November 24, 2024

Mambo yatakayokusaidia kuboresha ubunifu kazini

Fikiria zaidi ya ulipo upate kufika utakapo. Hakuna njia ya mkato kwenye dunia inayohitaji ubunifu ili kuendelea kuwepo.

  • Ubunifu ni msingi wa kupata wateja na kuvutia watu wengi
  • Fikiria zaidi ya ulipo upate kufika utakapo
  • Kuwa mjanja na kubali kubadilika pale unapoona uendako hakuna mwelekeo

“Kinachokuja kirahisi hakiwezi kudumu na kinachodumu hakiji kirahisi” ni msemo maarufu kutoka kwa mfanyabiashra wa Tanzania, Mohammed Dewji.

Katika hali ya kawaida, jambo lolote zuri au mafanikio hayapatikani kirahisi. Ubunifu unahitajika katika kila jambo unalolifanya ili utimize malengo yako.

Ubunifu unaweza kutafsiriwa kuwa ni kitu fulani halisia na chenye mchango wa wazi kinachoweza kuleta matokeo chanya katika jamii. Pia ubunifu huchukuliwa kama matumizi ya njia bora zaidi zinazoweza kutatua changamoto mpya, changamoto ambazo tayari zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi kwenye soko au jamii kwa kipindi husika.

Dhana hii hutimilika pale ambapo bidhaa, huduma, teknolojia, mpangilio wa biashara au njia nyingine yoyote inayoweza kutatua changamoto husika katika jamii ni adimu kuipata katika mazingira ya kawaida. 

Ubunifu ni kutafuta njia rahisi kukamilisha malengo yako. Picha| Mtandao

Leo tuzungumzie ubunifu katika eneo la kazi iwe umeajiriwa au umejiajiri na jinsi gani mawazo ya kibunifu yanavyoweza kukusaidia kutimiza malengo yako na kukufanya uwe bora zaidi. Japo kuna mengi yanaweza kukufanya ufanikiwe kuna mambo muhimu ya kuzingatia:

Jifunze kufanya vitu tofauti

Usifanye kitu ambacho kila mtu anafanya. Tafuta namna ya kuongeza thamani ya kazi yako ili uwe bora zaidi. Kujitofautisha na wengine ni kutafuta njia sahihi za kukamilisha kazi yako kwa wakati na kufikia malengo yaliyokusudiwa.  

Kwanini kampuni ya Apple hawafanyi vitu sawa na Samsung? Kwa sababu utofauti wao ndiyo ngazi ya mafanikio. Upekee ndiyo mtaji wako katika ubunifu. 

Vilevile hapa unaweza kuiga mifano ya watu waliojaribu kufanya vitu tofauti na kufuatilia mwenendo wao wamefikia wapi. Hata hapa Tanzania, huwezi kuongelea watu waliofanikia katika tasnia ya muziki bila kumtaja Msanii maarufu  Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) ambaye kupitia sauti, maudhui na mpangilio wa ala za muziki wake utagundua kuna utofauti mkubwa na wasanii wengine nchini. 

Kubali mabadiliko

Usiwe mtu wa kung’ang’ania kitu kimoja kwa muda mrefu jaribu njia tofauti, acha mazoea. Upo msemo unaosema usitegemee matokeo tofauti katika kitu unachofanya kwa njia zile zile. 

Utamkuta mtu ana biashara ya kuuza magauni lakini hafikirii hata mara moja kuongeza viatu au kuboresha ofisi iwe na vioo vya kisasa pamoja na vitu vingine ambavyo mwanamke anapenda akiwa anajaribu nguo. 

Ubunifu ni pamoja na kuwa na jicho la udadisi kuangalia wengine wanafanya nini katika kazi zao. Udadisi utakupa mwanga na mwelekeo sahihi wa kuboresha kazi yako kulingana na nyakati na soko lilivyo. Hivyo ubunifu ni mtaji kwa kila mpenda maendeleo.

Tumia vizuri rasilimali zinazokuzunguka

Tumia kikamilifu uwezo ulionao, usikimbilie kuanza kitu kikubwa ambacho huwezi kukiendesha au hauna uwezo wa kukifanya. Gundua vitu vidogo vinavyobadilika na vyenye uwezo wa kuingia sokoni, chagua kimoja ambacho watu wengi hawafanyi badala ya kuchagua kilichopo tayari.

Hapa ndipo vijana wengi katika nyanja mbalimbali tunaweza kubuni vitu na kutumia teknolojia iliyopo kwa kujitangaza katika mitandao ya kijamii na kuwasaidia watu kuona fursa mbalimbali zilizopo katika maisha ya kila siku.

Imarisha mahusiano na wafanyakazi wenzako

Hakuna kazi inayoweza kukamilika bila kushirikisha watu. Kufahamu uwezo na umahiri wa watu wanaokuzunguka ni njia sahihi ya kukamilisha malengo uliyojiwekea. 

Kufahamu uwezo wao itakusaidia kufahamu changamoto walizonazo na jinsi ya kuzikabili na kuhakikisha huduma inayotolewa inakuwa bora na  yenye maslahi kwa jamii.  

Watu wanaokuzunguka wana nafasi kubwa kuharibu au kufanikisha kazi yako. Picha| MEST

Jifunze kuangalia mapungufu yako

Tathmini uwezo na mapungufu uliyonayo katika kutekeleza malengo yako. Itakusaidia kujirekebisha na kutafuta njia iliyo bora zaidi ya kufanya kazi au kumtafuta mtu mwingine ambaye anaweza kumudu eneo ambalo wewe huna ujuzi nalo.  

Hata hivyo, ubunifu ni dhana mtambuka lakini ukizingatia mambo yaliyotajwa hapo juu unaweza kupiga hatua kuelekea katika mafanikio unayoyataka. 

Ni muhimu kufahamu kuwa ubunifu pekee hauwezi kukufanikisha, lakini nidhamu ya kazi, uvumilivu, hekima na kusimamia kile unachokiamini ndio msingi mkuu wa ubunifu.