July 8, 2024

Abiria Air Tanzania waongezeka zaidi ya mara tano ndani ya miaka mitatu

Ongezeko hilo limechangiwa na maboresho ndani ya shirika hilo la ndege la umma ikiwemo ununuzi wa ndege mpya sita.

  • Ongezeko hilo limechangiwa na maboresho ndani ya ATCL ikiwemo ununuzi wa ndege mpya sita. 
  • Pia idadi ya watlii, ajira na mapato ya ATCL yameongezeka katika kipindi hicho.
  • ATCL inajipanga kujitanua zaidi ili kufaidika na soko la kimataifa. 

Dar es Salaam. Idadi ya abiria wanaosafiri na ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) imeongezeka zaidi ya mara tano katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutokana na Serikali kufanya maboresho mbalimbali ndani ya shirika hilo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya sita. 

Akiwasilisha hotuba ya Hali ya Uchumi mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2019/20,  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria 49,854 mwaka 2015/16 hadi abiria 242,668 mwaka 2018/19. 

Ongezeko hilo ni sawa na  asilimia 79.45 ya idadi ya abiria waliosafiri mwaka 2015/2016. 

Dk Mpango amesema ongezeko la idadi ya abiria wa ATCL linatokana juhudi za Serikali kuliboresha shirika hilo na kuliongezea uwezo wake wa kufanya kazi na kuwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi kwa huduma bora za ndege. 

Maboresho na ongezeko la abiria limetokana na Serikali kununua ndege sita aina ya   Boeing 787-8 Dreamliner, tatu aina ya Bombardier Dash 8-Q400 na mbili aina ya Airbus A220-300 ambapo nyingine mbili zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwaka huu.

“Lakini pia tumelipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na ndege nyingine moja  Bombardier Dash 8-Q400 zinazotarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwaka huu 2019,” amesema Waziri Mpango.


Zinazohusiana: 


Pia Serikali imegharamia mafunzo ya marubani 51, wahandisi 14 na wahudumu (66 na kuanza kwa ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). 

Kuimarika kwa ARCL siyo tu kumechangia kuongezeka kwa abiria bali watali wanaoingia nchini, vituo na safari za ndege za shirika hilo zimeongezeka na kusaidia kutengeneza ajira kwa Watanzania waliobobea katika sekta ya usafiri wa anga na ukuaji wa sekta ya utalii. 

“Kuongezeka kwa idadi ya vituo vya nje kutoka kimoja (Hahaya – Comoro) hadi vituo 5 (Hahaya, Bujumbura, Entebbe, Harare, na Lusaka); kuongezeka kwa idadi ya ajira kutoka 134 hadi 448; na kuongezeka kwa mapato ya Shirika kutoka Sh11.75 bilioni hadi Sh45.6 bilioni. 

“Vile vile, kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania kumechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2016 hadi watalii 1,505,702 mwaka 2018 ambao wameliingizia Taifa mapato ya dola za Marekani bilioni 2.4,” amesema Waziri Mpango. 

Hivi karibuni ATCL inatarajia kuanza safari za moja kwa moja kwenda Mumbai (India), Guangzhou (China) na Johannesburg (Afrika Kusini), ikiwa ni hatua ya kujitanua katika anga la kimataifa.