September 29, 2024

Alichokisema RC Chalamila baada ya kukabidhiwa ofisi Mwanza

Mkuu wa Mkoa mpya wa Mwanza, Albert Chalamila ameahidi kukaa pamoja na viongozi wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga ili waweze kufanya biashara zao kwenye maeneo yaliyotengwa na siyo barabarani.

Mkuu wa Mkoa mpya wa Mwanza Albert Chalamila (kushoto) akitambulishwa kwa wafanyakazi wa mkoa huo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wa zamani John Mongella, wakati wa hafla ya kukabidhiana ofisi. Picha|Mariam John.


  • Ataka kuimarishwa kwa usalama na utulivu wa mkoa huo.
  • Atakaa na wafanyabiashara wadogo kuangalia namna nzuri ya kufanya biashara.
  • Atakiwa kushirikiana na wananchi ili kuleta maendeleo mkoani humo. 

Mwanza. Mkuu wa Mkoa mpya wa Mwanza, Albert Chalamila  ameahidi kukaa pamoja na viongozi wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga ili waweze kufanya biashara zao kwenye maeneo yaliyotengwa na siyo barabarani. 

 Akizungumza baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya ofisi kati yake na  aliyekuwa Mkuu huo, John Mongella ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha,  amesema wafanyabiashara hao  hawatakiwi kupanga bidhaa zao  barabarani. 

 Amesema miundombinu kama barabara itumike kwa misingi iliyowekwa isiingiliwe na kuharibiwa na wafabiashara hao huku akionya kundi hilo kutumika kisiasa kwa kuwa wafanyabiashara hao ni walipa kodi wakubwa wa baadaye. 

 Aidha, kiongozi huyo ameahidi  kukaa na wawekezaji wote wa mkoa huo na kuwahakikishia kuwapatia ushirikiano wote kwakuwa wafanyabiashara sio maadui. 

 ” Mwekezaji au mfanyabiashara sio adui ni suala la kukaa pamoja na kung’amua ili mambo yaende sawa, ” amesema Chalamila. 


Soma zaidi: 


Katika hotuba yake Chalamila ametaja moja ya ajenda kuu ya mkoa huo  ambayo itatakiwa kuwa endelevu ni kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa huo. 

Amewataka watendaji, kamati za  ulinzi na usalama za vijiji na mitaa ziimalishwe  ili kutimiza azma ya Serikali ya kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha  uchumi kwenye ukanda wa maziwa makuu. 

“Haya yote yatafanyika endapo kutaimarishwa ulinzi na usalama ndani ya mkoa  na  agenda hii ikawe ya kudumu na lisitokee doa lolote la ujambazi au wizi,” amesema Chalamila.

Akimkabidhi ofisi hiyo,  Mongella amemtaka Chalamila kufanya kazi pamoja na wananchi kwa kuwa watamsaidia katika utekelezaji wa shughuli zake. 

Amesema mkoa wa Mwanza ni wa pili katika ukusanyaji wa mapato ukitanguliwa na mkoa wa Dar es salaam, hivyo anatakiwa kuongeza kasi ya utendaji ili kuufanya mkoa huo kuendelea kuwa kitovu cha uchumi.