TCRA yakusudia kusimamisha leseni za Multichoice na Zuku
Multichoice Tanzania na Zuku zinaongeza idadi ya kampuni zilizopo katika hatihati ya kufutiwa leseni kuwa tatu baada ya TCRA kutangaza kusudio la kuifuta Star Times siku 12 zilizopita.
- Iwapo TCRA itaifutia Dstv leseni zake, itakuwa pigo kwa wapenzi wa soka hususan kipindi ambacho Ligi Kuu ya Uingereza inaanza.
- Multichoice Tanzania na Zuku zinaongeza idadi ya kampuni zilizopo katika hatihati ya kufutiwa leseni kuwa tatu baada ya TCRA kutangaza kusudio la kuifuta Star Times siku 12 zilizopita.
Dar es salaam. Sekta ya utangazaji huenda ikapata pigo siku zijazo baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutangaza kusudio la kufuta leseni za kampuni kubwa mbili za visimbuzi za Multichoice Tanzania na Simbanet Tanzania kutokana na kushindwa kufuata masharti ya leseni zao yanayowataka kutobeba na kurusha chaneli za runinga zinazotakiwa kuonyeshwa bure.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na TCRA leo (7 Agosti 2018) imeeleza kuwa Multichoice inayofahamika zaidi kama DStv na Simbanet Tanzania maarufu kama Zuku zimevunja sheria baada ya kuendelea kutoa huduma ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa leseni zao kubeba na kuonyesha chaneli za televisheni zenye leseni za kutazamwa bila malipo (Free-to-Air) kupitia visimbuzi vyao isipokuwa kwa runinga ya Taifa, TBC 1, pekee.
Katika taaarifa yake iliyochapishwa katika gazeti la kila siku la Daily News la leo (7 Agosti 2018), TCRA inasema kuwa kampuni hizo zimeendelea kukaidi amri ya mamlaka hiyo hata baada ya kuzuiwa kufanya hivyo.
Kusudio hilo la TCRA linakuja zikiwa ni siku 12 tu tangu itoe kusudio la kusimamisha leseni ya Star Media Tanzania (Star times) kwa kushindwa kuhakikisha chaneli za televisheni zenye leseni za kutazamwa bila kulipia zinaoneshwa kupitia ving’amuzi vyao bila ya watazamaji kufanya malipo yoyote.
TCRA inasema kuwa kwa nyakati tofauti iliwataka Multichoice na Zuku kutii masharti ya kuacha kubeba na kuonyesha chaneli hizo lakini uchunguzi uliofanywa na mamlaka hiyo unaonyesha kampuni hizo zinaendelea kukiuka masharti hayo.
“Hata baada ya TCRA kuiamuru kampuni ya Multichoice Tanzania Limited kuacha kubeba na kuonesha chaneli za televisheni zenye leseni ya kutazamwa bila malipo kupitia ving’amuzi (visimbuzi) vyao isipokuwa TBC 1 pekee, Multichoice imekaidi na bado inaendelea kubeba na kuonesha chaneli za televisheni zenye leseni za kutazamwa bila malipo,” inasomeka sehemu ya moja ya taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo pia imebainisha pia Zuku nao pamoja na leseni yao kukataza kubeba na kuonesha chaneli za kutazamwa bila malipo imeendelea kukaidi masharti hayo jamblo lililofanya ikusudie kuinyang’anya kampuni hiyo leseni zake zote.
Hatua hiyo ya TCRA ya kutaka kampuni hizo kutobeba chaneli zenye leseni ya kuoneshwa bure itapeleka maumivu kwa wateja wa DStv na Zuku waliokuwa wakizipata chaneli hizo za kitaifa katika visimbuzi hivyo. Wateja hao sasa watabakiwa na chaneli moja ya TBC1 iwapo kampuni hizo zitaziondoa chaneli hizo katika visimbuzi hivyo kama inavyotakiwa na masharti ya leseni zao.
Pia endapo DStv itafutiwa leseni itakuwa ni pigo kwa wapenzi watazamaji wa DStv hususan wapenda soka wa Ligi Kuu ya Uingereza inayotarajia kuanza Agosti 10 kwa mechi kati ya Man Utd na Leicester.
Hayo yanajiri wakati idadi ya Watanzania wanaojiunga na visimbuzi vya kulipia ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Takwimu za TCRA za robo ya kwanza ya mwaka 2018 zinaonyesha kuwa hadi Disemba 2017 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa visimbuzi vya kulipia 2.23 milioni ikiwa ni zaidi ya mara tano ya watumiaji waliokuwepo mwaka 2012 ambao ni 422,384.