October 6, 2024

AfDB kuipandisha hadhi Tanzania utoaji mikopo

Mwakilishi wa benki hiyo nchini amesema Tanzania ikipandishwa hadhi itapata zaidi mikopo kupitia dirisha la benki hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango (kushoto), akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Alex Mubiru (kulia) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Jijini Dodoma. Picha| Waziri wa Fedha na Mipango.


  • Mwakilishi wa benki hiyo nchini amesema Tanzania ikipandishwa hadhi itapata zaidi mikopo kupitia dirisha la benki hiyo.
  • Kupandishwa hadhi kunategemea na uchumi wa nchi kufanya vizuri.
  • Tanzania ikipanda hadhi itaweza kupata mkopo hadi Sh1.8 trilioni kwa mwaka.

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inatarajia kuipandisha daraja Tanzania kutoka katika hadhi ya kunufaika na Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF) hadi kuwa na hadhi ya kuiwezesha kupata fedha zaidi kupitia dirisha la benki hiyo. 

Endapo Tanzania itafanikiwa kupandishwa hadhi, itaweza kunufaika na ongezeko la fedha kutoka hiyo kutoka Dola za Marekani milioni 350 (takriban Sh804.6 bilioni) kwa mwaka hadi Dola za Marekani milioni 812 (takriban Sh1.8 trilioni) kwa mwaka. 

Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo Tanzania, Dk Alex Mubiru  amesema hatua hiyo ya kupandishwa hadhi au kupandishwa daraja inatokana na uchumi wa nchi kufanya vizuri hususan katika maeneo ya kasi ya ukuaji wa uchumi na kuwa na deni himilivu.

“Hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kupata fedha zaidi kutoka katika Benki hiyo na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na vipaumble kwa Serikali,” amesema Mubiru kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mwakilishi huyo amebainisha mapendekezo hayo leo (Julai 9, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango.

Hata hivyo, haijafahamika bayana ni lini AfDB itaipandisha hadhi Tanzania ili iweze kunufaika na mikopo ya benki hiyo ya Afrika. 


Somo zaidi: AfDB yaipatia Serikali mkopo wa zaidi ya Sh589 bilioni


Katika mazungumzo yao, Dk Mpango ameeleza kuwa Serikali inajivunia kufanya kazi pamoja na benki ya AfDB kwa kuwa benki hiyo imekuwa na masharti rafiki katika upatikanaji wa mikopo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango leo inabainisha kuwa benki hiyo ina mtazamo chanya katika maendeleo ya watu na kuwa dira katika mipango ya maendeleo na kuahidi kushirikiana nao vyema katika kukuza uchumi wa nchi.

Aidha, waziri huyo ameipongeza benki hiyo kwa kukubali kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara ya mzunguko jijini Dodoma ya kilomita 110.2 kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato.

Amebainisha kuwa  uamuzi huo utalisaidia jiji hilo kukua kwa kasi kuwaunganishwa kwa miundombinu imara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara nchini. 

Benki hiyo, imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mikopo ya masharti nafuu.