October 6, 2024

Apps za elimu zitakazowasaidia wanafunzi 2019

Ni miongoni mwa Apps zinazowarahisishia wanafunzi kupata maudhui ya vitabu na masomo katika viganja vyao na kuwaondolewa changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifunzia shuleni.

  • Ni miongoni mwa Apps zinazowarahisishia wanafunzi kupata maudhui ya vitabu na masomo katika viganja vyao.
  • Wadau wa elimu washauri wamiliki wa Apps hizo waongeze wigo ili kuwafikia wanafunzi waliopo vijijini.

Dar es Salaam. Changamoto ya upatikanaji wa dhana  za kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hasa vitabu inaendelea kutafutiwa suluhu na wadau mbalimbali wa elimu wakisaidiwa na teknolojia.

Wabunifu wa teknolojia wanatengeneza programu tumishi (Apps) ili kuwafikia wanafunzi popote walipo kwa maarifa na ujuzi utakaowasaidia kufanya vizuri katika mitihani yao.   

Nukta inakuletea baadhi ya Apps za elimu za kuziangazia mwaka 2019 ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwa msaada katika sekta ya elimu wakati huu ambao wadau wanatafuta njia mbalimbali kuwawezesha wanafunzi wafanya  vizuri.  


Mtabe

Programu hii imelenga zaidi wanafunzi wa sekondari na inatumia mfumo wa meseji za kawaida (SMS) na Apps zinazotumiwa na simu janja kupata maarifa kulingana na mahitaji na maeneo wanayoishi. 

Hata wanafunzi wanaishi vijijini ambako wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi vya kujifunzia, kupitia simu za kawaida wanaweza kupata maudhui ya kujifunzia.  

“Tunatumia teknolojia ya meseji na mfumo wa kiintelejensia uliotengenezwa kufikisha maudhui ya kujifunzia kwa wanafunzi wasioweza kununua vitabu na wale wasio unganishwa na intaneti” inasomeka sehemu ya maelezo katika tovuti ya Mtabe.


Soma zaidi: 


Soma App

Ni programu mahususi iliyowalenga watanzania wanaotaka kusoma katika shule na vyuo vilivyopo nje ya nchi. Inarahisisha taratibu za udahili ambapo mwanafunzi halazimiki kuzunguka na nyaraka kwenye ofisi mbalimbali kukamilisha maombi. 

Atupelye Weston anayesomea Shahada ya Uzamivu ya  Sayansi ya Mazingira nchini Japan amesema kabla ya kutumia Soma app alijaribu zaidi ya miaka mitatu kuomba kupata nafasi ya kusoma vyuo vya nje lakini alikosa.  

“Kabla ya Soma app nimejaribu na kushindwa kupata dhamana ya elimu nje ya nchi kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini baada ya kutumia Soma app nimepata nafasi hiyo,” amesema Weston wakati akitoa ushuhuda wa programu hiyo.

Simu janja zikitumiwa vizuri zinaweza sehemu nzuri kwa wanafunzi kupata maarifa na ujuzi. Picha | Soma App.

Shule Direct

Ni programu tumishi inayolenga kuwafikia wanafunzi wa shule za sekondari wa kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo kupitia program hiyo, mwanafunzi anaweza kujipatia maudhui ya kujifunzia na hata kujipima kwa kutumia mitihani ya majaribio.

Baada ya mwandishi wetu kufanya majaribio ya program hii amegundua kuwa mwanafunzi anaweza kufanya mitihani, kusahishiwa papo kwa papo na baada ya kufanya mtihani huo, mwanafunzi hupewa alama zake za ufaulu.

Licha ya Apps hizo kuleta mageuzi ya upatikanaji wa maarifa katika sekta ya elimu, yapo mambo kadhaa ya kuangalia ili kuongeza ufanisi na kuwafikiwa wanafunzi wengi hasa wale ambao hawamiliki simu janja.  

“Sio rahisi kwa program hizi kuwasaidia wale ambao kweli wanakabiliwa na tatizo la uhitaji wa vitu hivyo. Anayendelea kufaidika bado ni mtoto wa mjini ambaye sio kwamba hana vitabu,” anaeleza Amina Kitula ambaye ni mzazi anayetumia Apps za elimu kuwafundishia watoto wake.