November 24, 2024

Ukosefu wa mtaala changamoto inayogharimu watoto wenye uziwi Tanzania

Walimu waomba Serikali ianzishe mtaala maalum kwa watoto wenye uziwi ili waweze kupata elimu bora kama wengine.

Mwalimu Mary Kaluzi wa Shule ya Msingi Twiga iliyopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam akifuatilia namna wanafunzi wake wenye uziwi wanavyojibu maswali darasani hivi karibuni. Picha| Zahara Tunda.

  • Walimu walia na ukosefu wa mtaala maalumu kwa wanafunzi wenye uziwi nchini.
  • Ukosefu wa misamiati ya masomo ya sayansi, uraia na historia  bado ni  changamoto.
  • Dakika 40 zaelezwa kutotosha kuwafundisha watoto hao wenye mahitaji maalum.
  • Wadau wataka elimu ya ufundi kwa vitendo iongezwe ili kuwapa ujuzi wanafunzi hao.

Dar es Salaam. Wakati wanafunzi wenzie wenye miaka 20 wakiwa sekondari, Abdulkareem Said anayekabiriwa na uziwi bado yupo darasa la 5 katika shule ya msingi Twiga wilayani Temeke jijini hapa akiendelea na safari ya kutimiza ndoto yake ya kufikia elimu ya juu. 

Licha ya maisha yake magumu yaliyochangia kuacha shule na baadae kurudi tena shuleni ili aweze kumalizia elimu yake ya shule ya msingi, sehemu kubwa ya kuchelewa kuhitimu masomo yake imechochewa na kuchelewa kuelewa masomo kutokana na muda mfupi unaotumika katika vipindi darasani.  

Kwa sasa wanafunzi wenye uziwi hutumia miaka 10 ili kumaliza elimu yao ya shule ya msingi ikiwa ni tofauti na wanafunzi wasio walemavu ambao hutumia miaka saba tu kumaliza elimu hiyo.

Ili waelewe vyema wanafunzi wenye uziwi kama Abdulkareem, walimu hutumia zaidi lugha ya alama pamoja na vitendo kuwaelimisha.

Hata hivyo,  mtaala uliopo unawanyima wanafunzi kama Abdulkareem fursa ya kufikia malengo yao katika masomo baada ya walimu kueleza kuwa hauwapi muda wa kutosha wa kujifunza na kuelewa vizuri wanachojifunza.

Kwa kawaida ratiba iliyopo kwenye mtaala wa sasa inampa mwalimu dakika 40 tu za kufundisha ikiwa ni muda sawa kwa wanafunzi wote wa shule ya msingi wenye mahitaji maalum na wasio walemavu. 

Abdulkareem ni miongoni mwa wanafunzi 180 wenye uziwi wa Manispaa ya Temeke katika nagazi ya elimu ya msingi wanaosubiri majaliwa ya Serikali kuwaandalia mtaala maalum kukidhi mahitaji yao. Takwimu kutoka kitengo maalumu cha manispaa hiyo zinabainisha kuwa wanafunzi hao wamegawanywa  katika shule nne tu za halmashauri hiyo yenye shule za msingi 126 hadi mwaka 2017.

Shule ya Msingi Twiga anayesoma Abdulkareem ina wanafunzi 42, Temeke 70, Mbagala kuu 26 wakati Mtoni ikiwa na wanafunzi 42.

Mbali na kuandikisha wanafunzi wenye uziwi, baadhi ya shule hizo zinahudumia pia wanafunzi wenye matatizo ya akili pamoja na wasiona.

“Kufundisha ni dakika zilezile 40 na mada ni ile ile sawa na wanafunzi wanaosikia vyema. Hii ni changamoto kwa sababu inabidi umfundishe mwanafunzi mmoja mmoja, wakati hawa wanahitaji vitendo zaidi kuliko maneno,” anasema Mary Kalozi ambaye ni mwalimu wa hesabu wa Abdulkareem.

Mwalimu Mary anasema sehemu kubwa ya wanafunzi wenye uziwi hawawezi kumaliza maswali katika majaribio ya saa moja na nusu kwa sababu ni ngumu sana kwao kusoma sentensi ndefu na hata kwenye hesabu swali moja la kufanya dakika mbili wao hutumia dakika tano ili waweze kupata jibu sahihi.

Mtaala wa elimu ni mwongozo wa masomo unaotoa dira ya mafunzo yanayotakiwa katika utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi katika ngazi fulani ya elimu.

Mbali na ufinyu wa muda katika vipindi, wanafunzi hao wenye uziwi wanakabiriwa na ugumu wa misamiati inayotumika katika masomo yao ambayo baadhi haitafsiriwa katika lugha ya alama. 

Walimu wa wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wanaeleza kuwa huwa ni vigumu kwa wanafunzi hao kufaulu kwa kiwango cha wenzao wasio na ulemavu kutokana na kutokuwepo misamiati ya kutosha ambayo ni chanzo cha kupelekea kuunda sentensi ambazo zitamsaidia mwenye uziwi aweze kujieleza vyema katika mitihani.

“Msamiati haijitoshelezi hasa katika haya masomo ya Maarifa ya Jamii. Ilitakiwa wawe na mtaala wao kwa vitu vichache vinavyoeleweka kwa kuwa unaweza kumwambia mwanafunzi neno Kani Mnyanyuko halafu akashindwa kukuelewa,” anasema mwalimu Sedute wa shule ya msingi Twiga.

Ubao wenye alfabeti  za lugha ya alama na namba ambao hutumika kuwafundishia wanafunzi wenye uziwi katika Shule ya Msingi Mbagala Kuu katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam. Picha| Zahara Tunda.

Walimu hao wanasema kuwa kama mtaala wao ungehusisha na elimu ya ufundi basi mwanafunzi kama Abdulkareem angeweza kupata ujuzi ambao ungemsaidia kufanya vizuri katika masomo na hata kujiajiri mara baada ya kumaliza elimu ya msingi na kushindwa kuendelea mbele.

Ukosefu wa msingi mzuri katika kujifunza umefanya sehemu kubwa ya watoto wenye mahitaji maalumu kama wenye uziwi kutoendelea na masomo ya sekondari kutokana na kufeli vibaya au kuacha shule njiani. Hata wale wanaoendelea na masomo ni wachache hufaulu kwenda ngazi za elimu ya juu. 

Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017 wanafunzi wote 21 wa shule ya sekondari ya Njombe Viziwi mkoani walifeli mtihani huo.

Wadau wa elimu wanashauri Serikali kuajiri walimu wengi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum na lugha ya alama inatakiwa kufundishwa tangu ngazi ya chini ili kuongeza uelewa kwa watoto hao.

“Viziwi kuanzia chekechea hadi sekondari wafundishwe kwa lugha ya alama. Njia ya kujifunza kwa kuona itumike zaidi,” anasema Nidrosy Mlawa, Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (Chavita).

Mlawa  anatoa wito kwa Serikali kuajiri walimu viziwi au walimu wenye taaluma ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum ili waweze kuwafundisha wenye uziwi na kuleta morali ya kujifunza kwa viziwi.

“Naomba Serikali itoe msisitizo wa utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (UNCRPD), Sheria ya Watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 na Sera ya Elimu na Mafunzo  ya mwaka 2015,” anasema Mlawa.

Hata wakati wanafunzi wenye uziwi wakisubiri Serikali kuajiri walimu maalum ili kukidhi mahitaji, Mtaalam wa kutafsiri lugha Jonathan Livingstone anaisihi Serikali kutumia mtaala wa lugha ya alama kufundishia viziwi, kuboresha madarasa kwa kufuata mfumo wa nusu duara  kwa madarasa ya wanafunzi wenye uziwi.

“Kuwepo pia na vifaa vya ufundishaji kama laptop (kompyuta mpakato) na projekta na mazingira mazuri yatakayo wawezesha wanafunzi kuwa jumuishi,” anaeleza Jonathan.

Serikali inakiri kuwepo changamoto ya uhaba wa walimu hao na kwamba inaendelea na mkakati wa kuzitatua.

“Bado tuna changamoto kubwa hasa kutokana na kuwa na walimu wachache, madarasa na mtaala nao sio rafiki kwa wanafunzi viziwi. Hili ni kundi lililosahaulika hivyo juhudi binafsi zinahitajika kwa wadau wote wa elimu kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora,” anasema Tatu Salumu, Afisa wa elimu maalum wa Manispaa ya Temeke.

Salumu anasema kuwa Serikali imeahidi kuwa itawaajiri walimu zaidi wa kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye uziwi. Hata hivyo, haijawa bayana ni lini itatekeleza ahadi hiyo.

Ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu bora yenye manufaa katika maisha yao, wadau wanashauri kuwa taala wa wanafunzi hao inabidi uwe rafiki kwa wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo na kuwa chanzo cha kuleta maendeleo nchini na katika jamii zao. 

Wanafunzi wenye uziwi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Twiga katika Manispaa ya Temeke wakitoa salamu darasani hivi karibuni. Wanafunzi hao wanahitaji mtaala maalum na misamiati zaidi ili waweze kuelewa masomo yao. Picha| Zahara Tunda.