November 24, 2024

Afrika yatakiwa kuunganisha nguvu mapambano ya Corona

Yatakiwa kuweka mikakati thabiti ya muda mfupi na mrefu kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona ikiwemo kuimarisha ushirikiano na kulegeza sera za kifedha kuwasaidia wananchi wao kuendeleza shughuli za uzalishaji.

  • Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wamezitaka nchi za Afrika kuungana kumaliza janga hilo.
  • Pia zimetakiwa kutoa ahueni ya kifedha kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wamezitaka nchi za Afrika kuweka mikakati thabiti ya muda mfupi na mrefu kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona ikiwemo kuimarisha ushirikiano na kulegeza sera za kifedha kuwasaidia wananchi wao kuendeleza shughuli za uzalishaji.

Takwimu za Shirika Afya Duniani (WHO) za hadi jana Aprili 18, 2020 zinaeleza kuwa nchi za bara hilo  zimeripoti wagonjwa 12,360 wa Corona huku kati yao 586 wamefariki dunia. 

Wakizungumza jana (Aprili 17, 2020) katika mkutano wa pamoja na wanahabari kuhusu hatua walizochukua kuisaidia Afrika kupambana na Corona, viongozi wa juu wa taasisi hizo mbili wamesema wako pamoja na watafanya kazi na nchi za Afrika kutokomeza janga la Corona.

Viongozi hao ambao ni Rais wa Benki ya Dunia David Malpass na mwenzake Kristalina Georgieva wa IMF wamesema fedha zinazopelekwa Afrika kwa sasa zisaidie kuimarisha mifumo ya sekta ya afya ili kuokoa maisha ya watu wengi maskini.

Pia wamezungumzia suala la marufuku ya kutembea na upatikanaji wa chakula, iangaliwe upya kulingana na mazingira ya kila nchi ili kutokuvunja haki za binadamu, ikizingatiwa asilimia 89 ya kazi za watu bara hilo siyo rasmi. 

Wameeleza mikakati zaidi ielekezwe katika kuwaletea nafuu wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo kwa kuanzisha programu za kuwapatia mitaji, mikopo yenye masharti nafuu itakayowasaidia kujikimu kipindi hiki cha mlipuko wa Corona. 

“Benki ya Dunia itatumia uwezo wake wote kuwasaidia wananchi wa bara la Afrika kupambana na janga hili,” amesema Malpass katika mkutano huo. 


Zinazohusiana


Amesema kutokana na janga la Corona, hawawezi kukaa pembeni na ndiyo maana wametoa msaada wa dharura kwa nchi 30 za Afrika na wanaendelea kutoa msamaha wa kulipa madeni hasa kwa nchi zilizoathirika zaidi na COVID-19.

“Ujumbe wetu uko wazi. Tunasimama na Afrika kupunguza makali ya kusambaa kwa COVID-19,”amesema Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Georgieva. 

Amewataka washirika wa maendeleo na wahisani kuzisaidia nchi za Afrika ili zisiingie kwenye mdororo wa uchumi. 

Bara la Afrika linahitaji dola za Marekani 114 bilioni mwaka huu ili kufanikisha mapambano ya Corona ambapo  dola 70 bilioni zimepatikana kutoka wadau wa maendeleo wakiwemo IMF na Benki ya Dunia.