwa na hatia, watakumbana na adhabu ya faini isiyopungua Sh10 milioni au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
  • Yawapa siku 50 kufanya hivyo la sivyo mkono wa sheria utachukua nafasi yake.

Dar es  Salaam.  Wafanyabiashara wanaopangisha nyumba zao kwa muda mfupi kwa wageni nchini (Homes stay) sasa watalazimika kuja na namna nyingine ya kufanya biashara hapa nchini baada ya Serikali kuwapa siku 50 kusajili kabla ya kuwachukuliwa hatua za kisheria. 

Mkurugenzi wa Utalii Deograsias Mdamu ameeleza katika taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 10, 2018 kuwa ni kinyume na sheria kwa watoa huduma hao kuendelea kupokea watalii bila kupata leseni.

“Watu binafsi na makampuni yanayojihusisha na kutoa huduma kwa watalii majumbani kinyume na sheria wanatakiwa kujisajili kabla ya atarehe 30 Oktoba ,2018,’’ inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Uamuzi wa notisi hiyo ya Serikali imetokana na matakwa ya vifungwa namba 10, 21 na 31 (1-6 ) vya Sheria ya Utalii ya mwaka 2008 vinavyomtaka mtu au kampuni yenye nia ya kufanya utalli katika majengo kujisajili kwa Mkurugezi wa Utalii iliapatiwe leseni ya utalii (Tanzania Tourism Business License).

Ili kupata leseni hiyo, mzawa anayeendesha biashara hiyo atatakiwa kutoa Dola za Marekani 400 (Sh930,000) kwa mwaka wakati wageni wanaofanya biashara ya kukodisha nyumba hizo kwa muda mfupi kwa watalii watatakiwa kulipia Dola za Marekani 600 () kwa kipindi hicho.

Miongoni mwa watakaothirika na hatua hiyo ya Serikali ni wale wanaotumia mitandao kukodisha nyumba hizo kama mtandao maarufu wa Marekani wa Airbnb ambao unaoeleza kuwa katika mwaka unoishia Septemba 2017 ulikuwa na maorodhesho ya kukodisha nyumba 24,000. 

Muonekano wa nyumba ni kivutio kwa watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali nchini. Picha| Living+Nomads

Ripoti ya mtandao huo inayoangazia soko la Afrika iitwayo ‘Overview Airbnb Community in Africa’ inaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya tano Afrika kwa kuwa na wageni wengi wanaoingia kupitia Airbnb huku wapangishaji wa nyumba hizo nchini wakiingiza Dola za Marekani milioni 2.1 sawa na Sh4.8 bilioni.

Iwapo wanaoendesha biashara hiyo bila leseni watakamatwa na kukutwa na hatia, watakumbana na adhabu ya faini isiyopungua Sh10 milioni au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja, kwa mujibu wa Kanuni za Utalii za Hifadhi na Makazi ya mwaka 2015 (The Tourism (Accommodation facility) Regulations 2015.

Baadhi ya wadau wameeleza kuwa hatua hiyo italeta usawa katika biashara kwa kufanya wadau wote wajisajili na kulipa kodi inayotakiwa kwa Serikali.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato) Sirili Akko ameeleza kuwa licha kuwa hawana wanachama wanaofanya biashara hiyo ya kupangisha nyumba hizo kwa muda bila kujisajili, hatua hiyo itasaidia kuleta usawa katika tasnia ikizingatiwa kuwa baadhi ya watalii kwa sasa wanapenda kuishi maisha nje ya hoteli. 

Nyongeza na Nuzulack Dausen