October 6, 2024

Apps zitakazowasaidia wanafunzi wakati wa mlipuko wa virusi vya Corona

Programu hizo za simu zinamuwezesha mwanafunzi kusoma masomo akiwa mtandaoni au kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS). Zinawasaidia wanafunzi kuwasiliana na walimu na kujadili mada muhimu za masomo.

  • Programu hizo za simu zinamuwezesha mwanafunzi kusoma masomo akiwa mtandaoni au kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
  • Zinawasaidia wanafunzi kuwasiliana na walimu na kujadili mada muhimu za masomo. 
  • Wanafunzi wasio na intaneti washauriwa kusoma vitabu vya kawaida na notsi za darasani.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa virusi vya Corona bado unaendelea kuitesa duniani huku viongozi, wanasayansi na watalaam wa afya wakiendelea kukuna vichwa kutafuta chanjo na dawa ya ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani. 

Katika nchi ambako umefika, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo kuzuia watu kusafiri, mikusanyiko na kuwaweka karantini wagonjwa waliombukizwa. 

Nchini Tanzania mpaka jana (Machi 19, 2020) kwa mujibu wa Wizara ya Afya kuna wagonjwa sita wa virusi hivyo, wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari hasa kuosha mikono kwa mara kwa mara. 

Pia Serikali imefunga shule zote za awali, msingi na sekondari pamoja vyuo, vyuo kati na vyuo vikuu na wanafunzi wametakiwa kukaa nyumbani kwa siku 30 ili kuwakinga na maambukizi hayo. 

Kwa sasa wanafunzi hawawezi tena kusoma na kupata maarifa kwa sababu miundombinu ya shule imefungwa na walimu nao hawawezi kuwaona moja kwa moja na wanafunzi. 

Lakini hakuna lililoharibika, kwa sababu teknolojia na mifumo ya elimu ya kidijitali ipo kuwawezesha wanafunzi kuendelea kusoma masomo ya darasani wakiwa nyumbani pasipo kumuhitaji mwalimu.

Wabunifu nchini Tanzania wamebuni programu tumishi za simu na kompyuta (Apps) ambazo zinaweza kumsaidia mwanafunzi kusoma kama ambavyo alikuwa anasoma darasani. Baadhi ya apps hizo ni pamoja na:

My Elimu

App ya MyELimu ni jukwaa la mtandaoni linalowaunganisha walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari kukutana na kujadili pamoja masomo.

Kupitia programu hiyo iliyoanzishwa na Mtanzania Given Edward, wanafunzi kutoka shule mbalimbali wanaweza kujumika na kufanya midahalo na kujadiliana masomo mbalimbali ili kuongeza ukaribu na uelewa wa masomo.

Hata wanafunzi wa shule moja wanaweza kuanzisha mijadala inayohusu masomo yao ili kuangalia mada za kusoma na kuwashirikisha walimu wao.

Uongozi wa My Elimu umesema watatoa msaada wa kitaalamu bure kwa shule na taasisi zozote za kielimu zitakazotaka kuendelea na masomo kwa njia ya mtandao katika kipindi hiki cha kuepuka mikusanyiko.

Shule Direct

Ni programu tumishi inayolenga kuwafikia wanafunzi wa shule za sekondari wa kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo kupitia program hiyo, mwanafunzi anaweza kujipatia maudhui ya kujifunzia na hata kujipima kwa kutumia mitihani ya majaribio.

Programu hiyo iliyoanzishwa na aliyekuwa mlimbwende wa Tanzania, Faraja Nyalandu inamuwezesha  mwanafunzi kufanya mitihani, kusahishiwa papo kwa papo na baada ya kufanya mtihani huo, mwanafunzi hupewa alama zake za ufaulu.

 

Mtabe

Programu hii imelenga zaidi wanafunzi wa sekondari na inatumia mfumo wa meseji za kawaida (SMS) na Apps zinazotumiwa na simu janja kupata maarifa kulingana na mahitaji na maeneo wanayoishi wanafunzi.

Hata wanafunzi wanaoishi vijijini ambako wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi vya kujifunzia, kupitia simu za kawaida wanaweza kupata maudhui ya kujifunzia kwenye simu zao.  

“Tunatumia teknolojia ya meseji na mfumo wa kiintelejensia uliotengenezwa kufikisha maudhui ya kujifunzia kwa wanafunzi wasioweza kununua vitabu na wale wasio unganishwa na intaneti” inasomeka sehemu ya maelezo katika tovuti ya Mtabe.


Soma zaidi: 


Smart Class

Ni jukwaa la mtandaoni linalowaunganisha wanafunzi na walimu wenye uzoefu katika sekta ya elimu ili kuwapatia maarifa sahihi wanayotaka.

Katika jukwaa hilo mwanafunzi ana uhuru wa kumchagua mwalimu anayemtaka kufundishwa naye ikizingatiwa kuwa jukwaa hilo lina walimu 1,000 binafsi wanaosubiri kuwafundisha wanafunzi.

ili kujiunga na madarasa hayo ya mtandaoni, mwanafunzi anapaswa kujisajili katika tovuti ya www.smartclass-tz.com na kuchagua  mwalimu wa somo unalotaka kusoma.

Baada ya hapo anamtumia ujumbe mfupi ndani ya smartclass kuhusu unachotaka kusoma. Kwa pamoja watapanga ratiba ya kusoma. 

Ubongo Kids

Kwa wanafunzi hasa wa madarasa ya awali, app hii inaweza kuwafaa kwa sababu inatumia katuni za 3D kuwatengenezea watoto maudhui yanayoweza kuwafanya kuelewa kwa haraka kupitia picha na sauti. 

Kupitia app hiyo, mtoto atasikiliza hadithi, kujifunza kusoma na kuandika huku akiburudika kwa katuni tofauti. 

Hapa mzazi anahitajika kumuongoza mtoto wake kuhakikisha maudhui anayoyapata yanaendana na umri wake.

Apps zingine za kimataifa ambazo wanafunzi wanaweza kupanua uelewa wao wa masomo ni pamoja na BrainPop, Curiosity Stream, Tynker, Outschool, Udemy, iReady, Beast Academy, Khan Academy, Creative Bug na Discovery Education ambazo zote zina maudhui ya elimu kulingana na uhitaji wa wanafunzi.

Wanafunzi wanaweza kusoma wakiwa nyumbani kupitia simu na kompyuta ikiwa wataunganishwa na teknolojia ya uhakika. Picha|Mtandao.

Wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu nao hili linawahusu

Kutokana na ukweli kuwa elimu ya chuo humuandaa mwanafunzi kwenda kufanya kazi, vipi vitabu vya mtandaoni ambavyo mwanafunzi anaweza kusoma popote alipo ili kujiongezea maarifa kipindi hiki cha mlipuko wa corona. 

Kwa sasa baadhi ya maduka ya mtandaoni na taasisi za elimu zimetoa fursa ya bure kwa wanafunzi kupata vitabu vya masomo wanayosomea ili kujielimisha zaidi. Kinachotakiwa ni simu janja, kompyuta na intaneti ili kusoma. 

Baadhi ya taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza kimechapisha machapisho zaidi ya 30,000 mtandaoni ya rejea, vitabu, majarida. 

Hata hivyo, kwa wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuifikia mifumo ya kidijitali bado wana nafasi kusoma notsi na vitabu vya kawaida mpaka pale Serikali itakapotoa mwongozo wa kurudi shuleni.