Shule za Kinondoni zinavyokimbiza Dar es salaam
Shule sita kati ya 15 vinara ndani ya mkoa wa Dar es salaam zimeunda orodha ya dhahabu kwa kuwa hazijawai kutoka 10 bora kwa miaka yote mitatu
- Hakuna hata shule moja ya Serikali iliyoingia 10 bora ndani ya miaka mitatu iliyopita.
- Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuingiza shule nyingi katika orodha ya kumi bora.
- Shule ya Sekondari ya Stanley ndiyo sekondari pekee kutoka wilaya ya Temeke iliyofanikiwa kuingia 10 bora ndani ya miaka mitatu.
Dar es Salaam. Matokeo ya kidato cha nne yanapotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) mara nyingi shule zinazojulikana zaidi ni shule kumi bora au zile kumi za mwisho kitaifa.
Lakini ni mara chache unaweza kusikia matokeo ya shule katika ngazi ya mkoa yanayo onyesha shule zilizofanya vizuri ama vibaya zaidi. Hiyo inatokana na ukweli kwamba taarifa za aina hiyo hazitolewi mara kwa mara na wanahabari zaidi ya mzazi mwenyewe kufanya jitihada zake binafsi.
Nukta inakuletea shule 10 bora zilizotamba ndani ya Mkoa wa Dar es salaam wenye wilaya na halmashauri tano katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa na NECTA kuanzia mwaka 2015 hadi 2017.
Baadhi ya shule hizo hazijafanikiwa kuingia 10 bora ya kitaifa lakini ngazi ya wilaya na mkoa zinafanya vizuri na wakati mwingine zimekuwa zikipanda katika ufaulu.
Katika kipindi hicho cha miaka mitatu ni shule 15 tu ndio zimefanikiwa kuingia katika orodha ya shule 10 bora huku Manispaa ya Kinondoni ikiongoza kwa kuingiza wastani wa shule nane katika kinyang’anyiro hicho. Kinondoni ni halmashauri iliyofanya vyema kuliko nyingine Dar es Salaam.
Zinazohusiana:
- Shule 24 vigogo ‘zilizoteka” 10 bora ya kidato cha nne
- Safari ya kurudi kileleni: Lini Iyunga tech itarudi kwenye 10 bora kitaifa?
Mathalani mwaka 2015 katika shule 10 vinara shule nane zilitoka katika wilaya ya Kinondoni na shule mbili zilizobaki ambazo ni shule ya Sekondari ya Tusiime kutoka Manispaa ya Ilala na Shule ya Sekondari ya Stanley kutoka katika Manispaa ya Temeke.
Hata mwaka uliofuata wa 2016 Kinondoni iliendelea kutamba ambapo safari hii iliingiza shule tisa kati ya 10 huku Ilala Islamic Secondary ikiwa shule pekee kutoka Ilala.
Mwaka jana, Kinondoni ilifanikiwa kuingiza shule nane ukilinganisha na tisa zilizoingia mwaka uliotangulia. Katika mwaka huo Halmashauri mpya ya Ubungo nayo ilibahatika kuingiza shule moja ya St. Augustine Tagaste na huku Temeke ikiendelea kuwakilishwa na Stanley.
Shule sita kati ya 15 vinara ndani ya mkoa wa Dar es salaam zimeunda orodha ya dhahabu kwa kuwa hazijawahi kutoka 10 bora kwa miaka yote mitatu. Shule hizo ni Feza Boys, Feza Girls, Cannosa Girls, Barbro-Johansson, Alpha na Mtakatifu Josefu Millennium zote kutoka wilaya ya Kinondoni. Shule hizo zinamilikiwa na watu binafsi na mashirika ya dini.
Wahitaji kujua mchanganuo wa matokeo ya kidato cha nne kuanzia wilaya, mkoa na Taifa? Tafuta majibu kwenye Elimu yangu
Stanley ni sekondari pekee kutokaTemeke ambayo imefanikiwa kuingia kumi bora mara mbili ikiungana na Mivumoni na Shamsiye Boys za Kinondoni. Shule sita zilizobaki za Loyola, Tusiime, Ilala Islamic Seminary, St. Augustine Tagaste, Hellen’s na Thomas More Machrina zimefanikiwa kuingia mara moja tu katika miaka yote mitatu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Dk Charles Msonde.Picha kwa hisani ya mtandao
Licha ya shule hizo 15 kutamba katika 10 bora ya mkoa wa Dar es Salaam, bado zinafanya vizuri katika matokeo ya kitaifa. Mfano mwaka 2017 shule za nne za Feza Boys, Feza Girls, Canossa Girls na Shamsiye zifanikiwa kuingia 10 bora na kushika nafasi mbali mbali.