Zanzibar kitovu utengenezaji meli za uvuvi Afrika Mashariki
Meli zitachochea biashara ya samaki na kukuza pato la wananchi.
- Meli za kisasa kuongeza wigo wa biashara EAC.
- Pia zitapambana na uvumi haramu na uharibifu wa mazingira.
- SMZ kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji.
Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) huenda ikaanza kufaidika na mazao ya baharini kutokana na ujio wa meli za kisasa za uvuvi zitakazofanya kazi katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC).
Kisiwa cha Zanzibar kinategemea zaidi bahari ya Hindi lakini kwa muda mrefu sasa wananchi wake hawajafaidika na rasilimali zilizopo baharini kwasababu ya matumizi ya teknolojia duni ya uvuvi na uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Kwa mujibu wa ripoti ya rasilimali za bahari iliyotolewa na Chuo Cha Utafiti wa Samaki cha Wagengen kwa ushirikiano wa Wizara ya Uchumi ya Ujerumani mwaka 2017 inaeleza kuwa sekta ya uvuvi ya Zanzibar kwa sehemu kubwa inaendeshwa na wavuvi wadogo ambao wanatumia dhana za asili. Wanazalisha tani kati ya 14,000 na 20,000 kwa mwaka na samakI hao hutumika zaidi kukidhi mahitaji ya familia.
Lakini huenda hali hiyo ikabadilika siku zijazo kutokana na kampuni ya uwekezaji ya Privinvest and Advanced Marine Transport (AMT) ya nchini Dubai kuonyesha nia ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha utengenezaji wa meli za kisasa ambazo zitatumiwa na wavuvi katika eneo la bahari kuu.
Wachambuzi wa masuala ya biashara wanasema ujio wa kampuni hiyo utafungua milango ya ujenzi wa viwanda vya samaki na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo itasaidia kupunguza uvuvi halamu unaofanywa na maharamia wanaotumia meli zilizosajiliwa Zanzibar.
Mwenyekiti wa kampuni hizo, Jean Boustany anasema meli zitakazotengenezwa zitatumia teknolojia ya kisasa itakayosaidia kupambana na uvuvi halamu ili kuwawezesha wananchi wa kisiwa hicho kufaidika na rasilimali za bahari na kukuza uchumi wa taifa.
Pia itachochea utendaji na ufanisi wa bandari ya Zanzibar kwa kuongeza idadi ya meli na mizigo inayoingia na kutoka, mapato yatakayopatikana yatakayotumika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu.
Kampuni hiyo ambayo inajihusisha na utengenezaji wa meli, usafiri wa majini na usafirishaji wa mizigo inaendesha shughuli zake pia katika nchi za Afrika Kusini, Angola, Cameroon, Congo, Equatorial Guinea, Ghana, Nigeria, Madagascar and Msumbiji.
Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein anasema serikali yake inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa kitovu cha biashara ya samaki. “Tutatengeneza mazingira wezeshi kwa kampuni za ndani na kimataifa kutekeleza matakwa yao ya uwekezaji.”
Katika kuhakikisha inadhibiti biashara haramu ya rasilimali za bahari, SMZ imefunga ofisi zake za usajili wa meli zilizopo nchini Dubai. Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi sita tangu Tanzania isitishe usajili wa meli za kimataifa zinazopeperusha ya bendera ya nchi hiyo kutokana na kujihusisha na uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha.
Zanzibar imekuwa ikishutumiwa kwa kuziruhusu meli za Irani na Korea Kaskazini kupeperusha bendera ya Tanzania na kukwepa vikazwa vya Umoja wa Mataifa vya usafirishaji wa silaha za nyuklia zinazopelekwa Libya na nchi zingine za Afrika zenye machafuko ya kisiasa.
Moja ya meli ikiendelea na shughuli ya uvuvi wa samaki katika bahari kuu ya Hindi. Picha|Ocean71.
Ukosefu wa data na teknolojia
Utafiiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Overseas Development ya nchini Uingereza unaeleza tatizo la uvuvi haramu kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi unachochewa zaidi na ukosefu wa miundombinu ya mawasiliano, ushirikiano na teknolojia ya kutunza takwimu za meli za uvuvi.
Utafiti huo unaeleza kuwa ili kufuatilia eneo na safari, meli zinapaswa kuwa na kifaa cha mawasiliano kinachojulikana kama ‘Vessel Management Systems (VMS)’. Hata hivyo meli nyingi hazina kifaa hiki hasa katika nchi zinazoendelea ambako teknolojia hiyo haipatikani au wasimamizi wa meli huzima ili kuepuka kufuatiliwa na mamlaka husika.
Licha ya kifaa cha VMS kuwa na uwezo wa kutambua eneo, umbali na mwelekeo wa meli lakini hakiwezi kutambua meli zinazoharibu mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini.
Pia ukosefu wa takwimu za pamoja za dunia za meli za uvuvi ni changamoto nyingine. Vyombo vya baharini hubadilisha mara kwa mara bendera, umiliki na uendeshaji huku takwimu za umiliki zikiwa mikononi mwa mashirika ya kimataifa, mataifa yanayotoa usajili wa meli na bodi za leseni za uvuvi.
Kulingana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) linaeleza kuwa kuna meli 75,000 hadi 779,000 kati ya milioni 4.6 zinazojihusisha na uvuvi haramu duniani kote.