July 8, 2024

Anguko kubwa matumizi ya simu za mezani Tanzania

Licha ya wataalamu kubainisha kuwa simu za mezani zinaweza kuwa njia sahihi za kutunza nidhamu mahala pa kazi.

  • Ni watumiaji wawili tu kati ya 1,000 wanaotumia huduma za simu nchini wanatumia simu za mezani za waya. 
  • Machi mwaka huu zaidi ya watumiaji 46,000 wa simu za mezani waliachana nazo, ikiwa ni kiwango kikubwa kurekodiwa siku za hivi karibuni.

Dar es Salaam.Wakati watumiaji wa simu za mkononi wakiendelea kuongezeka hapa nchini upande mwingine watumiaji wa simu za mezani zinazotumia waya wanazidi kushuka kwa kasi kwa mujibu wa takwimu mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hadi Machi mwaka huu takwimu hizo za robo ya kwanza ya mwaka 2019 zinabainisha kuwa kulikuwa na watumiaji wa simu za mezani 78,081 kutoka watumiaji 124,159 walikuwepo Februari 2019, ikiwa ni anguko kubwa kuwahi rekodiwa ndani ya mwezi mmoja katika miaka ya hivi karibuni. 

Kwa takwimu hizo, watumiaji wa simu za mezani zinazotumia waya ni asilimia 0.2 tu ya watumiaji wote wa huduma za simu nchini ikiwa na sawa na watumiaji wawili tu kati ya 1,000.

Matumizi hayo ya simu za mezani yanapungua licha ya tafiti  kama za  Shirika la Du County Telecom la nchini Marekani kueleza umuhimu wa kuendelea kutumia simu za mezani kutokana  urahisi wake wakutumika unaoambatana na gharama ndogo za kupiga na kupokea simu ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wataalamu wa Tehama na mawasiliano waliiambia www.nukta.co.tz hivi karibuni kuwa simu za mezani bado zinatumika kama kitambulisho kwenye biashara  na taasisi za umma na njia rahisi ya kutunza nidhamu mahali pa kazi.

“Simu ya mezani ni identity (kitambulishi) ya biashara na ofisi,” anasema Clemence Kyara, Mhandisi wa Kompyuta kutoka Shirika la Code for Africa.  


Zinazohusiana:Miamala ya kifedha simu za mkononi yafikia Sh7.8 trilioni kwa mwezi Tanzania


Kyara anabainisha kuwa simu ya mezani inaweza kuwa njia sahihi ya kutunza nidhamu mahali pa kazi hasa katika kuhakikisha wafanyakazi wanakuwepo ofisini katika muda waliopangiwa kukamilisha majukumu yao. 

Pamoja na umuhimu huo bado simu hizo za mezani zimekumbwa na anguko kubwa Machi 2019 baada ya watumiaji 46,078 kuachana nazo ikiwa ni tofauti na Februari mwaka huu ambapo watumiaji 24 pekee walipungua. 

Mabadiliko ya teknolojia hasa ujio wa simu za mkononi yamechangia kwa kiwango kikubwa kuporomoka kwa matumizi ya simu hizo za mezani ambazo miaka 20 iliyopita ilikuwa ni moja ya alama ya utajiri miongoni mwa wanafamilia nchini. 

Wakati watumiaji wa simu za mezani za waya wakipungua, wale wa simu za mkononi wanazidi kuongezeka kutoka watumiaji milioni 43.7 Januari mwaka huu hadi watumiaji milioni 43.9 Machi 2019.

Kwa mujibu wa TCRA  katika kipindi hicho cha miezi mitatu watumiaji takribani 214,828  waliongezeka na kufanya Watanzania wanaotumia simu za mkononi hadi mwezi Machi kuwa sawa na asilimia 99.8 ya watumiaji wote wa huduma za simu Tanzania.

Mdau wa mitandao ya kijamii, Kenney Mmari ameimbia nukta(www.nukta.co.tz) kuwa ongezeko la watumiaji wa simu Tanzania ni fursa kubwa kwa vijana nchini na watu walio wekeza kwenye teknolojia hapa nchini.

“Watu wote wali wekeza kwenye mfumo wa mawasiliano na teknolojia  na wanatengeza programu tumishi wanatakiwa kuona ongezeko hilo la watumiaji wa simu Tanzania kama fursa ya wao kuendelea kutatua matatizo mbalimbali kwa kupitia teknolojia,” amesema Mmari. 

Pia ameleza kuwa kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mikononi kunatoa tafsri kuwa huduma za mawasiliano nazo zinazidi kuongezeka hapa nchini hadi maeneo ya vijijini ambayo hayakuwa yamefikiwa hapo awali.