November 24, 2024

Kigogo wa Safaricom kuiongoza Vodacom Tanzania

Ni Sylvia Mulinge atakayempokea mikoba Ian Ferrao kuanzia Juni mwaka huu.

  • Atakuwa ni moja ya wanawake wachache barani Afrika kuongoza kampuni kubwa ya huduma za simu.
  • Atamrithi Ian Ferrao aliyefanikisha Vodacom Tanzania kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano kujiorodhesha DSE.

Dar es Salaam. Sekta ya mawasiliano Tanzania imepata kigogo mpya mwanamke aliyekuwa Safaricom  Kenya atakayeiongoza Vodacom Tanzania Plc kuanzia Juni mwaka huu kama Mkurugezi Mkuu.

Sylvia Mulinge ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Masoko na Biashara wa Safaricom alitangazwa Jumatatu (Aprili 9 2018) kuwa atachukua mikoba ya Ian Ferrao anayemaliza muda wake mwezi ujao. Mulinge (41) atakuwa moja wanawake wachache wanaongoza kampuni kubwa za mawasiliano barani Afrika. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Safaricom, Bob Collymore amenukuliwa na gazeti la Business Daily la Kenya kuwa  Mulinge ameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi ambao umeusaidia sana kampuni hiyo kuivusha katika kipindi kigumu.

“Kwa miaka takribani 17 ya kazi amejenga heshima kama moja ya wafanyabiashara, kiongozi, mshauri, mtu wamafanikio hakika Safaricom tutamkumbuka,’’anasema Collymore.

Safaricom ambayo toka ilipo wekwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi (NSE) Machi 2007 imekuwa ni kampuni kubwa yenye mapato kwa mwaka yanayofikia Sh200 bilioni za Kenya (Sh4 trilioni).

Mama huyo mzaliwa wa Kenya atakuwa na kibarua cha kuisukuma Vodacom Tanzania katika kilele cha mafanikio ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu kampuni hiyo ilipoingia katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Vodacom ilijiorodhesha DSE kutii Sheria ya Mawasilaino ya Kieletroniki na Posta (Epoca) na Sheria ya Fedha ya mwaka 2016  inayozitaka kampuni za mawasilano kuuza asilimia 25 ya hisa zake katika sokob hilo. 

Ferrao anaondoka akiwa ameifanya Vodacom kuwa kampuni ya kwanza nchini kujiorodhesha DSE. 

Ujio wa Mulinge huenda ukaongeza matumaini zaidi kwa wawekezaji wa kampuni hiyo ambayo Aprili 9 2018 hisa yake moja ilikuwa na thamani ya Sh850. 


Ni historia: watumiaji wa intaneti tanzania sasa wafikia milioni 23


Takwimu za robo ya mwisho ya mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilizotolewa mapema mwaka huu zinaonyesha Vodacom inaongoza kwa kuwa na wateja milioni 12.86 kati ya kampuni za simu saba zinazotoa huduma hiyo hapa nchini. Vodacom ina watumiaji wa Mpesa zaidi ya milioni  nane. 

Tanzania kwa sasa ina watumiaji wa simu milioni 40 wakati wale wa intaneti wamefikiamilioni 23.