AfDB yaipatia Tanzania mkopo wa Sh323 bilioni kuzalisha umeme
Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimesaini mikataba miwili ya mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 140 (takriban Sh323.4 bilioni) kwa ajili ya kufadhili mradi wa kufua umeme wa nguvu ya maji wa Malagarasi uliopo mkoan
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba (kulia), na Nnenna Nwabufo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Kanda ya Afrika Mashariki, wakibadilishana hati za mikataba miwili ya mkopo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 140 (takriban sSh323.39 bilioni) kwa ajili ya kufadhili Mradi wa kufua Umeme wa Malagarasi, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam. Picha| Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.
- Fedha hizo ni kwa ajili ya kufadhili mradi wa kufua umeme wa nguvu ya maji wa Malagarasi uliopo mkoani Kigoma.
- Utasaidia kuongeza uwezo wa kusambaza wa umeme kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma.
Dar es Salaam. Sasa, Watanzania wana uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme ili kufanikisha shughuli za uzalishaji na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimesaini mikataba miwili ya mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 140 (Sh323.4 bilioni) kwa ajili ya kufadhili mradi wa kufua umeme wa nguvu ya maji wa Malagarasi uliopo mkoani Kigoma.
Kiasi hicho cha fedha kitasaidia kukidhi bajeti ya mradi huo ambayo ni Dola za Marekani milioni 144.2 (Sh334.3 bilioni) ambapo Serikali ya Tanzania itachangia Dola za Marekani milioni 4.14 sawa na Sh9.6 bilioni zilizobaki.
“Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 120 zitatolewa kupitia dirisha la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Dola za Marekani milioni 20 kupitia Africa Growing Together Fund”, ameeleza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba.
Mikataba ya mkopo huo wenye masharti nafuu imesainiwa leo Mei 26, 2021 jijini Dar es Salaam na Tutuba kwa niaba ya Serikali na Nnenna Nwabufo, Mkurugenzi Mkuu wa AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki.
Tutuba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utalijengea uwezo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa usambazaji wa vifaa vya kuunganisha wateja 4,250 katika Wilaya za Kigoma, Kibondo na Kasulu ikiwemo kaya 1,000 zenye kipato cha chini, zahanati nne na shule za msingi sita.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa kituo kipya cha uzalishaji wa umeme wa gridi ya megawati 49.5 chenye uwezo wa kuzalisha wastani wa GWh 181 za umeme kwa mwaka ili kuboresha usambazaji wa umeme na kupunguza utegemezi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta mazito,” amesema Tutuba
Mradi huo utajumuisha ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme, upanuzi wa mtandao wa kusambaza umeme wa kilovoti 132 na ununuzi wa transfoma mpya 15 ili kuongeza uwezo wa kusambaza wa umeme kwa wananchi.
Soma zaidi:
- CHATI YA SIKU: Kinachofahamika kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali mwaka 2017-2018
- Sababu zilizofanya Tanzania iporomoke viwango vya ufanyaji biashara duniani
Mradi huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya AfDB vya kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya nishati ya umeme ili kuchochea maendeleo ya viwanda na kuboresha maisha ya watu barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo amesema kuwa mradi huo ni moja ya miradi sita iliyoidhinishwa na benki hiyo katika kipindi cha miaka mitatu.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma, mradi wa uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato, barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu, barabara ya Bagamoyo – Horohoro – Lunga – Malindi na mradi wa usambazaji umeme wa Nyakanazi – Kigoma.
Nnenna amesema kuwa uwekezaji wa benki yake nchi Tanzania imefikia thamani ya dola za Marekani bilioni 2.4 (Sh5.4 trilioni) zilizowekezwa katika sekta za miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji na usafi wa mazingira, kilimo, utawala bora na fedha.