ARU yabeba jukumu kuratibu mafunzo tathmini ya maafa Afrika
Dar es Salaam. Moja ya changamoto inayoikabili miji na majiji yanayokuwa kwa kasi duniani likiwemo Jiji la Dar es Salaam ni maafa na majanga yatokanayo na nguvu za asili na shughuli za kibinadamu.
- Ni mafunzo ya kwanza kufanyika Tanzania huku yakivikutanisha vyuo vikuu 12 vya Afrika
- Wasomi kukuna vichwa kutafuta suluhisho la athari za maafa zinazotokea katika nchi za Afrika.
- Ujenzi holela wa miji katika ukanda wa Afrika Mashariki nao kujadiliwa katika mafunzo hayo.
Dar es Salaam. Moja ya changamoto inayoikabili miji na majiji yanayokuwa kwa kasi duniani likiwemo Jiji la Dar es Salaam ni maafa na majanga yatokanayo na nguvu za asili na shughuli za kibinadamu.
Maafa hayo hujitokeza katika sura mbalimbali ikiwemo vimbunga, mafuriko na mabadiliko ya mfumo wa joto na mvua ambayo yanachochewa zaidi na ujenzi wa viwanda, ongezeko la watu na ukuaji wa miji usiozingatia kanuni za mipango miji.
Maafa hayo yamekuwa na athari hasi ikiwemo uharibifu wa miundombinu, makazi na hata kusababisha vifo kwa viumbe hai wakiwemo binadamu.Lakini kila changamoto inayojitokeza katika uso wa dunia ina ufumbuzi wake,
Vyuo vikuu 12 vya Afrika kikiwemo Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wameazimia kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho la maafa yanayotokea katika majiji makubwa ya Afrika ambapo kazi kubwa wanayoifanya ni kufanya tathmini ya athari za maafa yanayotokea na kuhahakikisha hayazuii shughuli za maendeleo.
Katika hatua za awali wameandaa mafunzo ya kubadilishana uzoefu na kutoa mafunzo ya mbinu za namna ya kutathmini athari zitokanazo na maafa (Risk Methods School).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ARUA mafunzo hayo yanafanyika Tanzania kwa mara ya kwanza utashirikisha wanafunzi mbalimbali kutoka mashirika ya umoja wa Mataifa ambapo yanawaleta pamoja wasomi kutoka vyuo vikuu vya barani Afrika ili kuwa na sauti ya pamoja.
“Ushirikiamo huu ni wa aina yake unashirikisha wakufunzi kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa na vyuo vikuu sita kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, unakusudia kuongeza kasi ya makubaliano ya pamoja ya kimtazamo kati ya vyuo vikuu na jumuiya za kimataifa juu ya namna ya kukabiliana na athari za maafa,” inasomeka sehemu ya taarifa ya ARU.
Kupitia mafunzo hayo, wasomi wanajadili kwa kina mbinu za kukabiliana na maafa yanayochochewa na mabadiliko ya tabia nchi na ukuaji holela wa miji katika eneo la Afrika Mashariki.
ARU ambacho kimebeba jukumu la kuwa mwenye wa mafunzo hayo kimesema yanayofanyika kwa siku 22 hadi Septemba 21, 2018.
“Mafunzo hayo yatahudhuriwa na washiriki wapatao 38 kutoka nchi kumi na moja , tisa kati ya hizo zikiwa ni kutoka Bara la Afrika watakaojumuisha wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu pamoja na watendaji wanaotaka kuimarisha ujuzi wa kukabiliana na maafa’” inaeleza taarifa ya ARU.
Mada zinazotegemea kugonganisha vichwa vya wasomi hao ni pamoja na Athari za maafa mjini; Matumizi ya mifumo ya Taarifa za kijiografia (GIS), Athari za maafa kwenye sekta ya Afya, na namna ya kubaini Athari za Maafa ili kuboresha uwezo wa wataalamu wa fani mbalimbali za maafa.
Kufanikiwa kwa mafunzo hayo kunategemea zaidi ushirikiano kutoka kwa wadau wa maendeleo kama Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID/OFDA), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Afya Duniani (WHO), Ushirikiano mpya wa maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (The African Union/New Patnership for Africa’s Development’s Southern African Network of Water Centers of Excellence) na Chuo kikuu cha Stellenbosch.
Mafunzo kama hayo yanatarajiwa kufanyika tena katika Chuo Kikuu cha Gaston Berger, St. Louis, Sengal Februari, 2019.
Licha ya mafunzo kuwa na umuhimu katika kudhibiti athari za maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha usimamizi na udhibiti maafa kimeendelea kuratibu shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Pia kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa taarifa za tahadhari za awali ili kupunguza madhara ya maafa.