July 5, 2024

Aina tatu za habari za uzushi zinazopotosha kuhusu Corona

Aina hizo ni “misinformation”, “disinformation” na “malinformation”. Habari hizo zote hutumiwa kwa malengo tofauti ili kuzidisha athari za Corona.

  • Aina hizo ni  “misinformation”, “disinformation” na “malainformationtion”.
  • Habari hizo zote hutumiwa kwa malengo tofauti ili kuzidisha athari za Corona.
  • Kutosambaza habari hizo ni njia mojawapo ya kupunguza madhara kwa jamii.

Dar es Salaam. Upotoshaji kuhusu ugonjwa wa Corona umekuwa ukijitokeza kwa namna tofauti za habari ambazo mara nyingi husambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambako watu hukutana zaidi.

Bila kufahamu kwa undani kuhusu aina za habari za upotoshaji inaweza kuwa kazi ngumu hasa kwa wathibitishaji habari (fact checkers) kupambana na uzushi na uongo kuhusu janga hilo linaloitesa dunia kwa sasa.

Kwa mujibu taasisi ya uthibitishaji habari ya  First Draft, kuna aina tatu za habari za uzushi ambazo ni  “misinformation”, “disinformation” na “malinformation”.

Kwa sehemu kubwa uzushi wote wa Corona hufanyika kwa kutumia aina hizo tatu za habari za uzushi. Kila habari ina maana yake na inatumika tofauti:

1. Misinformation

“Misinformation” wakati mwingine hutambulika kama habari potofu ambapo hutokea kutokana na makosa mbalimbali ya kihabari ambayo yanafanyika kwenye habari. 

Makosa hayo yanaweza kuwa ya kisarufi, takwimu na hata tarehe. Mfano mwandishi badala ya kuandika “watu 10 wamefariki duni kwa ugonjwa wa Corona Tanzania” akasema “watu 100 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Corona Tanzania”

Kimsingi takwimu za hiyo habari zitakuwa zimepotosha na zinaweza kuzua taharuki kwenye jamii, licha kuwa mwandishi alikuwa hajadhamiria kupotosha. 

Hii huwatoa zaidi watengeneza maudhui na wanahabari kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo linahitaji umakini ili kuepuka mtego huo.


Zinazohusiana:



2. Disinformation

Aina hii ya habari ya uzushi, muandaaji anakuwa anajua anachofanya na anakuwa na dhamira ya dhati kufanya upotoshaji kuhusu jambo fulani ikiwemo Corona.

Habari ya aina hii inaweza kuwa na ukweli fulani au ikawa ya uongo kabisa ambapo muandaaji anaweza kutumia picha, tukio au habari iliyochapishwa tayari na kuibadilisha ili kutimiza makusudi aliyokusudia.

Mara nyingi muandaaji wa habari hii ya upotoshaji analenga kujipatia fedha isivyo halali, kuzua taharuki au kusababisha zaidi athari za kiafya kwa watu fulani. 

Mathalan, hivi karibuni wakati chanjo ya corona ilipoanza kutolewa duniani ilisambazwa habari picha kwenye mitandao ya kijamii hasa wa Whatsapp yenye chapa ya shirika la habari la CNN la Marekani inayoeleza kuwa wagonjwa wa Corona wameanza kula wenzao baada ya kupewa chanjo ya corona.

Msambazaji wa habari hiyo alifanya hivyo huku akijua habari hiyo haina ukweli kwa kuwa alichukuwa picha ya tukio lingine na kuihusisha na chanjo ya Corona.


3. Malinformation

Aina hii ya habari huwa ni ya kweli lakini inasambazwa ili kuleta madhara kwa wahusika. Mara nyingi habari za namna hii huibua taarifa za siri, faragha na binafsi za mtu au taasisi ili kumvunjia heshima au kumdhuru kifikra au saikolojia. 

Mfano, muandaaji anaweza kutengeneza video ikiwa inamuonyesha mtu akiwa faragha au kusambaza picha za mgonjwa wa Corona akiwa hospitali bila ridhaa yake ili kumnyanyapaa au kumvunjia heshima.

Kwa kutokufahamu kuhusu aina hizo tatu za habari, ni rahisi kwa watu kupotoshwa na kufanya mapambano ya Corona kuwa magumu. 

Njia rahisi na ya kwanza ili kukabiliana na habari za upotoshaji ni kupunguza kasi au kuacha kabisa kusambaza kwa watu bila kuzithibitisha kama ni za kweli kutoka mamlaka za afya.