November 24, 2024

Uganda kuwatoza kodi watumiaji wa mitandao ya kijamii

Hatua hiyo inafanana na utaratibu mpya wa Serikali ya Tanzania wa kuzitoza tozo za usajili na leseni blogu, tovuti na televisheni za mtandaoni.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Kiongozi huyo ameagiza watumiaji wa mitandao ya kijamii kutozwa kodi kwa madai ya kupunguza “umbea”.

•Hatua hiyo inafanana na utaratibu mpya wa Serikali ya Tanzania wa kutoza tozo za leseni na usajili blogu, tovuti na televisheni za mtandaoni.


Wakati Tanzania ikianza kutumia Kanuni mpya za Maudhui ya mtandaoni, serikali ya Uganda imesema itawatoza kodi watumiaji wa mitandao ya kijamii ili kukabiliana na ‘umbea’ unaoendelea katika mitandao hiyo.

Zoezi hilo litaanza Julai mwaka huu ambapo serikali itawatoza Sh200 za Uganda wateja wa kampuni za simu wanaotumia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Viber, Twitter na Skype. Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Yoweri Museveni kuiandikia barua Hazina Machi 2018 akielezea jinsi mijadala isiyo na tija kama ‘umbea’ inavyolikosesha taifa hilo mapato na muda wa uzalishaji mali.

Ikiwa ni sehemu ya kodi mpya, kampuni za simu zinazotoa huduma ya vifurushi vya intaneti zitawajibika kuwa na takwimu za wateja wao na kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Matia Kasaija tayari ameanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Kodi ya mwaka 2014 na muswada umepelekwa bungeni kwa mapitio baada ya kupitishwa na Baraza la Mawaziri.

Uamuzi huo sasa utawafanya watumiaji wa mitandao hiyo nchini humo kutoboa zaidi mifukoni kugharamia mawasiliano ikiwa ni gharama nje ya zile za kununua intaneti na simu za mkononi. Wastani wa kipato cha mtu kwa mwaka nchini Uganda ni Dola za Marekani 662 (Sh1.5 milioni) kwa takwimu za Benki ya Duni za mwaka 2016.

Akihojiwa na wanahabari nchini humo, Waziri Kasaija alisema kodi itakayotozwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii itasaidia kuimarisha usalama wa taifa na kuongeza uzalishaji wa umeme.


Soma zaidi kuhusu: Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify

                                  Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo


“Kodi hii itasaidia kuimarisha usalama wa nchi na kuongeza umeme ambao mtatumia ili kufurahia zaidi mitandao ya kijamii,” amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo.

Chapa za mitandao maarufu ya kijamii duniani. Watumiaji wa mitandao hii wataanza kutozwa kodi kuanzia Julai mwaka huu nchini Uganda. Picha kwa hisani ya VentureBeat.

Kawaida, watumiaji wa mitandao ya kijamii hununua vifurushi vya intaneti kupitia simu lakini bado haijafahamika wazi jinsi serikali itakavyokata kodi hiyo kwa watumiaji hao au namna watakavyoweza kujua watu walioingia kwenye mitandao kama Facebook na Twitter. Kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa Waganda kuwa kila mtu mwenye simu ya mkononi inayotumia intaneti atatozwa kodi.

Mabadiliko hayo yamewashangaza watu wengi hasa watumiaji wa teknolojia ya mawasiliano ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa intaneti nchini humo ni wa asilimia 22 tu ikilinganishwa na Tanzania yenye asilimia 45 hadi Desemba mwaka jana.  Uamuzi huo umekosolewa vikali kwa baadhi ya wadau kuhitimisha kuwa ni makakati wa serikali ya Museveni kudhoofisha uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa sababu Rais Museveni anakusuidia kufanya mabadiliko ya sheria ili kumruhusu kugombea tena nafasi ya urais.

Kama ilivyo Uganda, Tanzania nayo imeanza kutumia kanuni mpya za maudhui ya mtandaoni ambazo zimeongeza nguvu kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao  ya mwaka 2015. Sheria hizo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau wa demokrasia na maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji nchini.

Wadau wengi wamekuwa wakiikosoa utawala wa Rais John Magufuli kwa kufungia baadhi ya magazeti nchini licha ya Serikali kueleza kuwa hatua ambazo huchukuliwa hufuata taratibu na sheria za nchi.