Wahandisi wapya 430 waingia rasmi sokoni
Waaswa kufuata maadili ya taaluma ya kazi zao ili waweze kuaminika zaidi na jamii na wateja wao.
- Wataalamu hao wapya wanaongeza idadi ya wahandisi nchini hadi kufikia 2,876 huku 184 kati yao wakiwa ni wahandisi washauri.
- Waaswa kufuata maadili ya taaluma ya kazi zao ili waweze kuaminika zaidi na jamii na wateja wao.
Dar es Salaam. Wahandisi 430 wameingia rasmi sokoni nchini baada ya kuapishwa jana (Septemba 7, 2018) ikiwa ni tiketi yao maalum ya kuanza kufanya shughuli za kiuhandisi.
Idadi hiyo ya wahandisi wapya walioapishwa katika hafla ya kufunga maadhimisho ya miaka 50 ya kuundwa kwa ERB, inafanya jumla ya wataalamu hao sasa kufikia 2,876 waliohitimu na kula viapo vya kufanya shughuli hizo kwa weledi. Kati ya wahandisi wote waliopo nchini, wahandisi wataalamu (professional engineers) ni 2,716 na wahandisi washauri (consulting engineers) ni 184.
Kiutaratibu, wahandisi hao hutakiwa kula viapo na kupatiwa leseni kabla ya kuanza kazi zao ikiwa ni kutimiza matakwa ya Sheria ya Viapo namba 34 ya mwaka 2002. Madhumuni ya kula kiapo hicho ni kwamba mwandisi atakua mwaminifu na atazingatia sheria zote za uhandisi katika utekelezaji wa taaluma hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amewashauri wahandisi hao kuzingatia yale wanayotakiwa kuyafanya ili kuhakikisha wanaendana na taratibu na misingi ya taaluma hiyo.
“Ndugu wahandisi niwapongeze kwa hatua mliofikia, lakini kwa ueledi na uaminifu mkubwa tunategemea mtatekeleza sheria na taratibu zote zilizopo katika sheria zenu ili wananchi wawaamini katika kazi zenu zote mnazozifanya,”. amesema Kwandikwa.
Wahandisi wapya 430 wakisubiri kula viapo kabla ya kukabidhia leseni zao za uhandisi ili kuingia sokoni Septemba 7, 2018. Picha|Tulinagwe Malopa.
Mwenyekiti wa ERB, Prof Ninatubu Lema amewasihi wahandisi kuhakikisha hatua ya kuapishwa ni kianzio cha hatua ya kwanza ya kuhakikisha wanatekeleza yale wanayotakiwa kuyafanya kama watu muhimu katika nchi hii.
“Tunategemea kwa kuapishwa kwenu iwe dalili ya watanzania kuona mambo makubwa kutoka kwenu kuzingatia maadili yote ya taaluma yenu kama inavyotakiwa,” amesema Prof Lema.
Wahandisi ni moja ya nguvukazi muhimu katika ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini kutokana na mchango wao katika usanifu, ujenzi na usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote binafsi na umma.