November 24, 2024

Namna wanafunzi wanavyoisaka huduma ya maktaba kama dhahabu Mbeya

Mkoa wa Mbeya unakabiriwa na uhaba mkubwa wa maktaba katika shule za msingi jambo linalorudisha nyuma jitihada za kuongeza maarifa kwa wanafunzi.

  • Shule za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Kyela zinahitaji maktaba 102 lakini hadi sasa hakuna hata moja.
  • Baadhi ya wadau wajitoa kujenga maktaba ili kuwapa fursa wanafunzi kuongeza maarifa kwa kujisomea vitabu.

Mbeya. Alafati Ramadhani, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mpanda kata ya Ipyana wilaya ya Kyela anatamani asome hadi afike chuo kikuu ili apate maarifa ya kusaidia jamii yake kuondokana na ujinga wa fikra.

Hata hivyo, huenda matamanio ya Alafati yasitimie kama anavyotaka kutokana na kukabiliwa na changamoto lukuki katika shule yake ikiwemo ukosefu wa maktaba ya vitabu.

Kwa kipindi kirefu Alafati anasoma tu kwenye vitabu kuwa shule kama yao inatakiwa kuwa na maktaba ya vitabu ambayo wanafunzi wanaingia na kusoma ili kupata maarifa.

Lakini Alafati (13) ambaye anasoma darasa la tano amebakiza miaka miwili kuhitimu elimu ya msingi hivyo itamlazimu kutumia njia mbadala ya kusoma vitabu ili kufikia ndoto yake ya kufika chuo kikuu kwa kuwa hakuna dalili  ya kukaa siku moja ndani ya maktaba ya shule yao siku za hivi karibuni.

“Hatuna chumba cha maktaba hapa shuleni, mwalimu analeta vitabu darasani tukitumia anavirudisha ofisini kwake,” anasema Alafati.

Lengo kuu la kuwepo kwa maktaba shuleni ni kutoa fursa kwa wanafunzi kupanua akili na kujipatia elimu, maarifa na taarifa mbalimbali zitakazowasaidia katika kujikwamua kutoka katika umaskini na ujinga. Pia usomaji vitabu hutoa burudani na kudumisha utamaduni wa kujisomea.

Alafati ni miongoni mwa wanafunzi wengi wa shule za msingi nchini ambao hawapati haki ya kusoma vitabu katika mazingira tulivu kutokana na shule zao kukosa majengo ya maktaba.

Kabati linalotumika kama mbadala wa maktaba katika Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Kyela mkoani Mbeya. Picha| Daniel Samson.

Uchunguzi uliofanywa na Nukta katika shule za msingi za Wilaya ya Kyela umebaini kuwa kwa miaka mitano mfufululizo tangu mwaka 2013 hadi 2017, wilaya hiyo haikuwa na maktaba hata moja katika shule za msingi, jambo linalokwamisha muamko wa wanafunzi kupenda kusoma vitabu na kupata maarifa mapya.

Hadi kufikia mwaka 2017, wilaya hiyo ilikuwa wanafunzi 55,821 wa shule za msingi lakini wanafunzi wa shule za umma hawana fursa ya kujisomea katika maktaba tofauti na wenzao wa shule binafsi.

Pamoja na kuwepo jitihada mbalimbali za Halmashauri kuboresha miundombinu ya madarasa na vyoo bado ujenzi wa majengo ya maktaba umesahaulika.

Takwimu za Ofisi ya Afisa Elimu Takwimu wilaya Kyela zilizotolewa kwa Nukta katikati ya Mei 2018 zinaonyesha kwa miaka hiyo mitano, shule za msingi wilayani humo zilikuwa na mahitaji ya maktaba 102 lakini ndani ya kipindi hicho hakuna maktaba yoyote iliyojengwa.

Hata hivyo, takwimu za elimu za msingi Tanzania (BEST) za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa wilaya hiyo ilikuwa na mahitaji ya maktaba 108 mwaka huo lakini zilizokuwepo ni saba pekee.

Kwa bahati mbaya Afisa Elimu Shule za Msingi wa wilaya hiyo, Palemon Ndarugiliye ameimbia Nukta kuwa hata maktaba hizo saba zilizotajwa na takwimu za Best hazipo.

Kuna wasiwasi kuwa takwimu hizo huenda zilijumuisha vituo vya kusomea ambavyo vilikuwa kwenye baadhi ya kata na sasa havifanyi kazi kabisa.

“Kusema ukweli hatuna maktaba hata moja kwa sasa. Tulikuwa na vituo vitano vya kusomea navyo vimekufa. Havifanyi kazi,” anasema Ndarugiliye.

Kuna kila dalili kuwa hali hiyo huenda isibadilike kutokana na vipaumbele vinavyopangwa katika halmashari hiyo kuelekezwa katika ujenzi wa madarasa na vyoo ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi linachochewa na sera ya elimu bila malipo.

“Tuna mipango ambayo tunatekeleza. Kipaumbele chetu ni kujenga madarasa na vyoo labda tukikamilisha tutajenga maktaba,” amesema Mratibu wa Elimu kata ya Kyela, Hezron Mwaikinda.

Hali hiyo haitofautiani na ya Manispaa ya Jiji la Mbeya iliyo kwenye mkoa mmoja na Kyela ambayo nayo inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na maktaba hata moja katika shule za msingi za umma.

Katika shule za msingi kama Inyala, Iyela, Iyunga na Jitegemee ambazo Nukta ilitembelea hivi karibuni wanafunzi na walimu wanapenda kuwa na maktaba lakini “hawajabarikiwa” kuwa nazo.

“Hakuna hata maktaba moja hata vitabu tunahifadhi katika makabati hapa ofisini. Hii ni changamoto kwa kweli,” anasema Mwalimu Generosa Samira kutoka Shule ya Msingi Inyala.

Kutokuwepo kwa maktaba katika shule za msingi katika mkoa huo, huenda ni miongoni mwa sababu zilizofanya mkoa huo kutofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba ukilinganisha na mikoa mingine ya Tanzania bara.

Mathalani katika matokeo ya mwaka jana, Mbeya ilishika nafasi ya 17 kati ya mikoa 26 ikipitwa na mikoa ya Lindi, Rukwa, Katavi, Tabora na Geita ambayo inakabiliwa na changamoto lukuki za elimu. Hali hiyo ilikuwa nafuu kidogo ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2016 ambapo ilishika nafasi ya 22 juu kidogo ya mikoa ya Songwe, Mtwara, Dodoma na Morogoro.

Ifahamike bayana kuwa uwepo wa mahitaji muhimu ya elimu kama uwepo wa walimu wazuri na wenye ari, madarasa safi, madawati ya kutosha, vitabu na chakula shuleni husaidia wanafunzi kufanya vyema katika masomo yao.

Nini kinafanyika kukabiliana na hali hiyo?

Ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma vitabu na kupata maarifa wakati wakisubiri maktaba ambazo haijulikani zitajengwa lini, walimu katika shule hizo wameweka utaratibu maalum ambao wanafunzi hupewa vitabu na kwenda navyo nyumbani kwa kupokezana.

“Hatuna maktaba, vitabu tunatunza kwenye maboski, kama mwanafunzi anataka anachukua na kuandikisha jina lake na tarehe ya kurudisha ili na wenzake wasome,” anasema Hilder Kajubili, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mpanda iliyopo Kyela.

Mwalimu Kajubili anasema licha ya kukosa maktaba, bado vitabu havikidhi mahitaji ya wanafunzi wote katika shule hizo na kuongeza tatizo kwa wanafunzi kukosa fursa ya kusoma vitabu.

Tofauti na wenzao wa vijijini kama wilaya za Kyela, Mbarali na Rungwe, wanafunzi wa jiji la Mbeya wanaosoma karibu na Maktaba Kuu ya mkoa wa Mbeya wao hupata fursa ya kujisomea katika maktaba hiyo siku za mwisho wa wiki au baada ya masomo ya kila siku.

“Watoto wanakuja walio karibu na mazingira ya hapa mfano wanafunzi wa shule ya msingi Sisimba na zingine zilizopo maeneo ya jirani huja karibu kila siku,” anasema Mkutubi Mkuu wa Maktaba ya mkoa wa Mbeya, Justine Lwambano na kuongeza;

“Wanafunzi wanaopenda kusoma bila kuazima kitabu chochote huwa hawalipi kitu chochote zaidi ya muda wake tuu.”

Wanafunzi wanaopenda kuazima vitabu katika maktaba ya Mbeya hulazimika kulipa ada ya uanachama kwa mwaka mmoja ili kusaidia wanachama wanaopenda kwenda na vitabu nyumbani au shuleni kuvisomea kwa muda fulani.

Licha ya kuwa siyo wazazi wote wanaweza kumudu gharama za kulipia ada ya mwezi ya maktaba ya mkoa bado njia hiyo inaonekana kuwa ahueni kwa kuwa watoto wanauhakika wa kupata vitabu vya aina yeyote wanavyohitaji.

“Gharama za kuwa mwanachama wa maktaba ni Sh5,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wa shule ya msingi hivyo nishauri wazazi wahimize watoto wao waje. Hii ni kwa sababu ni vigumu mzazi kununua vitabu vyote ila kwa kuwa mwanachama basi wataweza kuazima vitabu vya kusoma kutoka maktaba,” anasema Lwambano.


Wafahamu masomo yanayotakiwa ili kusomea urubani? Kuyafahamu masomo hayo tembelea Elimu Yangu.


Hata wakati Serikali ikiendelea kujipanga kujenga maktaba, baadhi ya wadau wameamua kujitolea ili angalau makali ya uhaba huo.

Wilayani Kyela, Asasi ya The Mango Tree ilijenga maktaba ya kisasa ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa wilaya hiyo kwenda kujisomea ili wapate maarifa na kufaulu mitihani kama wengine walio na fursa hiyo.

Katibu wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Kyela, Loth Mwangamba anasema maktaba hiyo kubwa inatumiwa na wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari wilayani hapo.

Mwangamba, aliyekuwepo kwenye kamati iliyoratibu ujenzi wa maktaba hiyo, anasema maktaba hiyo ina vitabu vingi vya kutosha kuwasaidia watoto kupata maarifa ya msingi yatakayowasaidia kufaulu vyema mitihani yao.

Hata hivyo sio wanafunzi wote wanapata fursa ya kwenda kusoma katika maktaba hizo kutokana na umbali wa makazi wanakoishi zaidi ya kutegemea kusoma vitabu wakiwa darasani.

Wadau waitupia jicho mitaala ya elimu

Edson Anthony, anayefanya kazi na shirika moja nchini linalojishughulisha na ujenzi wa maktaba katika shule za sekondari, ameishauri serikali kuungana na asasi za kiraia kujenga maktaba ili kuongeza mwamko wa wanafunzi kusoma vitabu na kuongeza ubora wa elimu.

 “Suala la kubadilika kwa mitaala pia ni changamoto kubwa katika maktaba hivyo Serikali inabidi iweke mipango sahihi katika kuhakikisha hawabadili mitaala hovyo hovyo. Hii itasaidia maktaba ziwe na vitabu vitakavyotumiwa na wanafunzi,” anasema Anthony.

Lini Serikali itatua tatizo la maktaba?

Kutokana na changamoto zilizopo katika mkoa wa Mbeya, suala la maktaba kwa shule ya msingi linaonekana kuwa sio kipaumbele kwa sasa kwa kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu mingine yakiwemo madarasa.

“Tuna changamoto kubwa kwa shule za msingi hata vyumba vya madarasa ni vichache ukilinganisha na wanafunzi waliopo ila kwa shule ya Sekondari angalau zipo zenye maktaba kwa ajili ya wanafunzi,” anasema Pauline Ndigeza, Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya.

Ili kutatua changamoto hiyo kwa haraka, Ndigeza anawakaribisha wadau wa elimu kwenda katika Mbeya kusaidiana na serikali kujenga maktaba na kuwahakikishia wanafunzi mazingira mazuri ya kusomea.